*Ni kutokana na hatua ya kutangaza wanafunzi wasiokuwa na sifa
SIKU moja baada ya Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) kutangaza majina ya wanafunzi zaidi ya 8,436 wa elimu ya juu wasio na sifa ya kusoma kiwango hicho cha elimu, baadhi ya wakuu wa vyuo hivyo wameishukia tume hiyo kwa kusema yenyewe ndiyo iliyodahili wanafunzi huku yenyewe ikisema iliratibu tu zoezi hilo.
Taarifa ya tume hiyo iliyotolewa Februari 20 mwaka huu na kuwekwa kwenye tovuti yake, ilisema majina hayo yanatoka kwenye vyuo 52 ambavyo uhakiki wa wanafunzi wake umekamilika na kwamba wanafunzi hao wanatakiwa kuthibitisha sifa zao kabla ya 28 Februari, 2017.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, wanafunzi ambao hawatafanya hivyo hawatatambuliwa na tume hiyo na hivyo kukosa sifa za uanafunzi.
CBE
Mkuu wa Chuo cha Biashara (CBE), Profesa Emmanuel Mjema, alisema wao walipelekewa taarifa na TCU kwamba kunatakiwa kufanyika kwa uhakiki wa wanafunzi wao na miezi miwili iliyopita wakaandaa taarifa hizo na kuziwasilisha kwao.
Alisema alishangaa kuona idadi ya wanafunzi 476 kuambiwa kuwa hawana sifa, jambo ambalo alisema ni la kushangaza.
Alisema ni makosa kusema wanafunzi hao hawana sifa wakati wanakidhi vigezo, huku akisema kuwa hali hiyo inatilia shaka.
“Tayari baada ya kuona taarifa hizo nimemtuma naibu wangu hapa na tayari ameshakwenda kwa Profesa Mageni wa TCU kwa kuwa wao wana data zote ambazo ziko sawa wao ndio walioleta wanafunzi hatujawahi fanya udahili sisi na si kweli kitu hiki.
“Yani ni hivi wewe umeniletea wanafunzi na nimewapokea halafu tena unasema huwatambui. Hayo ni makosa yao nafikiri katika kuhakiki mambo yao kwa ufasaha ,’’alisema Profesa Mjema .
Alisema taarifa zao wanazo miezi miwili iliyopita na hakuna hata mwanafunzi mwenye matatizo katika hayo majina waliyoyataja huku akihoji na kushangaa kuwa sijui imekuwaje.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Taaluma, Prof. Frolence Luoga, alisema chuo chake hakina tatizo na kwamba wanatoa elimu kwa kiwango cha ubora unaotakiwa.
Alisema wanaprogramu zilizothibitishwa na TCU na wanafunzi wao wamedahiliwa na kuthibitishwa pamoja na kufanyiwa ukaguzi, hivyo ameishangaa TCU kuja na taarifa hiyo.
“Uhakiki ulifanyika sasa sijui ni vigezo vipi vimetumika sijui lakini bado tunaendelea kulifanyia kazi suala hili kwa umakini mkubwa,’’ alisema.
Alisema lakini kuna wanafunzi ambao walidahiliwa pia siku za nyuma mfumo wa udahili haukuwa wa kupitia TCU na kabla hawajaanza udahili wa pamoja waombaji walikuwa wakifika chuoni hapo moja kwa moja wakitokea kidato cha sita na wengine vyuoni moja kwa moja na kujiunga .
Alisema wanafunzi wengine pia waliingia vyuoni hapo kwa kutumia program maalum ambazo zilikuwepo zaidi ya miaka 40 iliyopita.
Alisema pia kulikuwa na waombaji nje ya nchi walifika chuoni hapo walipatiwa mafunzo maalum kwa muda wa mwaka mmoja na kujiunga na chuo pia.
Alisema lakini hawafanyi kazi za kurudi nyuma na kuangalia usahihi kama walikuwa wamekosa sifa na wakawachukua kinachotakiwa kwa sasa ni kuangalia hatua gani zichukuliwe.
Makamu Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Agustino (SAUT) Dk. Padre Thadeus Mukamwa, kilichotajiwa wanafunzi wake 1,046 kukosa sifa amesema huo ni uonevu mkubwa na kuharibiana sifa za vyuo.
Alisema TCU ina sheria zake na kabla ya kuwatangaza wanafunzi hao walitakiwa kuweka bayana kwamba wamekosa wao kwa kuwa udahili wote umefanywa na wao wenyewe.
Alisema walikuwa na utaratibu hata kabla majina hayo hayajapitishwa na TCU wanakutana wakuu wote wa vyuo vyote nchini, Dar es Salaam, wanafanya mkutano wa pamoja na majadiliano kwa kuangalia historia ya vyuo vyao nakisha kudahili wanafunzi.
Alisema walipata kutoka TCU na kuwaambia kwamba vigezo vya wanafunzi hao ni questionable kwa kudai kuwa namba za wanafunzi hao hazieleweki wengine kuonyesha walisoma nje.
“Lakini hata kama walisoma nje walikuwa wakihakikiwa na wengi walifanya mafunzo mbalimbali ya mwaka mmoja ya dilpoloma ,cheti na waliruhusiwa kwa kutambua hilo sasa iweje leo,’’alisema.
Alisema inawashangaza kwa kuwa TCU ndio wanaofanya utaratibu wote na hata kwa kupokea kiasi cha shilingi 50,000 kutoka kwa wanafunzi hao kwa ajili ya uhakiki.
“Sasa sijui fedha walizokuwa wakipokea ilikuwa rushwa au laa na kama waliwapitisha wanafunzi hao walitoa rushwa kwanini walipokea fedha hizo,” alisema.
Alisema kuna wanafunzi wengine tayari wamemaliza kama kuna matatizo walitakiwa kuwa wanasema na kufanyiwa marekebisho lakini si kuwaambia kuwa hawana vigezo.
“TCU inakusanya data sasa wanashindwa kufanya uhakiki matokeo yao wanaharibu sifa za vyuo, kutoa lawama , wanaharibu muda wa wanafunzi ,fedha za mikopo pia,” alisema.
Alisema chuo hata siku moja hakitoi mikopo ni wao bodi ya mikopo ambao baada ya kuona wanastahili waliamua kuwapa mikopo hiyo leo kusema hawana sifa hawaoni kwamba wanaharibu sifa za vyuo na kuwachanganya wanafunzi bila kujali na wao ni binadamu pia.
Akizungumzia kauli za wakuu wa vyuo hivyo, Ofisa Habari wa TCU, Erdward Mkaku, alisema hakuna mahali wamesema kuwa wanafunzi hawana sifa bali tangazo limesema kwamba zoezi la uhakiki wa sifa limekamilika.
“Hakuna mahali tumesema wanafunzi hawana sifa, tangazo letu linasema zoezi la uhakiki limekamilika na kuna wanafunzi ambao wamedahiliwa katika programu ambazo hawana sifa nazo,’’ alisema.
Alisema orodha yote iliwasilishwa vyuo husika na kwamba kilichobakia sasa ni kwamba watakaojiona waende kwa kiongozi wao wa taluuma wa chuo chake kwa uhakiki .
Ofisa huyo alisema TCU inafanya kazi ya kuhakiki, lakini vyuo ndivyo vinavyodahili.