Warioba: Mgogoro Zanzibar ni ajenda ya kitaifa
Agatha Charles na Johanes Respichius
WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, amesema mgogoro wa kisiasa unaoendelea sasa visiwani Zanzibar ni tatizo la kitaifa.
Kauli hiyo aliitoa jana wakati wa kongamano la saba la Jumuiya ya Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), lililofanyika katika Ukumbi wa Nkrumah chuoni hapo.
Jaji Warioba ambaye pia ni rais wa jumuiya hiyo, alisema yapo masuala ya msingi yanayotakiwa kubebwa kitaifa badala ya kuyafanya ya kisiasa na mojawapo ni mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar.
“Zanzibar ni tatizo la kitaifa sio la kisiasa, tulifanye kitaifa ili liweze kutatuliwa,” alisisitiza Jaji Warioba.
Alisema kuna jazba katika masuala ya uchaguzi na pia ziliibuka wakati wa kukusanya maoni ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo alikuwa Mwenyekiti wake.
“Hili wananchi walilizungumza sana na tulilifanyia tathmini, tuliamini hata iundwe tume gani bado hupati matokeo sahihi, kama huondoi rushwa, udini, ukanda huwezi kuwa na uchaguzi huru na wa haki,” alisema Jaji Warioba.
Alisema suala la rushwa nalo linapaswa kuangaliwa kitaifa na kushughulikiwa tangu wakati wa uteuzi wa wagombea ndani ya chama ili kuweza kupata uchaguzi huru.
“Rushwa ni tatizo la kitaifa, hivi sasa Chadema kinaangalia CCM na CCM kinaangalia Chadema hilo ni tatizo,” alisema Jaji Warioba.
Naye mwanazuoni nguli, Profesa Issa Shivji, alizungumzia suala la kupinga urais mahakamani linapaswa kuruhusiwa kisheria.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. James Jesse aliyetoa mada kuhusu Mamlaka ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), alisema uhuru wa Tume hizo unapaswa kujadiliwa kila unapokaribia uchaguzi mkuu.
“Ili Tume ya Uchaguzi ipimwe kuwa ni huru lazima yaangaliwe malalamiko yaliyojitokeza katika uchaguzi husika, changamoto ikiwa ni uwezo wa kuendesha uchaguzi bila malalamiko.
“Vyama vya upinzani hususani wale waliokuwa wanaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), walikuwa wakihamasisha watu kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili hata wakiibiwa kura ziendelee kutosha na wawe washindi.
“Tukaingia kwenye uchaguzi wenyewe watu wakapiga kura zikahesabiwa na Tume ikamtangaza mshindi na Ukawa wakakataa matokeo kwamba si halali na kuendelea kusema kuwa Tume haipo huru katika kufanya mambo yake,” alisema Dk. Jesse.
Alisema ingawa uchaguzi ulikuwa na wagombea wanane, lakini hamasa kubwa ilikuwa kwa Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa hasa alipokihama CCM na kwenda upinzani.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Lupa Ramadhani, aliyetoa mada juu ya uchangiaji rushwa na migawanyiko katika siasa alisema uchaguzi wa mwaka jana ulikuwa na msisimko na kwa mara ya kwanza watu walizungumzia uwezekano wa CCM kuondoka madarakani kutokana na nguvu ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Katika kipengele cha gharama za uchaguzi, Dk. Ramadhani alisema Serikali ilijitahidi kuchangia gharama hizo na kuiepusha NEC na utegemezi wa misaada ya nje.
Hata hivyo, Dk. Ramadhani alisema changamoto moja wapo iliyobainishwa ni kutopatikana kirahisi kwa takwimu za mapato ya vyama.
“Takwimu za 2010-2015 zilionyesha kuwa CCM kilikuwa kikipata ruzuku ya asilimia 71, Chadema asilimia 18 na CUF 10. Fedha inashawishi sana katika uchaguzi, Serikali iliweka kiwango cha ukomo wa matumizi ambapo cha chini kwa jimbo ilikuwa Sh milioni 33 na cha juu Sh milioni 88, lakini bado haisemi tangu wakati wa kuzunguka kwenye chama kiasi gani kitumike,” alisema Dk. Ramadhani.
Naye mchambuzi wa mada hiyo ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Alexander Makulilo, alisema sheria namba 6 ya mwaka 2010 ya gharama za uchaguzi inaficha taarifa za mapato na kuweka wazi ruzuku pekee.
“Vyama vya siasa vinategemea zaidi misaada na si wanachama wake. Mwaka 1992 Tume ya Jaji Francis Nyalali ilipendekeza CCM kuanza upya na kugawa mafanikio yake serikalini ili kuanza kama vyama vingine vipya kwani tangu 1978 kilikuwa kinapata ruzuku ya asilimia 78,” alisema Dk. Makulilo.
Mada nyingine kuhusu Vyombo vya Habari na Azaki katika uchaguzi uliopita ilitolewa na Dk. Ayub Rioba, ambapo alisema hamasa iliyojitokeza kwenye mchakato wa uchaguzi kwa kiasi kikubwa ulichangiwa na elimu ya hali ya juu iliyotolewa na vyombo vya habari pamoja na Azaki mbalimbali za kiraia.
“Ingawa watu wanasema kuwa ujio wa intaneti umeleta mabadiliko kati ya sekta ya habari lakini moja ya hamasa ya watu kujitokeza katika uchaguzi ni vyombo vya habari,” alisema Dk. Rioba.
Aidha, alisema vyombo vya habari vikumbuke kanuni kama maadili, ukweli, kuandika habari kwa usahihi na kuhakikisha taarifa inayotolewa inakamilika, kutenda haki sawa pia kupunguza makali ya migogoro.
“Vyombo vya habari vya sasa vinafanya kazi kubwa sio kama vya zamani, vimekuwa vikitoa fursa kwa mahojiano kwa watu wote ikiwa ni pamoja na kufuatilia utendaji wa kazi wa NEC na ZEC, kuangalia changamoto na kuwahabarisha wananchi ni kitu gani kunaendelea,” alisema.
Kwa upande wa mwakilishi wa NEC, Profesa Amon Chaliga, alisema malalamiko kuhusu tume hiyo ameyasikia na hivyo atayawakilisha.
Alisema matokeo yaliyotangazwa ni sahihi kulingana na kila mmoja alichokipata katika uchaguzi huo kwani yalikuwa wazi yakibandikwa vituoni.
Naye Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, Sixtus Nyahoza, alisema ingawa wana sheria ya gharama za uchaguzi lakini kila mmoja anapaswa kuwa na maadili na uzalendo.
Alisema sheria hiyo ya gharama za uchaguzi ina upungufu ambao unashughulikiwa kwani imeweka ukomo wakati wa kampeni lakini haina ukomo wakati wa nia.