23.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Uchaguzi Zanzibar kurudiwa Machi 20

am4Na Khelef Nassor, Zanzibar

HATIMAYE Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) jana imetangaza kuwa Machi 20, mwaka huu, ndiyo siku ambayo marudio ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar yatafanyika.

Tangazo hilo limetolewa jana na Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, kupitia Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC), ikiwa ni takribani miezi mitatu sasa baada ya kufutwa kwa uchaguzi mkuu huo kwa madai ya kujitokeza dosari mbalimbali wakati wa upigaji na uhesabuji wa kura.

Jecha amesema marudio ya uchaguzi mkuu huo yatawahusisha wagombea wa nafasi ya urais, uwakilishi na udiwani na alitoa wito kwa wananchi wa visiwa hivyo kuendelea kudumisha amani hadi hapo uchaguzi utakapofanyika.

Kuitishwa kwa uchaguzi huo wa marudio huenda kukawakutanisha tena mahasimu wawili wa kisiasa wa Zanzibar, Rais Ali Mohamed Shein wa CCM na Maalim Seif Sharif Hamad, ambao katika uchaguzi wa awali kila mmoja alitamba kuibuka na ushindi.

Wakati Jecha akitoa tangazo hilo, Chama cha Wananchi (CUF) kinachoundwa na vyama siasa vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kimekwishatoa msimamo kuwa hakitashiriki marudio ya uchaguzi huo, huku vyama vingine vikiwa bado kimya.

Kwa nyakati tofauti, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK), Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF, amekaririwa akieleza kuwa Jecha alikiuka sheria kwa kutangaza kufutwa kwa uchaguzi mkuu kwa sababu hana mamlaka hayo, hivyo chama chake hakiwezi kushiriki marudio ya uchaguzi.

Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF, Ismail Jussa Ladhu, alipoulizwa hivi karibuni kuhusu msimamo huo wa bosi wake, alisema chama chake hakiwezi kutoa tamko rasmi hadi pale viongozi wakuu watakapoketi kulijadili.

Kauli hiyo ya Jussa iliungwa mkono pia na Mwenyekiti wa Tanzania Labour Part (Zanzibar), Mkadam Hamad Mkadam, aliyeeleza kuwa uamuzi kuhusu jambo hilo unahitaji kutolewa baada ya kupitishwa na vikao vya vyama ambavyo vina uhalali wa kushiriki uchaguzi mkuu.

“Unajua ndugu mwandishi hili si suala la kukurupuka, ni lazima viongozi tukutane pamoja na tulijadili halafu ndiyo tutatoa tamko rasmi kama chama,” alisema Jussa.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima (AFP), Said Soud Said, amesema chama chake kimepokea tangazo la Jecha kwa furaha kubwa.

Alisema AFP kinaipongeza ZEC kwa kuzingatia agizo la Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, aliyoitoa wakati wa maadhimisho ya siku ya Mapinduzi, lililoitaka tume hiyo kutangaza siku ya marudio ya uchaguzi.

“Sisi kama chama tumezipokea kwa furaha taarifa hizo za Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi na hakuna ubishi kwamba uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 uligubikwa na kasoro nyingi kama zilivyotajwa na Mwenyekiti mwenyewe.

“Kwa hivyo chama chetu hakina sababu ya kutoshiriki kwenye uchaguzi huo,” alisema Said.

Jitihada za kumpata msemaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuzungumzia tangazo hilo hazikuweza kufanikiwa hadi tunakwenda mitamboni.

Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana visiwani Zanzibar ilifutwa na ZEC na kuibua mgogoro wa kisiasa visiwani humo, baada ya CUF kupinga hatua hiyo, huku CCM na baadhi ya vyama vingine vikiiunga mkono.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles