23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

IPTL yajivua zigo la Escrow

Mwanasheria wa kampuni ya IPTL/PAP, Joseph Makandege, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu nafasi ya makampuni hayo kwenye hukumu iliyoamuliwa na Mahakama ya Kimataifa kuhusu kesi ya kutaka Tanesco iilipe Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong. Kushoto ni Mwenyekiti Mtendaji wa IPTL’s Rajiv Bhesania.
Mwanasheria wa kampuni ya IPTL/PAP, Joseph Makandege, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu nafasi ya makampuni hayo kwenye hukumu iliyoamuliwa na Mahakama ya Kimataifa kuhusu kesi ya kutaka Tanesco iilipe Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong. Kushoto ni Mwenyekiti Mtendaji wa IPTL’s Rajiv Bhesania.

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM

SAKATA la Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), kugeuziwa kibao kwa kutakiwa kurejesha zaidi ya Dola za Marekani milioni 100 ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 216.2 kwa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), limezidi kuchukua sura mpya baada uongozi wa kampuni hiyo kuibuka.

Kuibuka kwa viongozi hao kumekuja siku chache baada ya Wakili wa Tanesco, kueleza hatua watakazochukua kuhusu uamuzi huo baadaya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara (ICSID), uliotolewa Septemba 12 mwaka huu unaoitaka Tanesco kuilipa Standard Chartered ya Hong Kong (SCB-HK) Dola za Marekani milioni 148.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Mwenyekiti ambaye pia ni Mwanasheria wa Kampuni  wa IPTL,  Joseph Makandege alisema hawatambui madai ya Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong (SCB-HK) kama mdai na wala hawana haki kwa mujibu wa sheria.

Kutokana na hali hiyo alisema inaungana na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kukata rufaa katika Mahakama ya ICSID kwani hukumu iliyotolewa ina mapungufu mengi ya kisheria.

Licha ya uamuzi huo Makandege alisema IPTL haikulipwa kwa kutumia viwango vya zamani bali walilipwa kutokana na umeme waliouuza kwa Tanesco na si vinginevyo.

Alisema watu wasifanye makosa kuilipa benki hiyo kwani inachotaka kufanya ni kitendo cha utapeli kwa msukumo wa kampuni za mabeberu.

“Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong hawastahili kulipwa fedha na Watanzania kwani hawastahili kwa mujibu wa sheria nasi kama IPTL/PAP hatuwatambui na hawana haki ya kutuzungumzia. Na ndiyo maana wameamua kukimbia mahakama zetu za ndani na kukimbili nje, hawa wana msukumo wa mabeberu wenye nia ovu.

“Kwa uamuzi huu wenye utata uliotolewa na ICSID ni wazi Standard Chartered walikuwa na nia ovu, ninasema hivyo kwa sababu tangu Septemba 5, mwaka 2013 suala hili liliamuriwa vizuri chini ya Jaji Utamwa (John) na IPTL ikashinda kesi na kutwaa uongozi.

“Na hili si la kwanza kwani Aprili 3, 2014  tulifungua shauri namba 60 chini ya Jaji Dk. Fauz Twalib la kuitaka Mahakama itamke kwamba  benki ya Standard Chartered Hong Kong si wadeni wetu, tena awali waliibuka na hoja kwamba hawasikilizwi na Mahakama zetu za ndani kwa wakati  ambapo shauri hilo lilipangiwa kusikilizwa mfululizo.

“Lakini pia dai letu lingine tuliomba Mahakama Kuu itupe nafuu ya Standard kutulipa gharama kama fidia ya Dola za Marekani bilioni 3.240 ambapo hata tuzo waliopewa na ICSID eti wanataka walipwe Dola za Marekani milioni 148 na kama wakitulipa fedha zetu hata madai yao yaingia humo nab ado kuna fedha nyingine inabidi watupatiwe sisi,” alisema Makandege

Wakili huyo ambaye alikuwa akizungumza kwa niaba ya mmiliki wa IPTL/PAP, Harbindar Singh Sethi mwenye makazi yake hapa nchini na Afrika Kusini, alisema licha ya mahakama kutoa uamuzi wataendelea kusimamia uamuzi huo wa kutomtambua mtu anayeitwa Martha Renju wala Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong.

“Sisi msimamo wetu kama IPTL/PAP tunasema hadharani kwamba hatuitambua Benki ya Standard Chartered ambao hawa kila wakati wamekuwa wakikimbia mahakama zetu za ndani na kukimbilia nje na hata hukumu hii ya tuzo ina viashiria vya mabeberu.

“Tuzo husika waliyopewa ni dhahiri Standard Chartered ni batili kwa mujibu wa sheria. Wao ni kina nani hadi wakafungie kesi kwa niaba yetu. Hii ni kesi ya ngedere imepelekwa kwa nyani,” alisema

Kutolewa fedha za Escrow

Akizungumzia mchakato wa kutolewa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow, Makandege alisema mchakato wa kutolewa kwa fedha hizo ulikuwa wa kihalali kwa mujibu wa sheria za nchi.

Alisema Julai 5, mwaka 2006, Serikali na IPTL waliingia mkataba wa Escrow ambao ulipelekea kutolewa kwa fedha hizo kwenye akaunti hiyo iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) bila kuwahusisha Benki ya Standard Chartered.

“Oktoba 8, 2010 IPTL na Tanesco kwa kuzingatia kipengele cha 10 cha mkataba huo ambayo kinaeleza kuwa endapo kuna mgogoro baina ya pande hizo mbili wahusika watakutana na kujadiliana  na hatua ya kuafikiana itahesabika kuisha kwa mgogoro.

“Hata ripoti mbalimbali ikiwemo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hakuna sehemu yoyote inayoeleza kuwa zile fedha ni za umma. Hata ICSID imetoa hukumu na kusema si fedha za Serikali lakini wanakiri zilitolewa kihalali ingawa hawakupewa Standard na kama kungelikuwa na mgogoro fedha zile singetolewa,” alisema

Kunyang’anywa mitambo

Alipoulizwa kuwa hatua ya suala hili kugubikwa na utata na utekelezaji wa maazimio manane ya Bunge la 10 likiwemo la wao kunyang’anywa mtambo, Makandege alisema wanajua kuna watu hivi sasa wanahaingika wakitaka kuona suala hilo linafanyika.

Pamoja na hali hiyo alisema kuwa mitambo bado ni mali yao kwa mujibu wa sheria na hakuna hatua itakayowafanya wafanikiwe watu hao ambao hakuwataja.

“Tunajua kuna watu hivi sasa wanataka kuona suala hili likitekelezwa ikiwemo IPTL kunyang’anywa mtambo, ninawaambia hakuna jambo kama hilo, nasi kila wakati tumekuwa wazi ikiwemo kulaani maazimio ya Bunge ambayo ni wazi yalikuwa na lengo la kukimbiza wawekezaji wazawa. Suala hili hata Rais mstaafu (Jakaya Kikwete) aliliweka wazi kwa nini lianze sasa baada ya mjadala wake kufungwa,” alisema.

Kauli ya Mwanasheria Tanesco

Wiki ilipita Wakili wa Tanesco, Richard Rweyongeza alisema walichokuwa wanabishania mahakamani si Tanesco kulipa bali walikuwa wanabishania italipa kiasi gani na analipwa nani.

Kauli hiyo aliitoa alipokuwa akizungumza na MTANZANIA ambapo alichambua hoja mbalimbali ikiwemo uamuzi wa ICSID kuhusu tuzo waliyoipa Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong.

“ Kabla hatujaingia katika kutetea kesi hiyo, mwaka 2014 mahakama hiyo ilisema inayo madaraka na ikaamuru Tanesco kuilipa  SCB-HK.

“Sisi tuliingia kutetea baada ya uamuzi huo Mei, 2014 tukaomba hesabu zifanyike upya kwa malekezo yaliyotolewa na mahakama hiyo ili kujua deni halisi, hesabu zilipofanyika kwa mtaji wa mwekezaji walichukua mkopo wakahesabu kuwa ni mtaji, hatua hiyo ilikataliwa na mahakama.

“Kabla ya hesabu kufanyika ndipo ikaingia suala la akaunti ya Tegeta Escrow, fedha zilipochukuliwa katika akaunti hiyo, SCB-HK wakabadilika wakasema hakuna haja ya kufanya hesabu upya kwa sababu Tanesco wamekubali viwango hivyo ndio sababu waliwalipa IPTL.

“Tulibishania hoja hiyo ya kulipa kwa viwango vya zamani ikaamuliwa hesabu zifanyike upya, mahakama ilikubali hesabu zifanyike kwa kutumia mkopo wa wana hisa.

“Baada ya kuamuru hivyo deni likashuka kutoka walichokuwa wakidai Dola za Marekani milioni 369 hadi kuamuliwa kulipa Dola za Marekani milioni 148,”anasema Wakili Rweyongeza.

Alisema IPTL walilipwa Dola za Marekani milioni 246 kwa kutumia viwango vya zamani na kwamba uamuzi uliotolewa unaanza kutumika katika kipindi chote ambacho Tanesco ilikuwa inadaiwa mpaka mwaka 2015.

“Kutokana na hesabu hizo gharama ilikuwa chini, IPTL ililipwa zaidi hivyo inatakiwa kurejesha Dola za Marekani zaidi ya milioni 100 kwa Tanesco,”alisema.

Rweyongeza alisema walipendekeza SCB-HK wadai fedha zao kwa IPTL lakini mahakama hiyo ilikataa na kuamuru Tanesco ndio walipe hivyo kwa mtazamo wa kawaida IPTL inatakiwa kurejesha fedha kwa shirika hilo.

Katika kuhitimisha mahakama hiyo ilisema pande zote mbili zinazopingana zilishinda katika maeneo muhimu waliyokuwa wakibishania lakini zilipoteza katika hoja zingine.

Baada ya kumaliza kusikiliza kesi hiyo mahakama iliamuru pande hizo mbili kulipa gharama za usuluhishi na zingine kwa viwango sawa.

Malipo hayo na anayelipwa katika mabano ni Dola za Marekani 254,775.02 (Profesa MC Rae), Dola 171,278.36 (Profesa Douglas) na Dola 370,126.76 kwa ajili ya Profesa Stem.

Gharama zingine zilizokadiriwa moja kwa moja ni Dola za Marekani 157,336.26 na gharama za utawala wa mahakama hiyo Dola za Marekani 180,000 ambapo jumla ya gharama zote wanazotakiwa kulipa Tanesco na SCB-HK ni Dola za Marekani 1,133,516.42.

Fedha hizo zilitolewa na kwenda kwa Kampuni ya Pan Africa Power Solutions Tanzania Limited (PAP) kwenda kwa mmiliki wake, Harbindar Singh Sethi mwenye makazi yake hapa nchini na Afrika Kusini.

Katika kesi hiyo Tanesco ilikuwa inawakilishwa na mawakili wa kampuni za R.K Rweyongeza & Advocates na Crax Law Partners.

Chanzo cha Escrow

Mwanzoni mwa miaka ya 1990  nchi ilikuwa na upungufu wa umeme kutokana na upungufu wa maji kwenye mabwawa, ambapo 1994 serikali ilitoa kazi ya uwekezaji kwa IPTL iliyokuwa ikimilikiwa na VIP ya Tanzania iliyokuwa na asilimia 30 na Mechmar ya Malaysia yenye asilimia 70.

Kutokana na hali hiyo Tanesco na IPTL walisainiana mkataba wa miaka 20, hata hivyo uzalishaji haukuanza mara moja kutokana na mgogoro ulioibuka baina yao (Tanesco na IPTL) .

Mwaka 2002  IPTL ilianza kuzalisha umeme na mkataba ukaanza kuhasabiwa hapo, lakini kutokana na mgogoro ikafunguliwa akaunti ya Escrow na mwaka 2004 Tanesco ilifungua shauri kupinga tozo la Capacity Charge

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles