23.7 C
Dar es Salaam
Sunday, August 14, 2022

Sinema ya CUF yazidi kunoga

Profesa Ibrahim Lipumba
Profesa Ibrahim Lipumba

Veronica Romwald na Patricia Kimelemeta,

HII ni sinema. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF), kuitisha kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa, ili kumhoji mwenyekiti aliyerudishwa madarakani, Profesa Ibrahim Lipumba.

Wakati wajumbe wa baraza hilo wakijiandaa kukutana kesho visiwani Zanzibar kutekeleza mpango huo, jana kutwa nzima, Profesa Lipumba alikuwa na kikao kizito na walinzi wa chama hicho (Blue Guard) makao makuu ya chama hicho Buguruni, Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui ilisema baraza hilo, linamtaka Profesa Lipumba afike mbele ya kikao hicho ili  ajieleze na kujitetea kwanini asichukuliwe hatua za kinidhamu kutokana na kitendo chake cha kuvamia ofisi za makao makuu na kusababisha uharibifu wa mali.

“Kamati haijakubaliana na maoni na ushauri uliotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi juu ya Lipumba. Ilikutana jana (juzi)  kwa kikao cha dharura ofisi za Makao Makuu, Zanzibar na kujadili taarifa ya msajili,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo, ilisema  kamati pia ilijadili  kitendo cha uvamizi wa ofisi za Buguruni, kilichofanywa na Profesa Lipumba akiwa na kundi  la vijana ambao si wanachama wa CUF.

Alisema baada ya kikao kupitia maoni ya msajili, kamati iliamua kukataa na kupinga kwa hoja thabiti ushauri na maoni aliyoyapendekeza na badala yake inaendelea kusimamia maamuzi ya Mkutano Mkuu Maalumu  Taifa uliofanyika Agosti 21, mwaka huu.

“Katika mkutano ule, wajumbe walikubali Lipumba kujiuzulu kama mwenyekiti wa chama na katika kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa cha Agosti 28, mwaka huu, waliridhia kuwasimamisha uanachama Lipumba, Magdalena Sakaya, Maftaha Nachuma, Abdul Kambaya, Masoudi Mhina, Thomas Malima, Ashura Mustafa, Kapasha H. Kapasha, Musa Haji Kombo, Habibu Mnyaa, Haroub Shamis na kumfukuza uanachama Shashu Lugeye,” alisema.

Taarifa hiyo, ilisema Katiba ya CUF  haina kifungu chochote kinachompa mamlaka Msajili wa Vyama vya Siasa kupokea rufaa kuhusiana na uamuzi wa vikao vya chama na kubatilisha uamuzi wa vikao halali.

“Kutokana na kitendo cha kuvamia ofisi za Buguruni na kusababisha uharibifu wa mali za chama, kamati kwa mujibu wa ibara ya 85(5) na ibara ya 108 ya Katiba ya CUF ya mwaka 1992 Toleo la mwaka 2014 imeitisha kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa Septemba 27, mwaka huu saa nne asubuhi ofisi za Zanzibar.

“Kwa mujibu wa Ibara ya 12 (6), (7) na (16) ya Katiba ya CUF ya mwaka 1992 , toleo la mwaka 2014, Kamati imeandaa ajenda ya kumfikisha Lipumba mbele ya Baraza Kuu na atatakiwa kujieleza na kujitetea kwa nini baraza lisimchukulie hatua za kinidhamu kwa matendo yake aliyoyafanya jana (juzi),” alisema.

Katika taarifa hiyo, Mazrui alisema ibara hizo zinaeleza juu ya kulinda heshima ya chama kwa kuwa na tabia njema, kutekeleza masharti ya Katiba, kutii kanuni za sheria na sheria ndogondogo za serikali iliyoundwa kihalali na.

Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba jana kutwa nzima alikuwa na kikao na walinzi wa chama hicho, (Blue Guard).

Pamoja na mambo mengine, kikao hicho kilikuwa  na ajenda mbili ikiwamo ya kuimarisha ulinzi katika ofisi zote za chama na kujadili mali za chama ambazo ni pamoja na magari saba na kompyuta zilizoibwa wakati wa vurugu.

Tamko la Kambaya

Pamoja na hali hiyo jana Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma, Abdul Kambaya, alitoa tamko la kuwataka wanachama wa CUF kuwa watulivu kwa ajili ya kukijenga chama hicho.

Alisema pamoja na hali hiyo CUF ni taasisi na sio eneo la mtu fulani kwani tamko la Naibu Katibu Mkuu CUF Zanzibar, Nassor Hamed Mazrui la kuukataa ushauri wa Msajili wa Vyama vya Siasa uliotolewa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2002 ni la upotoshaji.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2002, sehemu ya 20, tamko la msajili ni uamuzi na si tu ushauri kama wanavyotaka kupotosha. Uamuzi huu ni mzito kwa kiwango ambacho hata mahakama inaweza tu kuurejea lakini si kuufuta (rejea ibara ya 20(2).

“Ieleweke kwamba hii si mara kwanza msajili kufanya maamuzi kama haya. Mtakumbuka kwamba aliyekuwa Mwenyekiti wetu Ndugu James Mapalala alienda kwa msajili baada ya kufukuzwa.

“Lakini msajili alitoa uamuzi kwamba maamuzi yale yalikuwa sahihi Kwa kuwa yalifuata katiba yetu ya CUF. Sasa iweje hawa wenzetu leo waseme kwamba ule ni ushauri tu?,” alisema na kuhoji Kambaya ambaye ni mmoja wa wanachama waliosimamishwa na kikao cha Baraza Kuu la Uongozi.

Alisema kilichofanyika Vuga Zanzibar ni uasi wa hali ya juu, hivyo watakaa kama chama kutafakari hatua za kuchukua baada ya kuzuia uasi na kile alichodai mapinduzi haramu kwa chama hicho.

“Sasa kazi yetu ni kujenga chama. Wenzetu walioendesha uasi wana hiari ya kujirudi ili tuungane kufanya kazi ya ujenzi wa chama na kuhudumia wananchi katika maeneo mbalimbali ambapo chama kimepewa ridhaa ya kuongoza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,712FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles