29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Siasa yetu ifuate lipi?

Na ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

NI miaka 28 tangu Taifa letu liingia katika mfumo wa demokrasia wa vyama vingi, siasa imekuwa ikifanyika katika mazingira tofauti kutegemea na utawala uliopo madarakani.

Ikumbukwe kwamba, Taifa liliingia katika mfumo huo chini ya utawala wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi ambaye ndiye alisimamia Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi, alipokuwa akimaliza muda wake mwaka 1995.

Rais Mwinyi aliongoza katika kipindi ambacho vuguvugu la kuhitaji demokrasia ya vyama vingi likiwa limepamba moto na kufikia kiwango cha juu kabisa hivyo ukatolewa uamuzi wa kuruhusu mfumo huo kufanya kazi, japokuwa katika uchanga wake, vyama vya siasa vilipata nafasi ya kujiimarisha mfano  NCCR-Mageuzi kupata viti vya ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa kwanza mwaka 1995.

Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alipokea kijiti baada ya Uchaguzi Mkuu wa 1995, utawala wake haukuwa rafiki sana kwa vyama vya yupinzani na vyombo vya habari, lakini alivipa vyama nafasi ya kutekeleza majukumu yake yanayoruhusiwa kikatiba.

Mkapa alimaliza muda wake na kukabidhi kijiti kwa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, ambaye katika awamu yake, hakuwapa wapinzani uhuru usio na mipaka, bali aliwapa nafasi ya kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Katiba na nafasi ya kukaa nao meza moja na kuwasikiliza pale walipoibua tuhuma au malalamiko dhidi ya Serikali.

Ni wazi kwamba, nafasi ya vyama vya siasa katika siasa za Tanzania ni kubwa na kwa kuwa vyama hivi vimeanzishwa na Watanzania kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi, ni haki ya wanasiasa kufanya siasa na kujenga vyama vyao katika maeneo yote nchini.

Siasa ambayo inahusisha mikutano ya ndani kwaajili ya kuweka mikakati ya kujenga chama na mikutano ya hadhara kwa ajili ya kuwafikia watu na kutoa ushawishi wa kutafuta kuungwa mkono inakuwa na maana iwapo mikutano ya hadhara inapewa nafasi yake stahiki.

Mikutano ya hadhara kwa wanasiasa ni miongoni mwa nyenzo inayotumiwa kuwashawishi wananchi ili waunge mkono vyama vya upinzani lakini tangu mwanzoni mwa mwaka 2016 wabunge na wanasiasa wanaruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara katika majimbo wanayowakilisha, na si vinginevyo na mara nyingi hata hao wanapotaka kufanya mikutano hiyo wanatakiwa kuomba vibali polisi, ambavyo havitolewi.

Hali hii imepunguza kasi ya upinzani kuwafikia wananchi. Tofauti na ilivyokuwa katika awamu za uongozi zilizopita, ambapo tumeshuhudia wanasiasa wakiendesha vuguvugu mfano, Chadema waliendesha Operesheni Sangara katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, Movement For Change (M4C) kote nchini.

Matunda ya mikutano hiyo ndiyo yalichochea kuongezeka idadi ya wabunge wa upinzani kufika 116 baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Katika hili, Akizungumza na MTANZANIA, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema anasema tatizo lililopo vyombo vya dola hasa jeshi la polisi linaamua kwa makusudi kuweka kando maelekezo ya sheria inayovipa vyama vya siasa uhuru wa vyama, hivyo watahakikisha viongozi wakuu wanatumia haki yao kupitia sheria namba 5 ya vyama vya siasa kufanya mikutano.

Anasema kimsingi sheria inawataka viongozi wa siasa kutoa taarifa polisi ili wapate ulinzi na si kuomba kibali na ndivyo watakavyofanya kulitaka jeshi la polisi kusimama kwenye sheria na lisitake kujificha kwenye matamko yasiyo ya kisheria.

 “Polisi wanaposema wanaoruhusiwa ni wabunge kwenye majimbo yao wanatumia sheria gani? Mbona Dk. Bashiru Ally anazunguka huko akifanya kampeni, yeye ni mbunge wa wapi, au polepole anapozunguka huko kufanya kampeni yeye ni mbunge wa wapi?” anahoji.

Anasema viongozi wa Chadema watafuata taratibu za kisheria na watatumia haki yao ya kikatiba kufanya mikutano hiyo katika maeneo yote ya nchi hasa kipindi hiki ambacho Taifa linaelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji, anasema si kwamba Chadema imerudi nyuma kufanya mikutano ya hadhara, bali walikuwa wametingwa na majukumu mengine lakini wanaandaa utaratibu.

“Tumeona CCM huko Karatu wamefanya mikutano ya hadhara na kukashifu. Sisi tulishaamua tutafanya mikutano ya hadhara na mchana peupe kwani kufanya mikutano si jinai.

“Tunaandaa ratiba, niwatake wapenda demokrasia duniani kupinga kuingiliwa. Tuna sera zetu, hatutakuwa na muda mchafu wa kupambana na watu,” anasema Dk. Mashinji.

Wakati Chadema wakieleza kuwa nafasi ya polisi si kutoa vibali vya mikutano bali ni kupokea taarifa ya mkutano na kutoa ulinzi, Msemaji wa Polisi, DCP Ahmed Msangi anasema vyama vya upinzani havijazuiwa kufanya mikutano ya hadhara ila vinatakiwa kufuata taratibu za kisheria.

Anasema taratibu hizo ziko wazi na kwamba viongozi wote wa vyama vya siasa wakiwemo Chadema wanazijua, kwa hiyo hakuna anayezuiwa kufanya mikutano hiyo iwapo watazifuata.

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili, DCP Msangi anasema utaratibu wa kisheria unawataka viongozi wa vyama vya siasa kuwasilisha barua ya kuomba kibali ndani ya saa 48 kabla ya kufanyika kwa mikutano hiyo.

“Sisi wakifuata taratibu zote zinazoelekezwa kisheria hatuna wasiwasi, watume hizo barua saa 48 kabla ya kufanyika kwa mkutano na sisi tunatoa vibali. Ila ikumbukwe kuwa ni kila mtu kwenye jimbo lake. Ni kwamba hatujazuia mtu kufanya mkutano kwenye jimbo lake,” anasema.

Kuhusu nafasi ya viongozi wakuu wa vyama kitaifa ambao wanatakiwa kujenga chama maeneo yote ya nchi hivyo kuhitajika kufanya mikutano ya hadhara kwenye maeneo yoyote alijibu kwa ufupi; “Hao wote wanajua utaratibu na walishapekwa maelekezo”.

Anasema katika utaratibu huo wanatakiwa kufuata sheria na maelekezo ya kufanya mikutano katika majimbo na kata zao na si vinginevyo.

Katika ufuatiliaji, kinachoonekana ni kuwepo kwa ukinzani baina ya matamshi ya viongozi, sheria za nchi na wasimamizi ambao ni watendaji hasa jeshi la polisi ambalo japokuwa wapinzani wanadai suala la mikutano lipo kwa mujibu wa sheria, Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini ambaye ndiye mlezi na mwangalizi wa vyama vyote amekuwa kimya katika hili.

Wataalamu wa siasa wanasemaje?

Mtaalamu wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), Dk. Richard Mbunda anakaririwa na BBC akisema “Haki za vyama vya siasa zipo kwenye Katiba. Na zinaungwa mkono na sheria nyingine za Bunge kuhusu vyama vya siasa na haki za uhuru wa kisiasa kwa ujumla wake. Lakini pale ambapo watawala wanazikanyaga haki kama hizi kwa makusudi, vyama vya upinzani vinafanya nini?”

Anaongeza: “Mosi, tunategemea mapambano ya kisheria. Mapambano haya yakisimamiwa na upinzani. Tunategemea kuona wanasiasa wa upinzani wakiomba ‘Tafsiri ya Mahakama’ kulingana na kauli kama za kuzuia mikutano ya siasa kitaifa. Na watafsiri sheria wetu nchini wangewekwa kwenye kipimo cha mizani,

“Pili, uzoefu wangu wa tafiti za migogoro Zanzibar unanikumbusha kuwa unapolegeza mapambano ndipo unapokuwa kwenye kona ya kushindwa. Ni lazima upambane ili uungwe mkono hata ya jumuiya ya Kimataifa.”

“Chukua mfano wa tamko la Ubalozi wa Marekani hapa Tanzania kuhusiana na chaguzi ndogo. Lilikuwa tamko muhimu sana kwa upinzani lakini lilikosa maana kwa kuwa upinzani wenyewe umelala.

Sisemi hivi kama mpinzani wa vyama vya upinzani, lakini ninatazama siasa kisayansi, na kama mwanataaluma nafahamu dhahiri kuwa hata operesheni Ukuta ulikuwa mpango mzuri. Walipoogopa tu wameijengea serikali nguvu ya kuwabana zaidi.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles