27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mfanyabiashara kizimbani kwa mbegu feki

NA KENNETH NGELESI-MBEYA

TAASISI ya Kuzuia na Udhibiti Mbegu nchini (TOSCI), imemfikisha mahakamani mfanyabiashara wa pembejeo, Fortunatus Lutanikwa, mkazi wa Uyole jijini Mbeya, kwa tuhuma za kuwauzia wakulima mbegu feki na kughushi nembo ya taasisi hiyo na makampuni yanayozalisha mbegu nchini.

Lutanikwa ambaye anajihusisha na uuzaji wa pembejeo katika eneo la Uyole jijini hapa, amepandishwa kizimbani katika mahakama ya hakimu mkazi Mkoa wa Mbeya ambako amesomewa mashtaka matatu ya kuuza mbegu feki, kuuza pembejeo bila kuwa na leseni na kughushi nembo za makampuni yanayozalisha mbegu.

Akimsomea mashtaka ya kesi namba 73 /2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya, Paul Ntumo, Wakili wa Serikali, Hannarose Kasambala, aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa alikamatwa akiuza mbegu feki kinyume cha sheria ya mbegu namba 18 kifungu cha 13(1) na kifungu cha 26(1) na (2).

Wakili Kasambala, alisema mshtakiwa alikamatwa na maofisa ukaguzi wa mbegu kutoka Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu nchini (TOSCI), Januari 29, mwaka huu akiwa dukani kwake maeneo ya Uyole hapa.

Ilidaiwa kuwa mahakamani hapo kuwa mshtakiwa huyo siku hiyo alikutwa na mbegu feki za aina mbalimbali huku akiwa ameghushi nembo za makampuni ya mbegu.

Kasambala ameiambia mahakama kuwa mtuhumiwa alikutwa na aina tano za mbegu feki za mazao yakiwemo mahindi kiasi cha kilogramu 105.3 yakiwa katika ghala na dukani alikuta mbegu za karoti, alizeti, bamia na matango.

Baada ya kusomewa mashtaka yake, mtuhumiwa amekana kutenda makosa hayo na ndipo mwendesha mashtaka wa Serikali, Hannarose Kasambala, aliieleza Mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika na upande wa mashtaka upo tayari kwa kuanza kutoa ushahidi wake.

Kutokana na kauli hiyo, Hakimu Ntumo, aliutaka upande wa mashtaka kuanza kutoa ushahidi wake na ndipo shahidi wa kwanza kwenye kesi hiyo kwa upande wa mashtaka, Emmanuel Mwakatobe, akapanda kizimbani na kutoa ushahidi wake.

Akiongozwa na Wakili Hannarose Kasambala, Mwakatobe ambaye ni mkaguzi kutoka TOSCI Makao Makuu Morogoro, alisema walifika jijini Mbeya kwa lengo la kufanya ukaguzi baada ya kupata malalamiko kutoka kwa baadhi ya wakulima na makampuni yanayozalisha mbegu.

Wakili Mwakatobe, alisema Machi 11, 2018, mfanyabiashara huyo alisimamishwa kujihusisha na uuzaji wa pembejeo baada ya kumkuta hana vigezo lakini waliporejea wamekuta mbegu zimeongezeka dukani kwake na hii ni baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wakulima za wazalishaji wa mbegu.

Alisema mnamo Januari 29, mwaka huu akiwa na askari wa Jeshi la Polisi, walikwenda kufanya ukaguzi na ndipo walipofika kwenye duka la mshtakiwa ambako walikamata gunia moja la mahindi yaliyopakwa rangi nyekundu yakiuzwa ndani ya duka hilo kama mbegu.

Akasema katika ukaguzi huo pia walikamata mbegu za bamia, karoti, alizeti, matango na vifungashio tupu vikiwa na nembo za makampuni ya uzalishaji mbegu ambazo zimeghushiwa.

Baada ya shahidi wa kwanza kutoa ushahidi wake, Hakimu Paul Ntumo, aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 23, mwaka huu itakapoendelea kusikilizwa tena mahakamani hapo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles