30.8 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

Matukio 12 ya kukumbukwa duniani 2018

MARKUS MPANGALA

MWAKA 2018 unafika tamati kesho. Yapo matukio kadhaa ambayo yamevigusa vyombo mbalimbali duniani.

Miongoni mwa matukio hayo yapo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii pia kuna ya kusikitisha yaliyosababisha hata vifo.

Haya ni baadhi ya matukio ya kukumbukwa katika mwaka huu 2018 ni:-

Uzunduzi wa treni yenye kasi zaidi Afrika

Taifa la Morocco lilizindua treni inayokwenda kwa kasi zaidi barani Afrika ambayo  imepunguza nusu ya muda wa kilometa 200 unaotumika kusafiri katika miji ya kibiashara na kiviwanda ya Casablanca na Tangier katika safari ya saa mbili.

Uzinduzi huo ulifanywa na Mfalme Mohammed VI na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.Treni hiyo inakwenda kwa kasi ya kilometa 320.

Afrika inatazamia kuimarisha miundombinu ya usafiri kushinikiza biashara, uwiano na utangamano wa kieneo. Mataifa ya Afrika yanakumbatia mfumo wa reli ya mwendo kasi katika kujaribu kushinikiza na kukuza uchumi na kuimarisha kasi za kusafirisha bidhaa baina ya mataifa kibiashara.

Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita jitihada za kufufua mfumo wa reli umechangia baadhi ya mataifa kuamua kubinafsisha huduma hizo hususan katika mataifa ya Magharibi na Mashariki ya Afrika.

Kenya: Mradi wa reli mpya ya kisasa nchini Kenya SGR, umefadhiliwa na serikali ya China ambao unaunganisha Mji wa Pwani wa Mombasa na Nairobi ulifadhiliwa kwa mkopo wa kiasi cha dola bilioni 3 kutoka kwa Benki ya China ya Exim katika kipindi cha miaka 15.

Reli hiyo ya SGR ni miongoni mwa miradi muhimu iliyoahidiwa na Rais Uhuru Kenyatta, katika kampeni za uchaguzi uliopita, ulizinduliwa mwezi mmoja kabla ya uchaguzi wa urais uliopita. Awamu ya kwanza ya reli Kenya ilianza kazi Juni 2017.

Tanzania: Jiwe la msingi la ujenzi wa awamu ya kwanza ya mradi mkubwa wa reli ya kisasa ya Standard Gauge liliwekwa na Rais Dk. John Magufuli Aprili 2017. Mradi huo umenuiwa baadaye kuziunganisha nchi za Rwanda na Burundi.

Katika awamu hii ya kwanza, ujenzi utakuwa wa reli yenye urefu wa kilomita takribani 300, ambayo itatoka jijini Dar es Salaam na kuishia Mkoa wa Morogoro.

Ni reli ya kisasa, na ya kwanza Afrika Mashariki na Kati itakayokuwa na uwezo wa kupitisha treni zitakazoendeshwa kwa nguvu ya umeme.

Reli hiyo inajengwa kwa awamu ya kwanza na kampuni kutoka nchi mbili, Uturuki na Ureno kwa gharama ya takriban dola bilioni 1.2 za Marekani.

Ethiopia: Reli mpya ya aina yake inayounganisha Mji Mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa na Mji Mkuu wa Djibouti imezinduliwa Oktoba 2016.

Reli hiyo mpya ina urefu wa kilomita 752 inatoka Addis Ababa hadi Bandari ya Doraleh katika Mji wa Djibouti, kwenye ghuba ya Aden.

Sehemu kubwa ya reli hiyo imo Ethiopia, kilomita 652 kutoka Addis Ababa hadi Dewale mpakani, na sehemu iliyosalia inaingia nchini Djibouti.

Gharama ya ujenzi wa reli hiyo ni dola bilioni 4 za Marekani. Ufadhili umetoka kwa benki ya serikali ya China ya Exim na Import kwa asilimia 70 na sehemu iliyosalia kutoka kwa serikali ya Ethiopia.

Benki ya maendeleo ya Afrika inaeleza kwamba katika ubinafsishaji ufadhili bora, muongozo wa sheria na utaalamu ni mambo muhimu. Mradi wa mtandao wa reli za kasi Afrika, ni sehemu ya ajenda ya Umoja wa Afrika hadi mwaka 2063 na umenuiwa kuimarisha mifumo iliyopo sasa ya kitaifa ya reli.

JACOB ZUMA ANG’OLEWA MADARAKANI

Suala la Zuma kung’oka madarakani lilitikisa katika duru za kisiasa. Cyril Ramaphosa ndiye amerithi nafasi ya Zuma, ambaye amekumbwa na sakata la ufisadi na matumizi mabaya ya madarakani yaliyomlazimu kujiuzulu.

Wachambuzi wa kisiasa wanadai kuwa kivuli cha Zuma bado kipo madarakani.

George Weah kutoka kusakata kabumbu hadi Urais

Nyota wa zamani wa kandanda duniani George Weah, alichaguliwa kuwa Rais wa Liberia, Januari mwaka huu. Weah amechukua nafasi ya rais wa kwanza mwanamke kuwahi kuchaguliwa kuongoza Taifa la Afrika, Ellen Johnson Sirleaf, ambaye amestaafu.

Kuingia kwa Weah madarakani kumekamilisha shughuli ya kwanza ya amani ya mpito nchini humo tangu mwaka 1944.

Wanaume marufuku kwenda Ukraine

Serikali ya Ukraine ilipiga marufuku wanaume wote ambao ni raia wa Urusi wa kati ya umri wa miaka 16 hadi 60 kuingia nchini humo.

Uamuzi huo ulitolewa na mkuu wa kikosi cha kulinda mipaka Petro Tsygykal, aliyesema kuwa raia wa kigeni, hususan wanaume wa Urusi hawataruhusiwa kuingia nchini humo.

Agizo hilo lilitolewa baada ya Ukraine kutangaza hali ya hatari ikihofia Urusi kupanga njama za uvamizi kamili baada ya meli za kijeshi za Urusi kuzishambulia meli za Ukraine na kuzikamata pamoja na manahodha wake.

Kuuawa kwa mwandishi wa habari Khashoggi

Mwandishi wa habari na mkosoaji wa utawala wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi alifariki dunia Oktoba 2 mwaka huu.

Khashoggi aliuawa baada ya kufichua kuwa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia unafadhili kituo cha Televisheni ambacho kimekuwa kikitumika kuipinga na kuikosoa Serikali ya Iran, kituo hicho lidaiwa kurusha matangazo yake kutoka Uingereza.

Kwa mujibu wa ujumbe ulioandikwa kwenye ukurasa wa mwandishi wa gazeti la The Guardian nchini Uingereza, Saeed Kamali Dehghan, kupitia mtandao wa Twitter amesema katika makala iliyochapishwa Oktoba 2 mwaka huu na Guardian, alinukuu duru za karibu na utawala wa Saudia ambazo zilimdokezea kuwa, Televisheni ya Iran International, hupokea msaada wa dola milioni 250 kutoka Saudia kila mwaka.

Khashoggi aliuawa kinyama siku hiyo ambayo gazeti hilo lilichapisha ripoti hiyo. Baada ya mauaji hayo, gazeti la The Guardian  liliandika kuwa Televisheni ya Iran International inafadhiliwa na mfanyabiashara Msaudi, Saud al-Qahtani, amabye ni mpambe na mshauri wa mrithi wa kiti cha ufalme, Mohammad Bin Salman.

Al-Qahtani ni kati ya maafisa wa ngazi za juu wanaodaiwa kutimuliwa na Bin Salman baada ya kuuawa Khashoggi ili kupunguza mashinikizo ya kimataifa.

Baadhi ya duru zinasema al-Qahtani ni miongoni mwa wapambe wa Bin Salman waliosimamia na kuelekeza mauaji ya Khashoggi.

Imedokezwa kuwa al-Qahtani aliongoza mauaji hayo kwa njia ya video kupitia Skype ambapo aliamuru wauaji wampelekee kichwa cha Khashoggi.

Jamal Khashoggi aliuawa Oktoba 2 mwaka huu baada ya kuingia katika ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul nchini Uturuki.

Hadi sasa mwili wa Khashoggi haujapatikana na wakuu wa Uturuki wanasema wana ushahidi kuwa mwili wake uliyeyushwa kwa asidi.

Serikali ya Uturuki imesema inaendelea na uchunguzi wa mauaji ya Khashoggi na kwamba itaendelea kutoa taarifa zaidi kuhusu ukatili huo.

KIFO CHA KOFI ANNAN

Kifo cha kiongozi huyo aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, na mwanadiplomasia nyota, Kofi Annan kiliwaibua viongozi mbalimbali duniani na  kummwagia sifa nyingi huku wakibainisha kuwa dunia imempoteza mtu muhimu sana katika masuala ya upatanishi wa amani.

Mke wa mwanadiplomasia huyo Nane Maria Annan ndiye aliongoza mamia ya waombolezaji, wakiwemo viongozi wa sasa waliohudhuria ibada ya mazishi.

Rais wa Ghana, Nana Akufo Ado, alimtaja Annan kuwa mmoja wa viongozi mashuhuri kabisa wa zama hizi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alimsifia Annan akisema alikuwa kiongozi wa kipekee duniani aliyekuwa mwenye heshima, jasiri na mtu aliyekuwa muadilifu na aliyejitolea katika kazi yake.

Annan aliongoza Umoja wa Mataifa kuanzia mwaka 1997 hadi 2006, na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel mwaka 2001, alifariki dunia nchini Uswisi Agosti 18, mwaka huu, akiwa na umri wa miaka 80.

Kushambuliwa kwa kisu mgombea urais

Mgombea wa chama cha mrengo wa kulia katika kinyanganyiro cha kuwania urais nchini Brazil, Jair Bolsonaro(63), alijeruhiwa baada ya kushambuliwa kwa kuchomwa kisu wakati alipokuwa akifanya kampeni Kusini Mashariki mwa Brazil.

Mwanaume mmoja anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 40 alitiwa mbaroni akihusishwa na shambulizi hilo. Hata hivyo Bolsanaro alishinda kiti hicho.

Kuzama Kivuko cha MV Nyerere

Septemba 20, mwaka huu Taifa la Tanzania lilipata pigo baada ya watu takribani 224 kufariki dunia, baada ya Kivuko cha MV Nyerere kilichokuwa kinafanya safari kati ya Bugorora katika Kisiwa cha Ukerewe na Kisiwa cha Ukara katika Ziwa Victoria, mkoani Mwanza kuzama.

Mgogoro Rwanda, Burundi

Jumuiya ya Afrika Mashariki imeshuhudia mgogoro wa wanachama wake wawili, nchi za Rwanda na Burundi, na kuwaachia kibarua kigumu wengine  Tanzania, Kenya, Uganda na Sudan kusini.

Mgogoro wa sasa umefika mahali pabaya zaidi baada ya Rais wa Pierre Nkurunziza kuandika barua kwenda kwa Mwenyekiti wa sasa Jumuiya hiyo, Rais Yoweri Museveni wa Uganda na kueleza kinaga ubaga juu ya hali ya kisiasa nchini mwake, uhusiano wake na jirani yake Rwanda na sababu za kutohudhuria vikao vya Jumuiya hiyo vilivyotakiwa kufanyika jijini Arusha nchini Tanzania.

Ndani ya barua hiyo Rais Nkurunziza, alitangaza kuna mzozo wa wazi kati ya taifa lake na taifa jirani la Rwanda katika kinachoonekana kuwa kudorora zaidi kwa uhusiano baina ya mataifa hayo mawili.

Kwa upande wake Serikali ya Rwanda, mara kwa mara imekuwa ikikanusha tuhuma hizo, huku ikibainisha kuwa ni Burundi ndiyo inahusika kuwasaidia waasi wanaopambana na serikali ya Rais Paul Kagame.

Nkurunziza anataka kufanyike mkutano maalumu wa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kujadili mgogoro huo kati ya Rwanda na Burundi.

Viongozi wa mataifa ya jumuiya hiyo ambayo kwa sasa inajumuisha Burundi, Rwanda, Uganda, Kenya, Tanzania na Sudan Kusini, walipangiwa kukutana tena  Desemba 27, mwaka huu katika kikao cha kawaida cha wanachama ambacho kimeshindikana kufanyika baada ya akidi kutotimia.

Mwenyekiti wa EAC, Rais Museveni aliijibu barua ya Rais Nkurunziza Desemba 8, mwaka huu, ikiwa ni siku nne baada ya barua ya Burundi kuwasilishwa nchini Uganda.

 “Nakiri kuwa mgogoro baina ya Rwanda na Burundi linapaswa kujadiliwa. Hilo ni kwa mantiki ya soko la pamoja. Suala la soko la pamoja ni muhimu, linahusu usafirishaji au usambazaji wa bidhaa kutoka nchi moja kwenda nyingine na kinyume chake. Uhuru wa watu na kufanya biashara miongoni mwa nchi wanachama. Iwapo kuna mgogoro, ni kwa kiasi gani familia, wafanyabiashara, kampuni zinaweza kuwa na maendeleo?” imesema barua ya Museveni.

Katika hatua nyingine Museveni amemkumbusha Nkurunziza juu ya vita vya muda mrefu kati ya Uganda na Joseph Kony, ambaye alilazimika kujadiliana naye ili kumaliza mgogoro na kuleta amani nchini humo.

Rais Kabila kutogombea Urais

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Joseph Kabila alitangaza kutogombea nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Desemba 23, mwaka huu kabla ya kuahirishwa hadi Desemba 30, mwaka huu na baadhi ya maeneo hadi machi 2019.

Kwa mujibu wa msemaji wa Rais Kabila, Lambert Mende alimtangaza Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Shadary kupeperusha bendera ya muungano wa chama tawala.

Uteuzi wa Shadary ulifuta minong’ono ya kuteuliwa wanasiasa wengine akiwamo Augustin Matata Ponyo (Waziri Mkuu wa zamani), Nehemie Mwilanya Wilondja (Mkuu wa Watumishi wa Rais) na Aubin Minaku (Rais wa Bunge la Taifa).

Shadary ni mzaliwa wa Mji wa Kasongo uliopo Mkoa wa Maniema Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Alizaliwa Novemba 29, mwaka 1960.

Aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa Tume ya PAJ bungeni kati ya mwaka 2006-2011, kabla ya kuchukua uongozi wa chama cha PPRD bungeni mbali na kuwa mshirikishi wa wabunge walio wengi katika Bunge hilo hadi sasa. Mei 17, 2015, aliteuliwa na Rais Joseph Kabila kuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama cha PPRD.

Michelle Obama na urais 2020

Mwaka huu jina la Michelle Obama, liliendelea kutajwa kwenye mbio za kisiasa kuliko mambo ya taaluma wala shughuli zake binafsi kwa mke huyo wa rais wa zamani wa Marekani, Barrack Obama.

Mwaka huu jina lake limerudi tena kwenye ramani ya kisiasa kama lilivyokuwa wakati wa mbio za uchaguzi wa mwaka 2016. Kwenye mbio za uchaguzi wa katikati ya muhula Novemba 4, mwaka huu, jina lililotamba zaidi lilikuwa la mumewe Barrack Obama ambaye aliingia kwa kishindo kwenye kampeni hizo za kukisaidia chama chao cha Democratic.

Matunda ya ushiriki wa Barrack Obama kwenye uchaguzi wa katikati ya muhula ni chama cha Democratic kupata ushindi mnono kwenye Bunge la Wawakilishi huku kikiwa na nusu ya wagombea wake ni wanawake.

Michelle Obama ambaye kwa sasa yuko kwenye kampeni ya kukitangaza kitabu chake cha ‘Becoming” kilichozinduliwa hivi karibuni na kuuzwa nakala takribani milioni moja na ushee.

Licha ya kampeni za kuzindua kitabu hicho kumehusishwa na uchaguzi mkuu wa urais wa mwaka 2020 ambao rais wa sasa Donald Trump atawania ngwe ya pili.

Michelle ni mwanachama wa chama cha Democratic amekuwa bega kwa bega na mumewe tangu alipokuwa Seneta wa Hawaii, na baadaye kuwa rais wa Marekani kwa awamu mbili kuanzia mwaka 2008 hadi 2016.

Duru za kisiasa nchini Marekani zinaonyesha kuwa Michelle Obama ni miongoni mwa hazina ya wagombea wanaoweza kukabidhiwa jukumu la kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu ifikapo mwaka 2020. Uchaguzi wa mwaka 2020 maana yake Michelle iwapo atateuliwa atapambana na mgombea wa chama tawala cha Rpublicans, Donald Trump.

Kampeni za uchaguzi wa urais wa mwaka 2016 ndizo zilisimika fununu za Michelle Obama kuwa mgombea wa urais wa Democratic ifikapo mwaka 2020. Katika uchaguzi wa mwaka 2016 Michelle alishiriki kampeni za kumnadi mgombea wao Hillary Clinton.

Wanawake walivyong’ara Ethiopia

Taifa la Ethiopia lilichomoza na kwa mara nyingine baada ya waziri mkuu wa nchi hiyo, Abiy Ahmed kumteua Birtukan Mideksa kuiongoza Tume ya Taifa ya uchaguzi nchini humo.

Mwanamama huyo anaingia kwenye orodha ya wanawake wanaoshikilia madaraka ya juu zaidi nchini Ethiopia. Kihistoria wananchi wa Ethiopia hupenda kusema walitawaliwa na Malkia Sheba nyakati za biblia, jambo ambalo wana fahari kubwa nalo, hata hivyo ukweli ni kwamba taifa hilo la lina jamii iliyogubikwa kwa mfumo dume.

Takwimu zilizokusanywa na serikali ya Ethiopia na taasisi nyingine zinaonyesha kuwa: takriban asilimia 25 ya wanawake hutegemea maamuzi ya waume zao.

Novemba 18, mwaka Meaza Ashenafi aliteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Rufani nchini Ethiopia. Ashenafi amewahi kuwa wakili wa kutetea haki za binadamu, ambaye jitihada zake za kukabiliana na ndoa za utotoni ziliigizwa kwenye filamu ya muigizaji mashuhuri wa Hollywood nchini Marekani, Angelina Jolie mwaka 2014.

Billene Aster Seuoum ni mtaalamu wa mawasiliano ambaye aliteuliwa kuwa msemaji wa Rais wa Ethiopia.

Sahle-Work Zewde aliteuliwa kuwa rais wa kwanza mwanamke nchini humo. Sahle-Work ni mwanadiplomasia mwenye uzoefu ambaye sasa amekuwa kiongozi wa kipekee mkuu mwanamke barani Afrika.

Kuchaguliwa kwake katika wadhifa huo kumetokana na hatua ya waziri mkuu Abiy Ahmed kuliteua baraza la mawaziri ambapo nusu ya nyadhifa katika baraza hilo zimewaangukia wanawake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles