MWANDISHI WETU-DODOMA
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ametoa onyo kali kwa baadhi ya Watanzania ambao wanafanya biashara ya kuwaingiza wahamiaji haramu nchini huku wakijua kufanya hivyo ni kinyume na sheria za nchi.
Amesema Idara ya Uhamiaji itashirikiana na Jeshi la Polisi kuwasaka na kuwakamata watu hao na kuwafungulia mashtaka.
Akizungumza jana baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kumaliza kukagua eneo la ujenzi wa makao makuu ya uhamiaji Dodoma, Waziri Lugola alikiri kuwapo wahamiaji haramu nchini ambako alisistiza kuwa tatizo hilo litamalizwa.
“Naomba muwafikishie salamu watu ambao wanatabia hiyo ya kuwaingiza wahamiaji haramu nchini, Serikali ipo na pia inafanya kazi, kama wapo basi wajue tutawakamata tu,” alisema Lugola.
Aliwataka Suma JKT wanaojenga jengo la makao makuu ya uhamiaji wafanye kazi kwa weledi mpaka jengo hilo litakapokamilika, na pia mara kwa mara viongozi wa Wizara yake akiwamo yeye mwenyewe atakuwa anatembelea eneo hilo la ujenzi.
“Sitasubiri mpaka Mheshimiwa Rais haje hapa kukagua, litalifuatilia mwanzo mwisho ujenzi huu, na pia mlisema pale Magereza Ukonga mbele ya Rais, kuwa jeshi halishindwi, nami ninaamini nyie Suma JKT, ujenzi huu utakamilika bila kuwa na matatizo,” alisema Lugola.