27 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Makinda asisitiza bima ya afya kwa wanawake

COSTANCIA MUTAHABA(DSJ) na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Mama Anna Makinda amewashauri wanawake wajasiriamali sokoni kuhakikisha wanakata   bima ya afya kwa kuwa ndiyo msingi wa biashara na mkombozi kwao.

Akizungumza na wanawake hao katika mkutano ulioandaliwa na Shirika la Equality for Growth (EFG), Makinda alisema bima hiyo ni kinga kwa afya na biashara zao.

Alisema kwa sasa vimeandaliwa vifurushi mbalimbali vya bima vitakavyowasaidia watanzania   wengi.

“Tuna vifurushi mbalimbali ambavyo hivi karibuni Waziri wa Afya Mendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Watoto atavitambulisha, hivyo niwaombe kuchagua kifufushi kinachowafaa ,” alisisitiza Makinda.

 Makinda ambaye ni Spika wa Mstaafu wa Bunge la   Tanzania alisema kwa sasa magonjwa yasiyoambukiza kama figo yanatumia gharama kubwa kutibika hivyo kila fedha wanayopata kipaumbele cha kwanza wawekezwe kwenye bima ya afya.

Alisema wamegundua kuwapo  changamoto katika kifurushi cha kikoa kilichokuwa kinatumiwa na vikundi vya wajasiriamali hivyo utaratibu unaandaliwa kwa ajili ya vifurushi vingine.

“Ni asilimia 32 pekee ya Watanzania ndiyo wenye bima ya afya, hivyo kupitia utaratibu mpya unaoandaliwa tunaamini tutawafikia nusu ya Watanzania wote,” alisema.

  Makinda pia aliwataka wanawake hao kugombea nyadhifa mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa baadaye mwaka huu.

“Msisikilize kelele za watu wanaowazunguka akiwamo mume, majirani na wengine bali msimamie mnachokiamini mpaka mfikie malengo.

“Kipindi cha uongozi wangu bungeni nilipitia mitihani mingi lakini nilisimamia ninachokiamini na kufikia lengo nililojiwekea.

“Mimi mpaka kumaliza kazi ya uspika nimetukanwa sana hadi kuitwa dikteta lakini niliyavumulia na kusimamia nilichokiamini, hivyo msikatishwe tamaa na kelele,” alisema.

Makinda aliushukuru Umoja wa Mataifa kupitia kitengo cha UN women kwa kushiriki katika kampeni ya kutokomeza ukatili wa  jinsia sokoni.

Mkurugenzi wa EFG, Jane Magigita alisema ndani ya miaka mitano ijayo wamejipanga kuwafikia wanawake milioni saba.

“Tumefanikiwa kupunguza ukatili wa  jinsia katika masoko ya Manispaa ya Ilala kwa asilimia 75 kwa kushirikiana na UN Women,” alisema Jane.

  Mwakilishi wa UN Women, Lucy Tesha alisema kupitia ujumbe wa  Siku ya Mwanamke Duniani wataendelea kushirikiana na EFG kuhakikisha ukatili unakwisha nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles