24.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Kwanini bado aitwe mtoto wa mtaani

Na EVANS MAGEGE

NENO ‘ watoto wa mtaani’ ni moja ya maneno ambayo binafsi nimekuwa nayaweka katika tafsiri  hasi au yenye ukakasi dhidi ya ubinadamu.

Mara nyingi ninaposikia neno hilo nalitafsiri katika mtazamo wa udhalilishaji wa kibinadamu kwa kujenga picha ya kwamba ni neno lenye maana chafu zaidi kuliko hata kitendo cha udhalilishaji.

Kwa namna moja au nyingine nimekuwa  nikijiuliza ni neno lipi linaweza kuwa mbadala  ya hilo, je waitwe watoto wa wanaoishi kwenye mazingira magumu? au  waitwe watoto wanaoishi mitaani?

Hata hivyo tafakuri yangu imekuwa inanionyesha kwamba  kutumia neno watoto wanaoishi katika mazingira magumu hailengi sawia kusudio nililonalo kwa sababu naitafsiri kama ni kauli ya jumla sana.

Kama likitumiwa ipasavyo neno  watoto wanaoishi mitaani, binafsi naiona maana yake pia kutakuwa na hali ya kupoza kwa kiasi fulani ukakasi utokanao na kauli ya ‘ watoto wa mitaani’.

Hoja hii inatokana na maswali mengi ambayo nimekuwa nikijiuliza kwa  maana ya kuitafuta tafsiri sahihi ya kumtendea haki mtoto anayeishi katika mazingira yasiyo sahihi.

Kwanza  ninaposikia mtoto wa mtaani nimekuwa nahoji kwamba mtaa unazaa mtoto? Na mara kadhaa  swali kama hili nikiwauliza baadhi ya watu wanajibu hapana kwa maelezo ya kwamba hakuna mtaa unaozaa mtoto bali  mtoto anaweza kuishi mtaani.

Kwa muktadha huo aina hiyo ya maisha ya watoto wanaoishi mitaani ipo katika mataifa mbalimbali duniani, namaanisha kwamba kundi hilo la watoto lipo kwenye mataifa ambayo hayajaendelea, yanayoendelea na yaliyoendelea.

Tanzania  ni miongoni mwa mataifa yanayoendelea,  inakabiliwa na changamoto ya uwapo wa watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu, ndani ya kundi hili la watoto wapo wanaoishi mitaani kwa sababu ya kukosa makazi.

Tafiti na maandiko mbalimbali  yanaonyesha sababu mbalimbali zinazochochea hali hiyo na kikubwa zaidi ni umasikini ndani ya familia na unyanyasaji.

Kwa bahati mbaya sehemu kubwa ya mtazamo wa jamii dhidi ya watoto wanaoishi mitaani ni hasi na pengine hali hiyo ndiyo sababu kubwa inayochagiza neno ‘watoto wa mitaani’  kuonekana kama neno sahihi la kutumiwa japokuwa linaathari kubwa kisaikolojia kwa walengwa.

HALI IKOJE NCHINI?

Mtazamo wa kutafuta neno sahihi la kuwaita watoto wanaoishi mitaani ni mjadala ambao unahitaji michango ya mawazo na hoja mbalimbali kutoka kwa wadau si tu wa masuala ya watoto bali hata wanasiasa.

Mwanazuoni Martin Gross amepata kusema “Tunaishi kwenye dunia ambayo siasa imechukua nafasi ya falsafa,”. Nahuisha nukuu hii kwa kusema wanasiasa wana wigo mpana wa kupaza sauti ya  utetezi wa neno sahihi ambalo litafaa kuwaita watoto wanaoishi mitaani.

Ukiachilia mbali hilo, ipo haja ya kuiangalia hali ilivyo sasa ya watoto wanaoishi mitaani nchini.

Tafiti zinaonyesha Mkoa wa Dar es Salaama unaongoza kwa idadi kubwa ya watoto wanaoishi katika mazingira ya mitaani.

Mwaka 2017 bungeni jijini Dodoma, Serikali ilikiri uwapo kwa ongezeko la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani hasa katika miji mikubwa nchini, takwimu zinaonyesha kuwa Jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa asilimia 28 ya watoto hao

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto  Ummy Mwalimu alitoa maelezo hayo wakati akijibu swali la  Khatib Said Haji Mbunge wa Konde aliyetaka kujua serikali inachukua hatua gani kukabiliana na ongezeko la watoto wanaoishi mitaani.

“Ni kweli kumekuwa na ongezeko la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani hasa katika miji mikubwa. Kwa mujibu wa takwimu zilizofanyika katika miji ya Dar es Salaam na Mwanza mwaka 2012 zilionesha kuwa Jiji la Dar es Salaam lilikuwa na watoto 5,600 kutoka mikoa 10 ambayo ni Dar es Salaam asilimia 28, Dodoma asilimia 8, Mwanza asilimia 7, Morogoro asilimia 7, Tanga asilimia 6, Iringa asilimia 5, Pwani asilimia 5, Kilimanjaro asilimia 5 , Arusha asilimia 4”. Alisema Waziri Ummy Mwalimu.

Aidha, alisema serikali ina jukumu la msingi la kuhakisha ulinzi na usalama kwa watoto hao unapatikana pamoja na kushirikisha jamii iweze kuwasaidia kuwaokoa vijana wanaoishi katika mazingira hatarishi wakiwamo watoto wanaoishi mitaani.

Mussa Mgata ni Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto wanaoishi Mitaani la Railway (RCA) kwa upande wa Tanzania. Hivi karibuni katika mkutano wake na wanahabari  amezungumzia hali ilivyo kwa kundi hilo.

Anasema kwa mujibu wa utafiti  mpya uliofanywa na RCA kwa kushirikiana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto katika mikoa sita   inaonyesha katika idadi ya watoto wanaishi mitaani  watoto wa kiume ni wengi  kuliko wa kike.

Anatanabaisha katika idadi waliyoifikia kwa mchana watoto wa kiume ni 4,865 na wa kike 1,528.

Kwa upande wa watoto wa kiume waliofikiwa mchana, watoto wenye umri kuanzia 0 hadi miaka 6 walikuwa ni asililimia 3, miaka 7 hadi 10 asilimia 12, miaka 11 hadi 14 asilimia 31 na miaka 15 hadi 18 ni asilimia 54.

Kwa upande wa watoto wa kike waliowafikia mchana,  umri wa kuanzia mwaka 0 hadi 6 asililia 4, miaka 7 hadi 10 asilimia 14, miaka 11 hadi 14 asilimia 28 na miaka 15 hadi 18 asilimia 54.

Mgata anasema katika utafiti huo walipoufanya usiku waliwafikia watoto wa kiume 975 huku watoto wa kike wakiwafikia 410.

Anachanganua utafiti huo upande wa watoto wa kiume waliowafikia usiku makundi manne yenye utofauti wa kiumri.

Anasema watoto wenye umri kuanzia mwaka 0 hadi 6  ni asilimia 3, miaka 7 hadi 10 asilimia 11, miaka 11 hadi 14 asilimia 35 na miaka 15 hadi 18 asilimia 51.

Kwa upande wa watoto wa kike waliofikiwa, wenye umri kuwanzia 0 hadi 6 asilimia 1, miaka 7 hadi 10 asilimia 3, miaka 11 hadi 14 asilimia 10 na miaka 15 hadi 18 asilimia 86.

Anasema utafiti huo ulifanywa katika miaka ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa , Mbeya na Mwanza na ulifikia watu 10,595 ambapo watu 6,393 walikuwa nia watoto wa chini ya umri wa miaka 18 huku watu 4202 walikuwa ni wale wenye umri wa kuanzia miaka 18 hadi 25.

Katika utafiti huo Mgata anasema sababu kubwa waliyoibaini kuchochea uwapo wa watoto wanaoishi mitaani ni umasikini, manyanyaso na migogoro ya kifamilia.

HALI IKOJE DUNIANI?

Wakati idadi ya watu duniani kwa sasa ikiwa zaidi ya watu bilioni saba, takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia  Watoto(UNICEF) zinaonyesha kuwa idadi ya watoto wanaoishi mitaani inakadiriwa kufika milioni 120.

Katika idadi hiyo  watoto milioni 30 wapo ndani ya Bara la Afrika, huku idadi ya ujumla kidunia watoto milioni 50 ni wale waliopoteza wazazi wao kwa ugonjwa wa Ukimwi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles