25 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Kinachokwamisha kilimo chatajwa kwenye ripoti

GRACE SHITUNDU-DAR ES SALAAM

RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imeweka wazi kinachokwamisha maendeleo ya kilimo nchini.

Imeeleza kwamba, Serikali haijatekeleza ipasavyo mikakati mbalimbali iliyolenga kuifanya Sekta ya Kilimo kuwa na tija, endelevu, na uti wa mgongo wa uchumi wa nchi.

Kwamba mikakati mikuu iliyotambuliwa na Wizara ya Kilimo kama nguzo za maendeleo ya kilimo hazina utoshelevu wa usimamizi wa wizara pamoja na wadau wengine.

Kwa mujibu wa ripoti ya CAG, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ilifanya kaguzi sita za utendaji, na ukaguzi mmoja wa ufuatiliaji katika Sekta ya Kilimo.

Ripoti imeeleza udhaifu ulioonekana ulikuwa kwenye usimamizi wa pembejeo za kilimo; ubora wa udhibiti wa pembejeo za kilimo; visumbufu vya mazao na milipuko ya magonjwa; ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji; uwepo wa huduma za ugani kwa wakulima; na utoaji wa huduma za usaidizi kwa wasindikaji wa mazao ya kilimo.

“Mapungufu yaliyoonekana yalisababishwa na udhaifu wa mifumo ya kuhakikisha mipango, utekelezaji, usimamizi na tathmini za mikakati iliyotekelezwa na serikali kwa lengo la kusaidia maendeleo ya Sekta ya Kilimo.

Usimamizi wa pembejeo

Ripoti inaonyesha ukaguzi  ulibaini kuwa Wizara ya Kilimo kupitia Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Viuatilifu, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu (TOSCI) hazikuwa zimeweka mpango wa mahitaji ya pembejeo ya kilimo nchini.

Ilibainisha kwamba mahitaji yaliyokuwa yamepangwa hayakuwa na uhalisia, kwani hapakuwa na utafiti uliokuwa umefanywa ili kujua idadi halisi ya pembejeo zilizohitajika kwa kuzingatia kanda za kiikolojia za kilimo.

“Nilibaini hakukuwa na njia nzuri ya kukadiria mahitaji ya pembejeo za kilimo, hii ni kwa sababu hakukuwa na mfumo au njia sahihi na rahisi zilizotolewa wakati wa makadirio ya idadi kwa ajili ya kupanga mahitaji.

“Kulikuwa na mfumo usiojitosheleza wa kuhakikisha pembejeo zinasambazwa kwa wakulima kwa wakati, mfumo wa usambazaji ulikuwa na mapungufu yaliyooonekana kwenye maeneo ya muda wa usambazaji, ubora na udhibiti wa bei ambayo inaathiri ufanisi wa mfumo.

“Kwa ujumla, udhaifu huu una uwezekano mkubwa wa kuathiri uzalishaji wa mazao ya kilimo na kupelekea uhaba wa chakula pamoja na kushuka kwa kipato cha mkulima mmoja na nchi kwa ujumla,” ilieleza sehemu ya  ripoti hiyo.

Udhibiti wa ubora wa pembejeo

Ripoti imeeleza kwamba, wizara bado haijadhibiti kikamilifu usambazaji na utumiaji wa pembejeo za kilimo ili kuhakikisha wakulima wanatumia viuatilifu bora, mbegu bora na mbolea.

Ilibainishwa kulikuwa na mfumo usiojitosheleza wa kuhakikisha pembejeo za kilimo zinapatikana kwa wakulima na zinakidhi viwango vinavyohitajika.

“Wakulima nchini walitumia pembejeo ambazo zilikuwa ama na ubora wa chini, bandia, au chini ya kiwango, kutokana na mfumo usiojitosheleza wa kuhakikisha pembejeo zenye ubora mzuri zinapatikana kwa wakulima.

“Kulikuwa na upungufu katika ukaguzi uliofanywa kwa wasambazaji wa pembejeo za kilimo mipakani ili kudhibiti ubora wa pembejeo zinazoingizwa na kuuzwa nchini.

“Hapakuwa na mpango na mwongozo ulioanzishwa wa ukaguzi, badala yake, wakaguzi walitumia fomu za ukaguzi tofauti tofauti na ambazo ziliathiri ubora wa ukaguzi uliofanyika na hivyo kushindwa kutambua mapungufu ya ukaguzi,” ilieleza sehemu ya  ripoti hiyo.

Ripoti imeeleza kwamba, hali hii iliathiri bidhaa za kilimo katika masoko ya ndani na nje ambayo inaweza kupelekea athari mbaya kwenye uchumi wa taifa.

Udhibiti wa magonjwa na visumbufu

Kuhusu usimamizi katika visumbufu vya mimea na milipuko ya magonjwa, ripoti ilieleza kuna utekelezaji usiojitosheleza wa mikakati ya kinga na udhibiti, japokuwa kulikuwa na taarifa za mara kwa mara za milipuko ya visumbufu vya mimea na magonjwa.

“Kulikuwa na ushirikiano usio imara kati ya watendaji muhimu, pia ufuatiliaji na tathimini haukufanyika ipasavyo, hii ilipelekea mwendelezo wa matukio ya milipuko ya magonjwa na visumbufu vya mimea katika maeneo mengi nchini.

“Hivyo, kuna hatari ya kuwa na uhaba wa chakula na kupungua kwa kipato kwa wakulima kutokana na uzalishaji duni wa mazao, matokeo yake mchango wa kilimo katika uchumi wa taifa utaporomoka,” ilieleza ripoti.

Ripoti pia ilibaini usimamizi wa utoaji wa huduma za ugani nchini haujatekelezwa ipasavyo na wizara husika.

Kutokana na hayo, ripoti hiyo imetoa mapendekezo

12 kwa Wizara ya Kilimo, ikiwamo kuhuisha taarifa zake na kuboresha hatua zilizopo za usajili, ukaguzi na mafunzo kwa mawakala wa pembejeo na wakulima, ikiwa njia ya kudhibiti ubora kwenye viuwatilifu, mbegu na mbolea, ili kujihakikishia uwepo wa pembejeo zenye ubora katika soko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles