28.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Mahiga afichua siri za Sokoine

ELIYA MBONEA-MONDULI

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Balozi Dk. Agustine Mahiga, amefichua siri ya mambo mbalimbali yaliyowahi kufanywa na kuamuliwa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Sokoine, kwa masilahi ya Taifa.

Akizungumza wakati wa misa iliyofanyika Monduli Juu jana, Mahiga, alisema akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), alibahatika kufanya naye kazi akiwa Waziri wa Ulinzi na baadaye Waziri Mkuu.

“Niliona alivyokuwa na ari na nidhamu ya kufanya kazi, kuna siku aliwahi kuniita ofisini kwake saa saba usiku akitaka tupitie taarifa ya kupambana na mafisadi,” alisema na kuongeza:

“Tulifanya kazi ile hadi saa nane usiku kisha akaniambia kazi tuliyopewa na Mwalimu Nyerere lazima tuimalize hivyo aliomba niende kulala tukutane kesho saa 11 asubuhi, nimefika ofisini kwake kesho nikamkuta, kumbe hakwenda kulala alikesha.

“Uadilifu na kuwajibika ilikuwa sehemu ya maisha ya Sokoine, hakuwa tu mzalendo bali alifanya kazi ambayo wengi hamuijui.”

Pia alisema moja ya majukumu mengine aliyofanyia kazi na Sokoine ilikuwa ni tishio la amani lililofanywa na Iddi Amin wa Uganda.

“Aliniita, akaniambia Amin ana ndege, magari ya kivita na askari wanaotembea kwa magari sisi hatuna lakini tujiandae kupambana naye.

“Sokoine akaniambia lazima taifa tuwe na mizinga ya kuangushia ndege na mizinga ya kupiga magari yao. Lakini lazima tutatengeneza jeshi la askari watembea kwa miguu na walitembea kuanzia mwanzo wa Uganda hadi mwisho.

“Haya yalikuwa mawazo ya Sokoine, kama si yeye pengine tusingekuwa tunazungumza hapa leo (jana), lakini pia alipata taarifa za Uganda kutumia sumu kwenye vita, haraka akaniita na kunipa jukumu la kutafuta taifa rafiki litakalotusaidia bahati nzuri Amin hakuendelea kutumia sumu hiyo.

“Lakini pia Mwalimu Nyerere alipata taarifa za Amin kutumia Wapalestina katika vita hiyo, haraka Sokoine akaniita na kututuma kwenda kumwona Rais wa Palestina wakati huo Arafati ambaye aliwazuia askari wake,” alisema.

Balozi Mahiga aliendelea kumwelezea Sokoine akisema wakati wa kutaka kupindua Serikali ya Mwalimu Nyerere alifanikiwa kuzima maasi hayo alimwomba akaishi nje ya nchi.

“Aliniita ofisini kwake akaniambia naweza kudhurika kutokana na kazi iliyofanyika hivyo akaomba niende kuishi nje ya nchi nikiwa Canada mwaka 1983 mwaka mmoja baadaye nikasikia amefariki,” alisema Mahiga.

PENGO

Naye Askofu Mkuu wa Jimbo la Dar es Salaam, Kardinali Polycarp Pengo, aliwataka viongozi wa Serikali na Watanzania kumwomba Mungu ili wasiwe chimbuko la mafarakano na mapigano kwa taifa.

Akizungumza katika misa hiyo, iliyohudhuriwa pia na Askofu Mkuu, Isack Aman wa Jimbo Kuu la Arusha, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, Pengo, alisema kifo cha Sokoine kilichotokea miaka 35 iliyopita, kinapaswa kuwa fundisho kubwa kwa viongozi wa sasa wanaopaswa kujifunza kutoka kwake.

“Amani kati ya watu huvurugwa na watu mbalimbali, kwanza ubinafsi wa watu ambao wamepata uwezo wa kujikusanyia mali hata wengine wakifa kwa njaa ili mradi wao wajilimbikizie mali kwa kiwango cha juu.

“Hali hii haiwezi kuvumilika na watu kwa sababu itafika mahali watu watasema imetosha, hatuwezi kuendelea kufa kwa njaa wakati wachache wanakufa kwa ulafi,” alisema Pengo.

Akitolea mfano wa maisha ya Sokoine, alisema ipo mifano mingi inayoweza kudhihirisha kutokuwa na ubinafsi kwa kuwa alikuwa akimwomba Mungu awe chombo cha amani.

“Neema hiyo aliyokuwa akijiombea ilifanya kifo chake kisiwe cha mafarakano, kwa sababu mtakumbuka kifo chake kilizua maswali mengi kwa wapenda amani.”

PINDA

Naye Pinda alisema alimfahamu Sokoine tangu akiwa anafanya kazi Ikulu.

Alisema kifo hicho kilikigusa CCM kwa sababu Mwalimu Nyerere tayari alishasema anang’atuka hivyo mtu aliyekuwa amemwona anafaa na mwenye uadilifu anayepinga rushwa alikuwa ni Sokoine.

“Sisi tuliokuwa karibu pale Ikulu tulishaona na kujua tayari Sokoine anaandaliwa kwa sababu ishara zilikuwa wazi, bahati mbaya mwaka mmoja kabla ya Mwalimu Nyerere kung’atuka akafariki kwa ajali ya gari,” alisema Pinda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,908FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles