PRETORIA, AFRIKA KUSINI
RAIS wa Afrika Kusini Jacob Zuma amesema hana tatizo baada ya kuzomewa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wafanyakazi akisema nchi hii ni ya demokrasia, si kiimla.
“Utakubaliana nami kuwa katika nchi yenye viongozi wa kiimla, hakutakuwa na maandamano wala kuzomea,” Zuma aliwaambia waandishi wa habari.
Katika nchi isiyo na demokrasia, kutakuwa na rais mwenye hasira akiamrisha polisi kuwakamata watu hawa, alisema.
Wakati wa siku hiyo, Wafanyakazi walimkemea Zuma na kumtaka ajiuzulu.
Akijibu hilo, Zuma alisema, "Nina furaha kuwa watu wa Afrika Kusini wamekomaa kidemokrasia na wana rais ambaye wanaweza kumzungumzia chochote walicho nacho akilini mwao.”
Alionekana kupuuzia mbali uwezekano wa kuondoka madarakani, akisema kuwa katika nchi yenye demokrasia viongozi hupigiwa kura kuingia na kuondoka madarakani.
Zuma amekuwa chini ya shinikizo kutoka kwa makundi mbalimbali vikiwemo vyama vya wafanyakazi, biashara kubwa, vyama vya upinzani na wanachama wa chama chake kumtaka ajiuzulu.
Amekuwa akiandamwa na mlolongo wa kashfa za ufisadi wakati wa kipindi chake madarakani na kushutumiwa baada ya kumfuta waziri wake wa fedha aliyekuwa akiheshimiwa nchini humo Machi mwaka huu.