–Â Johannesburg
Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma amepewa muda wa kujifikilia kupendekeza adhabu ambayo mahakama kuu ya nchi hiyo inapaswa kutoa ikiwa atapatikana na hatia ya makosa ya dharau.
Adhabu hiyo inahusiana na kupuuza wito wa kufika mbele ya tume ya uchunguzi inayoongozwa na Jaji Ray Zondo kujibu tuhuma za ufisadi ambazo amekuwa akikana.
Mwezi Januari, mahakama ya katiba ya nchi hiyo ilimwamuru afike mbele ya tume hiyo, lakini akapuuza agizo hilo na mwezi uliopita, tume hiyo iliitaka mahakama imuhukumu rais huyo wa zamani kwa miaka miwili jela.
Mahakama hata hivyo ilizuia uamuzi katika kesi hiyo wakati huo Zuma alisema haogopi kwenda gerezani ikiwa mahakama zitaamua hivyo akielezea kwamba hakujitokeza mbele ya tume kwa sababu alikuwa amepoteza uaminifu kwenye mifumo ya haki.
Wakati huo huo mahakama ya rufaa Jumanne ilitetea uamuzi wa awali kwa serikali kupata pesa ambazo ilikuwa imezitumia kwa ada ya kisheria ya rais wa zamani.
Ilisema ufadhili wa serikali katika kesi hiyo ya ufisadi ulikuwa kinyume cha katiba na ni batili na inakadiriwa kuwa serikali ililipa kati ya dola milioni moja na milioni 2.2 kama gharama katika kesi hiyo.