26 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

ZUMA AIPASUA TENA ANC

PRETORIA, AFRIKA KUSINI

AWAMU ya pili ya utawala wa Rais Jacob Zuma imetawaliwa na matukio ambayo yamekitikisa chama tawala cha African National Congress (ANC) na kusababisha mgawanyiko ndani ya chama na wananchi kwa ujumla wake.

Wakati mgawanyiko na mpasuko huo ukitokea, rais wa zamani wa nchi hiyo, Thabo Mbeki, alikataa katakata kujihusisha na mtikisiko ndani ya ANC wala masuala ya kitaifa. Wengi waliamini kuwa Mbeki amesusia kutokana na hali iliyomtokea alipotolewa madarakani.

Zuma amenusurika mara mbili kung’olewa madarakani kupitia Bunge la nchi hiyo kufuatia matumizi mabaya ya fedha na ubadhirifu uliosababisha kuundwa tume ya uchunguzi. Matokeo ya tume hiyo iliyokuwa chini ya uenyekiti wa mwendesha mashtaka wa Serikali.

KUFUKUZWA WAZIRI WA FEDHA

Hatua ya Rais Zuma kufanya mabadiliko madogo katika baraza lake la mawaziri ambalo lilimtupa nje, Waziri wa Fedha, Pravin Gordhan, kumezusha malumbano makali ndani ya chama na wananchi kwa ujumla wake.

Tangazo la kubadilisha baraza la mawaziri lilitolewa juzi ambapo Zuma alimwondoa katika nafasi yake Gordhan na kumteua waziri mwingine kushika wadhifa huo.

Kutokana na kuondolewa katika nafasi yake muda mfupi baada ya kupigiwa simu ya kusitisha ziara zake katika nchi za Uingereza na Marekani, Waziri Gordhan, amezungumza na waandishi wa habari na kusema amechoshwa kusikia kwamba alifanya mikutano ya siri kuihujumu Serikali.

Kufutwa kazi kwa Gordhan anayeheshimika na kutajwa kuwa ni mchapakazi na mwadilifu, kumesababisha hasira dhidi ya Rais Zuma hata kutoka kwa vigogo wa ndani ya chama cha ANC, akiwemo Makamu wa rais, Cyril Ramaphosa.

Zuma amemteua, Malusi Gigaba ambaye alikuwa waziri wa mambo ya ndani kuchukua nafasi ya Gordhan. Gigaba ni mfuasi mzuri wa Zuma na ambaye mara zote amekuwa tayari kumtetea Rais Zuma licha ya kwamba rais huyo anakabiliwa na tuhuma lukuki za ufisadi na ongezeko la mashtaka ya kisheria.

Alipata ukosoaji mkubwa baada ya kuanzisha sheria ngumu ya upatikanaji wa viza ya kuingia nchini humo, hatua iliyoathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya utalii na ambaye pia ana uzoefu mdogo kuhusu masuala ya uchumi.

Raia wengi nchini Afrika Kusini walimchukulia Gordhan kama mlinzi bora wa uchumi ambao hadhi yake ya viwango inaweza kushushwa kabisa na taasisi za kimataifa zinazotoa makadirio ya mikopo katika siku chache zijazo.

Kutimuliwa kwa Gordhan ni pigo jingine kwa nchi hiyo iliyostawi zaidi kiviwanda barani Afrika, ambayo uchumi wake ulikuwa kwa asilimia 0.5 mwaka jana na kukabiliwa na mzozo wa ukosefu wa ajira kwa asilimia 27.

Mamia ya waandamanaji walikusanyika nje ya ofisi za wizara ya fedha ambako Gordhan aliwaambia waandishi wa habari kwamba inamchosha kusikia akituhumiwa kwa kuendesha mikutano ya siri inayolenga kuidhoofisha Serikali.

Makamu wa Rais, Cyril Ramaphosa, ambaye anaonekana kama mgombea anayeweza kuchukua madaraka kutoka kwa Rais Zuma kama kiongozi wa chama tawala, kwenye mkutano ujao wa Desemba mwaka huu, aliita hatua ya kumtimua Gorharn kuwa isiyokubalika.

Hatua hiyo ya Rais Zuma kumtimua Gordhan imechochea mpasuko ndani ya chama kikongwe cha ANC, huku upinzani ukiapa kupinga hatua hiyo mahakamani.

Gordhan ni miongoni mwa mawaziri 10 waliopitiwa na mabadiliko kwenye baraza la mawaziri lenye idadi jumla ya mawaziri 35, yaliyofanywa na Rais Zuma na mawaziri wapya wameapishwa jana.

Mabadiliko haya ya baraza yanakuja wakati kukiongezeka kwa shinikizo la kumtaka Zuma kuachia ngazi.

“Ni bunge ndilo lilimpa kazi Zuma na ni bunge ndilo linaweza kumfuta kazi," amesema kiongozi wa chama cha upinzani cha Democratic Alliance, Mmusi Maimane, ambaye alisema jana kuwa chama chake kitazindua mchakato wa kura ya kutokuwa na imani na Rais.

MGAWANYIKO NDANI YA ANC

Hatua ya kufutwa kazi kwa Waziri wa Fedha, Pravin Gordhan, imesababisha mgawanyiko katika chama tawala ANC. Mbali na mgawanyiko huo, thamani ya Rand imeshuka.

Matamshi ya Makamu wa Rais, Cyril Ramaphosa kupingana na Rais Zuma juu ya kuondolewa waziri Gordhan yameonyesha wazi hali ya ndani ya chama hicho.

Ramaphosa ambaye siku zote amekuwa akimuunga mkono Zuma, ameonesha wazi hali ya mgawanyiko ndani ya chama hicho tawala.

Hata hivyo, vuguvugu la wanawake na vijana katika chama hicho kwa pamoja yameunga mkono mabadiliko hayo na kusema ni ya manufaa kwa watu weusi nchini humo.

Vyama vya upinzani navyo vimelaani hatua hii na kudai, Gordhan alikuwa katika mstari wa mbele kupambana na ufisadi na kuwazuia washirika wa Rais Zuma kuiba fedha za umma.

Hata hivyo, Zuma na wafuasi wake wamekuwa wakimshutumu Waziri huyo wa zamani kuhusika na masuala ya ufisadi kwa kushirikiana na familia ya matajiri wa Kihindi ya Guptas.

KASHFA TANO

Rais Zuma amekuwa akikipasua chama cha ANC kutokana na kuandamwa na kashfa mbalimbali. Kashfa tano ambazo zimekichafua chama chake ni kama zifuatavyo;

1. Nenegate

Mnamo Novemba mwaka jana Rais Zuma alichukua uamuzi wa pupa kwa kumfukuza kazi waziri wa fedha wa zamani, Nhlanhla Nene.

Uamuzi huo uliigharimu Serikali na kubainishwa ulikuwa mbovu kupindukia ambapo ulisababisha kupoteza kiasi cha fedha randi bilioni 99.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya takwimu nchini humo Serikali italazimika kugharimia randi bilioni 250 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo ili kusimamia sera ya elimu bure vyuo vikuu. Kashfa hiyo iliitwa Nenegate sababu ya jina la Waziri Nene.

2. Kashfa ya Nkandla

Ukarabati wa makazi yake ya Nkandla, ulisababisha mtikisiko ndani ya chama ambapo Rais Zuma aligundulika kutumia fedha za umma kugharamia shughuli hiyo. Kashfa ilielezwa na Mahakama ya nchi hiyo kuwa Rais Zuma alivunja katiba ya nchi.

Aidha, kwa mujibu wa Tume ya uchunguzi, Zuma alivunja Ibara ya 83(b) na vifungu vya 181(3) na 182(1)(c). mahakama ilimwamuru kurudisha fedha zote za umma.

3. Kashfa ya ‘Mr 783’

Mnamo Aprili mwaka jana, Mahakama Kuu ya Pretoria ilieleza kuwa lilikuwa kosa kwa uamuzi wa kuondoa mashtaka ya ulaji rushwa ya mwaka 2009 dhidi ya Zuma.

Jaji Aubrey Ledwaba, alihoji usiri uliokuwepo katika uamuzi wa kuondoa mashtaka hayo na kwamba yalikuwa kinyume cha katiba.

4. Kupoteza majimbo

Chama cha ANC kimepoteza majimbo mbalimbali katika uchaguzi uliopita wa Serikali za Mitaa. Miongoni mwake ni Jimbo la Tshwane ambalo lilichukuliwa na chama cha upinzani cha Democratic Alliance (DA).

Aidha, chama cha upinzani cha DA kilishinda majimbo ya Johannesburg na Nelson Mandela Bay. Hii ilikuwa ni ishara ya wazi kuwa Zuma alipoteza mvuto ndani ya chama na chama chenyewe nacho kilipoteza mvuto. Lakini ANC kilikataa kumwondoa madarakani Zuma.

5. Kukwapua ripoti

Ripoti ya Mwendesha mashtaka mkuu wa zamani, Thuli Madonsela, ilinaswa na maofisa wa Zuma kabla haijapelekwa kusomwa bungeni ambapo ilionyesha namna rais huyo alivyokiuka maadili ya uongozi.

Aidha, ripoti hiyo ilionyesha uhusiano kati ya mtoto wa Zuma, Duduzane na familia ya Gupta, hali ambayo ingemtia hatiani Zuma kutokana na kuwa na mgongano wa kimasilahi.

Ili kuficha taarifa hiyo alilazimika kukwapua na kuielekeza tume ya uchunguzi kuondoa uwezekano wowote wa nyaraka zinazoonyesha uhusiano wa mtoto wake Duduzane na familia ya Gupta.

Ilielezwa kuwa Zuma alichakachua sehemu zote za ripoti zilizoonyesha uhusiano wa familia yake na Gupta.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles