26.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, January 18, 2022

MSAJILI ABARIKI SAKAYA KUKAIMU NAFASI YA MAALIM SEIF

Na EVANS MAGEGE,

OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, imebariki ombi la Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi(CUF) Taifa Profesa Ibrahim Lipumba la kumkaimisha Ukatibu Mkuu Magdalena Sakaya.

Hivi karibuni Profesa Lipumba alitangaza kumvua madaraka hayo Maalim Seif Sharif Hamad, kwa madai kuwa amekaidi wito wake na kususia ofisi kwa miezi kadhaa.

Kwa mujibu wa barua iliyosambaa  jana kwenye mitandao ya kijamii, imeeleza kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imejiridhia kisheria na kukubaliana na ombi hilo baada ya kupitia vifungo vya Katiba ya CUF.

Barua hiyo ambayo imeandikwa Machi 21, mwaka huu  yenye kumbukumbu namba HA.322/362/14/74 imetiwa saini na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza imemtaka Profesa Lipumba kurejea barua yake yenye kumbukumbu namba ya CUF /AK/DSM/MKT/02/2017 ya Machi 16,  mwaka  huu.

“ Msajili wa Vyama vya Siasa amepokea taarifa  uliyowasilishwa kuhusu Magdalena  Sakaya kukaimu  nafasi ya Katibu Mkuu wa CUF kwa mujibu wa ibara ya 93(3)ya Katiba ya CUF toleo la mwaka 2014, kutokana na Maalimu Seif  Sharif  Hamad kushindwa kutekeleza majukumu yake.

“ Ofisi imesoma Katiba ya Chama chenu (CUF)  na kujiridhisha kuwa ni kweli kwamba ibara ya 93 (3) imeelekeza hivyo.     Hivyo , Ofisi ya Msajili  wa Vyama vya Siasa itampa ushirikiano unaostahili Magdalena  Sakaya  katika kutekeleza majukumu ya Katibu Mkuu wa CUF,” barua hiyo imefafanua.

Akithibitisha kupokewa kwa barua hiyo Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma wa Chama cha Wananchi (CUF), Abdul Kambaya, alisema barua hiyo wameipokea.

Kambaya ameshangazwa na kitendo cha watu kuipiga picha barua hiyo na kuisambaza kwenye mitandao ya kijamii wakati jambo hilo linahusu mambo ya ndani ya chama.

“Hayo ni mambo ya chama na msajili wa vyama, sasa kama barua hiyo ipo wao kinachowafanya waisambaze ni nini? aliyeiandika kwa lengo la kutambulisha maamuzi ya vikao ni Profesa Lipumba ambaye aliituma kwa msajili,  msajili kama kajibu kwa kufuatana na Katiba ya CUF tatizo liko wapi?

“ Ni kweli tumepewa na msajili hiyo barua, hawa wanaoisambaza kwenye mitandao ya kijamii tunajua  wamepewa na vyanzo vyao vya kifisadi huko vinaoweza kuiba nyaraka. 

“Lakini ni kweli hii barua ni ya wazi na si ya siri  hata hivyo hatukuweza kuisambaza kwa sababu haihusiani na wananchi huko nje ni mambo ya chama ya ndani,” alisema Kambaya.

Gazeti hili liliwasiliana na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kutaka kufahamu kama ofisi yake imeandika barua hiyo, hakuwa tayari kuzungumza chochote kuhusu suala hilo.

“ Siwezi kuongea chochote kwa njia ya simu, njoo ofisini nitakujibu,” alisema Jaji Mutungi.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
174,926FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles