33.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

ZITTO: NINGEFANYA TOFAUTI

Na Zitto Kabwe        |       


KWA miaka kadhaa nimekuwa mtu ninayeamini katika kujipa muda wa upweke na kutazama dunia iliyonizunguka na kujiuliza maswali ama kunihusu mimi binafsi au kuhusu nchi yangu na Afrika.

Waingereza wangesema self reflection lakini ninapenda kutumia neno la lugha ya Kiswahili; kutafakari. Ninaamini kwamba ni muhimu kwa kiongozi kupata muda huu muhimu.

Siku chache zilizopita, nilijipa muda huo wa utulivu kwa ajili ya tafakari. Swali kuu nililokuwa nikijiuliza ni hili; kwamba kama ningekuwa nimepewa mamlaka ya kuongoza Tanzania nini ningefanya tofauti na wanaoongoza sasa?

Katika tafakari hii nilikumbuka safari niliyofanya wilayani Ludewa, Mkoa wa Njombe mwaka 2011 kukagua na kutoa nguvu kwa uwekezaji wa kimkakati wa uchimbaji madini ya chuma na makaa ya mawe na kuweka msingi wa viwanda mama nchini kwetu.

Nadhani ningeanza na mradi huu kabla ya kitu kingine chochote. Nina sababu za kufikia hitimisho hilo.

Mchuchuma na Liganga ni nini?

Madini ya chuma na makaa ya mawe ndiyo msingi wa maendeleo ya viwanda duniani kote. Nchi yetu ina madini haya yote kwenye eneo moja, wilayani Ludewa. Hakika Mungu alitupenda, maana aliumba dunia na akaisanifu Ludewa na kuiweka Tanzania ili iwe chanzo cha viwanda mama.

Katika eneo la Mchuchuma kuna mashapo yenye tani bilioni 1.2 makaa ya mawe yenye uwezo wa kuzalisha umeme megawati 600 kwa miaka 150. Makaa hayo pia hutumika kuyeyusha chuma na kuzalisha chuma cha pua. Vilevile eneo la Liganga lina mashapo ya madini ya chuma tani bilioni mbili ambayo ndani yake kuna madini yenye thamani kubwa ya Titanium na Vanadium.

Ujenzi wa kilometa moja ya reli unahitaji chuma cha pua (steel) chenye ubora wa hali ya juu kiasi cha tani 40 mpaka 60. Tanzania tunajenga kilomita 1,200 za reli kwa sasa hivi na baadaye zitaongezeka kwa vipande vya Tabora – Kigoma, Kaliua – Mpanda – Karema, Uvinza – Musongati na miradi mingine kama Mtwara – Mbamba Bay, Ruvu – Tanga, Tanga – Musoma – Kigali nakadhalika. Kwahiyo, Tanzania itahitaji si chini ya tani 500,000 za chuma cha pua katika kipindi cha miaka michache ijayo.

Afrika nzima inajenga reli za kisasa na zote zinahitaji chuma kwa ajili ya kujenga njia za reli.Nchi za Kenya na Ethiopia wamemaliza hatua za kwanza za ujenzi wa reli zao ambapo Kenya imeshajenga kilometa 485 kutoka Mombasa mpaka Nairobi na Ethiopia kilometa 760 kutoka Addis Ababa mpaka Djibouti. Miradi yote hii mataruma ya reli yameagizwa kutoka nje na kuletwa Afrika na hivyo kuzalisha ajira huko kwenye nchi hizo (ambazo mataruma hayo yamezalishwa ).

Fedha za miradi hii zitakwenda nje ya nchi, Waafrika hawatafaidika kabisa. Tanzania nayo inakwenda njia hiyo hiyo licha ya kwamba ina madini ya chuma na makaa ya mawe ya kuzalisha chuma cha pua ambacho huzalisha mataruma ya reli na bidhaa nyingine kadha wa kadha za ujenzi wa reli. Tanzania ingeamua, ingeweza kulisha miradi yote ya reli chuma kutoka Ludewa katika nchi za Kongo, Zambia, Angola, Uganda na Rwanda ambao wote wana miradi ya ujenzi wa reli na wamepanga kuagiza chuma kutoka China na kwingineko.

Bei ya tani moja ya chuma kwenye soko la dunia ni Dola za Marekani 600 sawa na (Sh milioni 1.3) hadi 1000 (Sh milioni 2.2). Kwa hiyo Tanzania ikizalisha chuma tani milioni moja tu kwa mwaka, inaweza kupata mapato ya fedha za kigeni kati ya dola za Marekani milioni 600 (sawa na Sh bilioni 13.6)hadi bilioni moja kwa mwaka. Kwa mashapo yaliyopo Tanzania, tunaweza kuzalisha kiwango hicho cha chuma kwa miaka zaidi ya 2000 na chuma cha Ludewa kisiishe.

Kwa hakika mahitaji ya chuma yatakuwa ni makubwa na tunaweza kuzalisha na kuuza nje mpaka tani milioni tano kwa mwaka. Hivi sasa nchi ya Australia ndiyo inaongoza duniani kwa kuuza chuma kingi zaidi. Mwaka 2017 waliuza tani milioni 49 za chuma na kupata Dola za Marekani bilioni 49.

Jambo kubwa ambalo Tanzania imebahatika ni kwamba mashapo ya chuma yana madini mengine yenye thamani kubwa zaidi. Kwa mfano Vanadium ya Ludewa inauzwa tani moja Dola za Marekani 50,000 sawa na (Sh 113,970) katika soko la dunia. Katika kila tani milioni moja ya chuma kutoka Ludewa, kuna tani 80,000 ya Vanadium. Tukiuza madini haya tunapata fedha za kigeni Dola za Marekani bilioni nne saw na (Sh. Trilioni 9.1) kwa mwaka.

Unapokuwa na mamlaka ya uongozi wa nchi unakumbana na changamoto nyingi na moja ya changamoto ni kuamua uanze na nini katika vipaumbele vya nchi ili kupiga hatua za kimaendeleo. Kiongozi mwenye maarifa huanza na mambo yatakayomwezesha kupata rasilimali fedha ili atekeleze majukumu mengine. Ni dhahiri hapa nchini tuna changamoto ya miundombinu ya usafirishaji, reli, barabara na hata usafiri wa anga.

Viongozi wetu wa sasa wameamua kuanza na hayo kwa kutumia fedha za kodi au mikopo ghali yenye riba kubwa kutoka benki za biashara za nje. Wameanza na ujenzi wa reli wa dola bilioni saba za Marekani, ununuzi wa ndege wa zaidi ya dola bilioni moja (Dreamliner ‘Terrible Teen’) imenunuliwa kwa Dola za Marekani milioni 224 na hata ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Rufiji maarufu kwa jina la Stiglers Gorge litakalogharimu dola bilioni 3.5.

Yote haya yanahitaji kukamua kodi wananchi na kuchukua mikopo inayokuza Deni la Taifa. Yote haya yanasababisha mzunguko wa fedha nchini kuwa mdogo kwa sababu fedha zinatoka nje ya nchi kulipia wakandarasi na kununua malighafi kama chuma.

Ningekuwa na mamlaka ningeyafanya haya yote, kabla ya kufanya hayo, ningeanza kwanza kwa kufanya jambo moja kubwa ambalo lingenipa fedha za kufanya hayo.

Ningefanya tofauti.

Ningeanza na mradi wa Mchuchuma na Liganga kwa kuhakikisha kuwa uwekezaji unaanza mara moja na uzalishaji wa chuma na makaa ya mawe unafanyika bila kuchelewa. Ningehakikisha kuwa ndani ya miaka 2 tunaanza uzalishaji wa chuma, Vanadium na Titanium.

Mauzo ya Vanadium peke yake ni sawa na dola bilioni nne kwa mwaka ambapo kwa kuwa haya ni bidhaa ambatana na chuma maana yake asilimia  80 ya mapato haya yangekuwa ya nchi. Kwa hiyo mwaka wa kwanza tu wa uzalishaji ningeweza kupata Dola za Marekani bilioni 3.2. Kwa fedha hizo, tungejenga reli kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma kwa mara moja bila kuungaunga na kubakia na chenji ya dola bilioni moja ambazo ningeweza kujenga hospitali tano kubwa kama Mloganzila katika kanda tano za nchi; Mbeya, Mtwara, Mwanza, Kigoma na Arusha.

Ningeweza kujenga vyuo vya VETA kila Mamlaka ya Serikali za Mitaa nchini ( Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji ) kwani unahitaji Sh bilioni 750 tu kujenga vyuo hivyo vilivyokamili na vifaa vya kutosha vijana kupata mafunzo.

Ningeweza kujenga vyuo vikuu vipya vitatu aina ya UDOM kwani UDOM moja ina thamani ya Sh bilioni 800 tu. Haya ni mapato ya mwaka wa kwanza tu. Kumbuka kuwa tunaweza kuendelea kuchimba chuma tani milioni moja kwa mwaka kwa miaka 2000!

Tungeamua kuzalisha tani milioni tano kwa mwaka maana yake mapato ya Vanadium peke yake kwa mwaka yangekuwa Dola za Marekani bilioni 16 sawa na (Sh Trilioni 36.4) ambazo ni sawa na kumaliza reli yote mpaka Kigoma na Mwanza na kuiwezesha Air Tanzania kuwa na ndege kubwa na ndogo sawa na Shirika la Ndege la Ethiopia na hata kuzalisha umeme zaidi ya megawati 10,000 ndani ya miaka mitano kwa kutumia makaa ya mawe, geo thermo, gesi asilia, upepo na jua – yote hayo bila kuathiri hifadhi ya Selous.

Kwa kuzalisha tani milioni tano kwa mwaka tungezalisha chuma, Vanadium na Titanium kwa miaka 400 mpaka kumaliza mashapo yote tuliyonayo. Kwanini hatuwekezi Mchuchuma na Liganga?

Kungoza nchi kunahitaji maarifa. Hakika Ningefanya tofauti.

MAKALA HAYA YAMEANDALIWA NA ZITTO KABWE

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles