PATRICIA KIMELEMETA, DAR ES SALAAM
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeitupa kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na viongozi wa tatu wa vyama vya upinzani wakiongozwa na Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe.
Zitto na wenzake Salim Bimani na Jorani Bashange wa CUF, walifungua kesi hiyo wakipinga muswada wa marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa huku mahakama ikiwataka kulipa gharama za uendeshaji wa kesi hiyo.
Kesi hiyo namba 31 ya mwaka 2018 ilifunguliwa Desemba 20, mwaka jana chini ya hati ya dharura na Umoja wa Vyama vya Upinzani nchini ambao wanapinga muswada huo kujadiliwa bungeni kwa minajili ya kuupitisha kuwa sheria kwa sababu unakinzana na katiba ya nchi.
Walalamikiwa katika kesi hiyo ni Serikali na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa na Jaji Dk. Benhajj Masoud huku upande wa Serikali ukiwakilishwa na mawakili wakuu wa Serikali, Ponsiano Lukosi, George Mandepo na Rehema Mtulia wakati upande wa waleta maombi ukiwakilishwa na mawaliki Mpare Mpoki, Daimu Khalfani, Stephen Mwakibolwa na Jeremiah Ntobesya.
Akisoma uamuzi wa kesi hiyo jana, Jaji Masoud alisema uamuzi wa kuitupa umetokana na uwasilishwaji wa maombi mawili kwenye kesi moja.
Alisema katika ombi moja waleta maombi waliitaka mahakama kukifuta kifungu namba 8 (3) cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi za Binadamu na Wajibu kilichopo kwenye muswada wa marekebisho ya sheria inayotarajiwa kusomwa bungeni.
Jaji Masoud alisema ombi la pili waleta maombi wanapinga maudhui ya muswada huo, pamoja na mambo mengine wakidai unapora haki na mamlaka ya vyama vya siasa na kufanya shughuli za kisiasa kuwa jinai.
Alisema kimsingi maombi hayo ni muhimu, lakini hayawezi kuletwa kwa wakati mmoja, hivyo basi waleta maombi walipaswa kuleta ombi la kwanza wakasubiri uamuzi ndipo walete ombi la pili.
Jaji Masoud alisema kutokana na hali hiyo mahakama ilijikita katika ombi la kwanza la kifungu namba 8 (3) kwa sababu ndicho kinachotoa dira ya usikilizaji wa kesi hiyo.
Alisema baada ya kukipitia na kupitia hoja za pande zote mbili, mahakama imeamua kukubaliana na hoja ya wajibu maombi (Serikali) na kuona haina haja ya kuendelea na kesi hiyo kwa sababu maombi hayo hayakupaswa kuwasilishwa pamoja.
“Mahakama imeamua kuifutilia mbali kesi hiyo baada ya kupitia hoja za pande zote mbili kwa sababu waleta maombi walipaswa kuleta ombi moja likishatolewa uamuzi ndipo walete ombi lingine,” alisema Jaji Masoud.
Alisema mahakama imewataka waleta maombi kulipa gharama zote za uendeshaji wa kesi hiyo kama zilivyoombwa na wajibu maombi katika hoja zao 10 walizowasilisha mahakamani.
KAULI YA ZITTO
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama Kuu baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, Zitto alisema wanafungua kesi nyingine mahakamani hapo ili waweze kuendelea na mpango wao wa kutetea demokrasia nchini.
“Mahakama ni sehemu ambayo tunaamini tunaweza kupata hali zetu za kidemokrasia, hivyo basi tumewasiliana na mawakili wetu ili waweze kufungua kesi nyingine kwa ajili ya kutetea demokrasia,” alisema Zitto.
Awali katika kesi hiyo, waleta maombi waliiomba Mahakama Kuu kukifuta kifungu namba 8(3) cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi za Binadamu na Wajibu kilichopo kwenye muswada wa marekebisho ya sheria inayotarajiwa kusomwa bungeni pamoja na kupinga maudhui ya muswada huo kwa madai kuwa unapora haki na mamlaka ya vyama vya siasa na kufanya shughuli za kisiasa kuwa jinai.
Waleta maombi hao walidai kuwa muswada huo unalenga kumfanya Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa na mamlaka ya usimamizi, kuwa na mamlaka ya kuingilia shughuli za kiutawala na maamuzi ya ndani ya vyama vya siasa ikiwemo kusimamisha na kumfukuza mtu uanachama, jambo ambalo linakinzana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na marekebisho yake.