28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Masauni: Tanzania ipo kwenye mabadiliko ya uchumi


Mwandishi Wetu – dar es salaam

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, amewataka Watanzania kuimarisha umoja na kumuunga mkono Rais Dk. John Magufuli kwa kumwombea dua katika kipindi hiki ambacho nchi inapitia kipindi cha mabadiliko makubwa ya kiuchumi.

Hayo aliyasema mwishoni mwa wiki Dar es Salaam alipomwakilisha Rais Magufuli katika dua maalumu ya kumwombea na kuombea amani katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa.

Dua hiyo iliyoandaliwa na Taasisi ya Dini ya Maridhiano Tanzania ilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Sabasaba.

Masauni alisema nchi sasa inapitia kipindi cha mabadiliko makubwa ya kiuchumi yanayosimamiwa na Rais Magufuli, lengo likiwa ni kuifanya Tanzania isiwe tegemezi na kupewa masharti yanayodhalilisha mila, tamaduni na dini zetu.

“Watanzania tumuunge mkono Rais Magufuli, anayoyafanya ni kwa faida ya Watanzania wote bila kujali dini, rangi, kabila au itikadi na hatutakuwa tayari kupangiwa na wageni ambao wanatuletea mambo ya hovyo, demokrasia ya nchi yetu tunaijua wenyewe Watanzania na sio aje mtu kutoka nje atuambie demokrasia ya kufuata, hawezi kuja mtu atupangie tufuate mambo ya ushoga,” alisema Masauni.

Akizungumza katika dua hiyo, Sheikh Nurdin Mangochi aliwataka Watanzania waitunze amani iliyopo na wala wasikubali kushawishiwa na mtu yeyote kuvuruga amani iliyopo.

“Kuna nchi jirani amani imetoweka na tunaona madhara yake, muhimu hii amani tuliyonayo tuitunze na kuilinda kwani nchi yetu Tanzania imekuwa darasa la amani kwa nchi jirani wanaokuja kujifunza jinsi Watanzania tunavyoishi bila kuwepo machafuko,” alisema Sheikh Mangochi.

Naye Askofu Silvestre Gamanywa aliwataka Watanzania kuwa na uzalendo na nchi yao kwa kuiongelea mema katika maisha yao yote hali itakayosababisha kuwapo na mapenzi ya nchi kwa kila Mtanzania.

“Uzalendo sio lazima kufia nchi yako, uzalendo ni kuwa na mtazamo chanya wa kuisemea na kuitetea nchi yako pamoja na kuitakia mema na sio kuiongelea vibaya,” alisema Askofu Gamanywa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles