27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Zitto, Lissu waibwaga Serikali bungeni

Pg 1b *Ilitaka kupitisha hoja kwa kuvunja taratibu wakashtukia

*Wamtaka Rais Magufuli awawajibishe AG Masaju na Dk. Mpango

Na Elias Msuya

WAZIRI  wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, jana alijikuta katika wakati mgumu na kulazimika kuitoa hoja yake aliyoiwasilisha ya Mapendekezo ya Mwelekeo wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21, baada ya wabunge wa upinzani kudai kuwa Kanuni za Bunge na Katiba imekiukwa.

Dk. Mpango alifikia hatua hiyo baada ya wabunge wa upinzani, akiwemo Zitto Kabwe (ACT) na Tundu Lissu (Chadema) kuomba mwongozo kwa nyakati tofauti wakisoma Kanuni za Kudumu za Bunge ibara ya 94(1) na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ibara 63(3c), wakisema Serikali imekosea kuwasilisha mapendekezo ya mwelekeo huo badala ya mpango wa maendeleo wa mwaka 2016/17- 2020/21.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, katika hitimisho lake alisema Katiba haikukiukwa, bali utaratibu tu.

Waziri Mpango aliwasilisha hoja yake kabla ya kipindi cha Maswali na Majibu, ikiwa ni miongoni mwa hoja nne zilizowasilishwa.

Baada ya kipindi cha maswali na majibu, saa 4:30, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, alikataa kupokea maombi ya miongozo kutoka kwa wabunge wa upinzani na kumwalika Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kuwasilisha Mapendekezo ya Mwelekeo wa Mipango wa Pili wa Maendeleo wa miaka mitano wa mwaka 2016/17- 2020/21.

Baada ya hotuba hiyo, Chenge aliruhusu maombi ya miongozo kutoka kwa wabunge wa upinzani, ambapo Zitto na Lissu walipinga uwasilishwaji wa Mwelekeo wa mpango huo.

Akiomba mwongozo wake, Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Mjini, alinukuu Katiba ya Jamhuri ya Muungano, akiitaka Serikali ilete mpango wa maendeleo.

“Waziri hajaleta mpango, Bunge halitakiwi kujadili mwelekeo wa mpango. Wabunge bila kujali vyama vyetu tunajidhalilisha kujadili mwelekeo, hakuna cha kujadili, Kanuni ya 68 inatukataza,” alisema Zitto.

Naye Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki, alimuunga mkono Zitto akinukuu Kanuni ya 94.

Hata hivyo, Chenge alisema amezichukua hoja zao na atazijibu baadaye na wakati huo akamkaribisha Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Hawa Ghasia, ambaye aliwasilisha tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka mitano 2011/12-2015/16 pamoja na Muundo wa Mwelekeo wa Mpango wa Pili wa Maendeleo.

Kabla Ghasia hajaanza kuzungumza, Zitto alisimama na kutoa hoja ya kuhitimisha mjadala kwa kanuni ya 62. Lakini Chenge alimwambia Zitto atulie, kwani hoja hiyo imeanzia kanuni ya 62.

Wakati Ghasia anaendelea kuwasilisha, Lissu alionekana akienda kushauriana na Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, huku Zitto Naye akishauriana na baadhi ya wabunge wa upinzani.

Baada ya Ghasia kuwasilisha hotuba yake, Chenge alimwalika msemaji wa kambi ya upinzani wa Wizara ya Fedha na Uchumi, David Silinde.

Silinde ambaye ni Mbunge wa Momba, alipofika mbele aligoma kusoma taarifa ya upinzani, akidai kuwa Katiba imekiukwa.

“Kwa kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ibara ya 63(3c) imekiukwa na kwa kuwa Kanuni ya Bunge ya 94(1) nayo imekiukwa, Kambi ya upinzani haitawasilisha Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa kwa Kipindi cha miaka mitano,” alisema Silinde.

Baada ya kauli hiyo ya Silinde, Chenge alisimama na kusema kwa kuwa hoja ilishawekwa mezani iendelee kujadiliwa hadi itakapotolewa.

“Hoja ikishawekwa mezani tunaendelea… nasema hivyo ili kuepusha matukio kama haya. Ukishawasilisha mezani lazima uombe kuutoa tena…” alisema Chenge.

Hata hivyo, baada ya Chenge kushauriana na mawaziri waliokuwa wakijadiliana kwa muda mrefu kwenye viti vyao, alitangaza kuahirisha Bunge ilipofika saa 6:25.

 

Waziri Mpango aondoa hoja bungeni

Baada ya Bunge kurejea saa tisa alasiri, Chenge alitoa ufafanuzi akisema kilichokosewa ni kukiukwa kwa kanuni na siyo Katiba, hata hivyo, alikiri kutokuwepo kwa Katiba.

“Ili twende vizuri, kwa wale wenye Katiba, maana kulikuwa na madai mazito kidogo ya ukiukwaji wa Katiba katika ibara ya 63(3c)… Hoja ilikuwa ndiyo hiyo, hatuwezi kukiuka. Pili, sheria hiyo iko wapi? Mpango wenyewe uko wapi?

“Nimelitafakari sana suala hili na baada ya hapo niseme wazi kabisa hakuna ukiukwaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Kilicholetwa na Serikali ni mchakato wa kuwashirikisha wananchi wa Tanzania ili watoe maoni…”

Chenge alisema kwa mujibu wa kanuni ya 94 fasili ya kwanza, Bunge linapofanya kazi hiyo haliketi kama Bunge, linaketi kama kamati ya mipango.

“Suala la kukiuka Katiba ni hoja nzito sana, ni suala la kughafilika tu, badala ya kukaa kama kamati, tumekaa kama Bunge.

“Mimi nashauri serikali kupitia kanuni ya 58(5) ambayo inaruhusu kwa hoja ambayo haijaamuliwa inaweza kuondolewa. Hiyo ndiyo njia sahihi nyoofu inayozingatia Katiba na kanuni, lakini nasisitiza hatujavunja Katiba…” alisema Chenge.

Akiondoa hoja hiyo, Waziri Mpango alisema:

“Kutokana na maelezo uliyoyatoa na kwa kutumia kanuni ya 58 (5)… ninaomba ruhusa ya kuondoa hoja niliyowasilisha leo asubuhi ya Mpango wa pili wa maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2016/17 – 2020/21,” alisema Dk. Mpango.

Zitto na Lissu wafafanua

Baada ya kuahirishwa kwa kikao cha Bunge kwa mara ya kwanza saa sita mchana, wabunge Zitto na Lissu waliwaita waandishi wa habari na kufafanua hoja yao.

Lissu alisema Kanuni za Kudumu za Bunge zinasema kila mwezi Oktoba na Novemba Serikali inatakiwa iwasilishe mpango wa maendeleo wa mwaka na katika mwanzo wa mwaka Serikali inatakiwa iwasilishe mpango wa maendeleo wa miaka mitano.

“Cha kwanza kinachotakiwa na kanuni za kudumu za Bunge, ni kuletwa mpango wa miaka mitano, unajadiliwa kwa siku tano na kuidhinishwa na kutungiwa sheria ya utekelezaji. Ni matakwa ya sheria, Katiba ibara ya 63(3c),” alisema Lissu na kuongeza:

“Serikali ilitakiwa ilete mpango wa muda mrefu wa miaka mitano na muda mfupi wa mwaka mmoja. Hatujaletewa chochote kinachotakiwa na Katiba kuidhinisha na kukitungia sheria ya kutekeleza. Sasa wanataka kufunika kombe kama alivyokuwa anataka mwenyekiti.”

Alisema miaka mitano iliyopita uliletwa Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2011/12-2015/16 na mpango mfupi, ukajadiliwa na ukapitishwa.

“Kwa sababu ya weledi mdogo wa serikali iliyopita, hatukutunga sheria ya utekelezaji kama inavyotakiwa na Katiba. Ubovu wa Serikali ya Kikwete (Rais mstaafu Jakaya) umehamia Serikali ya Hapa Kazi tu, Serikali ya Magufuli (John).

“Kuna siku tano ambazo wabunge tutakuwepo hapa Dodoma, tunajadili kitu ambacho hakipo?” alihoji Lissu.

Kutokana na hali hiyo, Lissu alisema ndiyo matokeo ya malalamiko yao ya kuvurugwa kwa Kamati ya Bunge.

“Kwa nini kamati zimevurugwa? Hili lisingetokea kama wajumbe wa Kamati ya Bajeti ya Bunge lililopita wangekuwepo kwenye miaka mitano ya bajeti, maana wangekuwa na kumbukumbu.

“Kina Chenge ambaye alikuwepo wangeuliza uko wapi. Wamewekwa watu wapya kabisa. Matokeo yake wamewekwa watu wapya hawajui watendalo, Mungu awasaidie,” alisema.

“Tusingeingia katika hii aibu, kwa sababu hakuna mpango, kilichobaki sasa ni kujikoshakosha tu. Tutajadili kitu gani, tutaidhinisha kitu gani?”

Lissu pia alisema ndiyo maana Serikali inakataza matangazo ya moja kwa moja ya televisheni ya TBC, akidai imeogopa aibu.

“Hii ndiyo maana wamekataza matangazo ya moja kwa moja ili kuziba aibu hii. Serikali ya Magufuli inafahamu uozo ulioko ndani ya Serikali, wanafahamu uwezo mdogo wa Serikali yao. Wanajua tutafichua uozo huu. Wanajua udhaifu wa Serikali ya Magufuli. Ukiruhusu ‘live broadcasting’ kila mtu ataona huu uozo,” alisema Lissu.

Kutokana na hali hiyo, Lissu alihoji Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango wameshindwaje, hili litapita hivi hivi? Wawajibishwe.

“Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa mujibu wa Katiba 59(3), ndiye anayeandaa miswada inayokwenda bungeni. Muswada wa mpango wa maendeleo ulitakiwa uandaliwe na muswada wa Serikali. Ndiye anayetakiwa kuishauri Serikali kuhusu sheria.

“Tulisema tangu awali, kwa nia njema kabisa kwamba George Masaju hawezi kuvaa viatu vya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Rais Magufuli anatumbua majipu, kama kuna jipu kubwa kwa sasa ni Masaju. Mimi ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, natoa ushauri wa bure…” alisema na kuongeza:

“Waziri Mpango naye ni jipu…Wenzake mwaka 2011 waliwasilisha mpango yeye akiwa Katibu Mkuu Mipango. Leo hajamaliza miezi mitatu, anatuthibitishia kuwa viatu vya Wizara ya Fedha ni vikubwa mno, havimtoshi.”

Akizungumzia mashauriano aliyofanya na baadhi ya mawaziri kabla ya Bunge kuahirishwa, Lissu alisema mawaziri wote wameonyesha kukubaliana na msimamo wa kambi ya upinzani.

“Mimi nimezungumza na mawaziri kadhaa pale, nimemwandikia Chenge pale… Nikaenda kwa Dk. Mwakyembe (ni bingwa wa Katiba nchini), nikaongea na mnadhimu wa CCM aliyepita, William Lukuvi, wote wamekubali kuwa kinachofanyika ni maajabu,” alisema Lissu na kuongeza:

“Wale mawaziri nimefanya nao mazungumzo wote wamekubali, hiki kitu kiko wazi, huwezi kupinga, hakuna tunachojadili.”

Lissu alidai kuwa tangu wakati wa semina ya wabunge waliomba kupewa nakala za Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano kama Kanuni zinavyoelekeza, lakini hawakupewa na badala yake walipewa taarifa za utekelezaji wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umasikini ya pili na taarifa za utekelezaji wa mpango wa kwanza wa maendeleo.

“Mapendekezo ya mpango wa maendeleo ni mnyama gani? Anatambuliwa wapi katika kanuni na Katiba hii? Bunge la Hapa Kazi tu, litalipa posho kwa siku tano kwa kwa kuidhinisha nini?” alihoji Lissu.

 

Zitto

Kwa upande wake Zitto, alisema jambo hilo limekiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano na halipaswi kuvumiliwa.

“Ni dhahiri kabisa kwamba shughuli ya kwanza ya Bunge badala ya hotuba ya Rais…ni mpango huu wa miaka mitano. Shughuli hii ya kwanza wameshindwa,”

“Kwa sababu wameona hili Bunge unaweza kulipeleka unavyotaka, waliamini kwamba kitu kitakuja na kitapita kwa namna wanayotaka wao. Walisahau kwamba hili Bunge limesheheni wabunge wenye uzoefu. Kwa sababu tulipitisha hii,” alisema Zitto.

Zitto alisema Serikali ya CCM imedhihirisha kuwa imeshindwa kuongoza nchi kwa kushindwa kufuata utaratibu uliowekwa.

“Kuna mtanziko, Serikali imethibitisha kuwa haiwezi kuongoza nchi, kwa sababu haya ni mambo madogo tu mnapaswa wayajue. Mnatakiwa mje na mpango kwanza, mnatakiwa muwe na sheria, hatujaletewa muswada wa sheria. Hakuna kilichobadilika kutoka utawala wa Rais Kikwete na huu wa sasa,” alisema Zitto.

Zitto aliendelea kuukosoa utawala wa Rais Magufuli, akisema hata hatua za kutumbua majipu ni geresha tu ya kuwapumbaza Watanzania wasiweze kuhoji.

“Juhudi hizi za kila siku mnasikia kila siku kukamua majipu, ni ‘spinning’ kuwaondoa watu kwenye attention. Kwa sababu kama watu wanaweza kugundua kuwa makontena yameibiwa na waziri mkuu akaenda, mnashindwaje kujua mambo madogo kama haya?” alihoji.

Aliwataka Waziri wa Fedha na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwajibika kwa kuvurugika kwa utaratibu huo.

“Lazima watu hawa wawajibike ili iwe fundisho kwa wengine,” alisema.

Huku akiitaka Serikali kuondoa hoja yake mezani, Zitto alisema hilo siyo jambo geni, kwani baadhi ya mawaziri walishaondoa hoja zao.

“Ni jambo jepesi tu. Chenge angeagiza tu Serikali ikalete mpango, maana hiki hatujui ni nini hakipo kwenye kanuni wala Katiba,” alisema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles