24.7 C
Dar es Salaam
Saturday, April 13, 2024

Contact us: [email protected]

CUF wampa mtihani mwingine Jecha

Jecha Salum JechaEVANS MAGEGE NA JONAS MUSHI

WAKATI wasomi wakiutazama msimamo wa Chama cha Wananchi (CUF) kususia marudio ya Uchaguzi Mkuu Zanzibar kama kinaweza kuibua kishindo kikali cha kisiasa visiwani humo, chama hicho kimewaelekeza wagombea wake wote visiwani Zanzibar kumwandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salum Jecha, kuomba kujitoa kwenye uchaguzi huo.

Tayari msimamo huo wa CUF uliotolewa juzi na Baraza Kuu la chama hicho umeanza kuibua hisia tofauti miongoni mwa wachambuzi wa kisomi na jamii kwa ujumla ambapo baadhi wanadai hali hiyo inaweza kufufua makaburi ya chuki za kisiasa zilizowahi kujitokeza baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000.

Wengine wamekwenda mbali zaidi kwa kuuhusisha msimamo huo kuwa unaweza kuchochea mtazamo hasi dhidi ya nchi katika uso wa kimataifa.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Kaimu Mwenyekiti wa CUF, Twaha Taslima, alisema watachukua hatua hiyo mapema iwezekanavyo kabla ya kuanza kwa maandalizi ya uchaguzi.

“Tumekubaliana kwamba tutawaandikia barua wagombea wetu ili wamwandikie barua mwenyekiti wa ZEC wamwombe kwamba wanataka kujitoa kwenye uchaguzi hivyo aondoe majina yao kwenye orodha na wasiwekwe kwenye karatasi za kupigia kura,” alisema Taslima.

Alipoulizwa kama uamuzi huo una nguvu kisheria alisema hakuna sheria inayomkataza mtu kujitoa kwenye uchaguzi na kuongeza kwamba wanajitahidi wamwandikie barua hizo mapema iwezekanavyo kabla ya maandalizi ya uchaguzi huo hayajaanza.

“Hakuna sheria inayomzuia mtu kujitoa kwenye uchaguzi kama ameona kwamba hawezi kushiriki, tunajitahidi kufanya suala hili mapema iwezekanavyo kabla ya uchaguzi,” alisema.

Alipoulizwa endapo maombi yao yatakataliwa na majina ya wagombea wao yakabaki kwenye karatasi za kupigia kura na hatimaye wakapigiwa kura na kushinda uchaguzi, alisema hawatakubali nafasi hizo kwasababu walishatangaza kususia uchaguzi huo na kwamba si halali.

“Mtu anaposema amesusia kitu inaeleweka, hata wakiacha majina ya wagombea wetu tukishinda hatutakubali nafasi hizo,” alisema Taslima ambaye kitaaluma ni mwanasheria.

MTAZAMO WA KISOMI

Akizungumza na gazeti hili Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema msimamo huo wa CUF uheshimiwe kwasababu kusudio lake ni kusimamia kile wanachokiamini kuwa ni haki kwao.

Alisema pamoja na heshima hiyo, uamuzi wa chama hicho hauna uhai kisiasa au tija kwa CCM na wananchi wa Zanzibar kwa ujumla kwa sababu una mwelekeo wa kufufua makaburi ya chuki za kisiasa ambazo zilipasua mahusiano ya kijamii baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2000.

“Jambo hili lina mshindo mkali wa kisiasa kama ule uliotokea mwaka 2000-2001, upo uwezekano mkubwa wa mpasuko wa kijamii na hakuna uhai kwa chama hicho au tija kwa CCM na wananchi kwa ujumla japokuwa msimamo wa chama hicho unastahili kuheshimiwa,” alisema Dk. Bana.

Alisema pamoja na kwamba suala hilo limehodhiwa na mvutano wa kisiasa baina ya CUF na CCM, lakini ikumbukwe kuwa vyama vingine vilivyosimamisha wagombea vinayo nafasi ya kupigiwa kura na kupata wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Dk. Bana alisema hoja ya kurudiwa kwa uchaguzi si ya vyama vya siasa pekee lakini hata wananchi wanao haki yao ya kupiga kura kutokana na uhuru wa nafasi zao.

“Msimamo huu wa CUF si wa wananchi, watu wanatakiwa kutofautisha kwa sasa si CCM au CUF pekee ndio wanastahili kupigiwa kura na wananchi….kuna vyama vingine pia vimesimamisha wagombea na wanaweza kupigiwa kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK)  ikaendelea,” alisema Dk. Bana.

Katika hatua nyingine aliongeza kwa kusema kuwa msingi wa mvutano wa kisiasa visiwani humo utaifanya dola kutumia nguvu kubwa kuongoza Serikali itakayochaguliwa katika uchaguzi huo wa marudio.

Mbali na hoja ya Dk. Bana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu), Profesa Gaudence Mpangala, amepongeza msimamo huo wa CUF kwa sababu umefuata kanuni na kuheshimu sheria za nchi.

Alisema uamuzi huo wa CUF unasimamia ukweli wa mambo pamoja na kwamba sheria za nchi zimeshakiukwa.

“Msimamo wangu ni kusema ukweli na tangu mwanzo sikuafiki kufutwa kwa matokeo ya Zanzibar, walichoamua CUF ni msimamo sahihi na wenye mashiko licha ya kwamba unaweza kuweka mtikisiko wa kisiasa visiwani humo kama itatokea,” alisema Profesa Mpangala.

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Mwesiga Baregu, alisema CUF wanastahili kusimamia uamuzi huo kwa sababu wanaamini katika haki ya kikatiba.

Alisema endapo CUF wangekubali kushiriki marudio ya uchaguzi inamaanisha wangekuwa wanatumika kutakatisha sheria iliyokuwa imevunjwa na Mwenyekiti wa ZEC, Jecha.

Alisema uamuzi huo wa CUF ambao unapinga ukiukwaji wa kisheria yanayolazimishwa na dola unaweza kurejesha visiwa vya Zanzibar katika historia ya chuki katika jamii.

“Tuliona uchaguzi wa mwaka 2000-2001 damu ilimwagika kwa mambo kama haya ya kutumia ubabe mbele ya haki za watu, jamii ikapasuka watu wakawa hawana mshikamano wa kijamii na chuki hiyo ilikuwa mbaya sana, binafsi nashindwa kuelewa hivi hawa wenzetu huwa hawajifunzi kila wanapotenda makosa?” alisema Profesa Baregu.

Wiki iliyopita Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi visiwani Zanzibar, Jecha Salum Jecha, alitangaza siku ya kurudiwa uchaguzi kuwa ni Machi 20 mwaka huu na kwamba wagombea watabaki wale wa awali na hakutakuwa na kampeni.

Kutokana na hali hiyo, licha ya CUF kutangaza katika vyombo vya habari kutoshiriki uchaguzi huo, majina yao yanaweza kuendelea kubaki katika karatasi za kupigia kura na wakapigiwa kura.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles