*Watuhumiana kwa wivu wa kisiasa, ushirikina
*Daraja la Kikwete Lawatesa
NA MWANDISHI WETU
WANASIASA wawili maarufu hapa nchini ambao wamekuwa na uhusiano wa kikazi na binafsi, wamefarakana.
Wanasiasa hao, Zitto Kabwe aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini na David Kafulila aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, kila mmoja anamshutumu mwenzake kwa kuwa na jicho la wivu wa kisiasa na kufikia kushambuliana kwa maneno makali kwenye mitandao ya kijamii.
Vita hiyo ya maneno kwenye mitandao ya kijamii imethibitishwa kuwapo na Kafulila ambaye aliliambia MTANZANIA Jumapili kupitia simu yake ya kiganjani kuwa imesababishwa na Zitto anayeugua kile alichokiita maporomoko ya kisiasa.
Kafulila alieleza kuwa alilazimika kupambana na Zitto kupitia kwenye kundi la mtandao wa kijamii wa Whatsapp ambalo linawajumuisha vijana wa Mkoa wa Kigoma linalojulikana kwa jina la Nguruka Yetu.
Katika vita hiyo ya maneno makali ambayo MTANZANIA Jumapili imeyaona, anayeanza kushambulia ni Zitto anayeandika akimtuhumu Kafulila kwa kujitekenya na kucheka mwenyewe.
Andishi hilo linasomeka: “Hivi ndivyo Kafulila anajitekenya mwenyewe na kucheka mwenyewe. Watu mliokuwepo Nguruka leo (Juzi) mthibitishe upuuzi huu. Mimi sitaki kumjibu Kafulila maana sio size yangu. Sikutamka hata jina lake kwenye mkutano.”
Andishi hilo ni mwendelezo wa vita ya maneno ambayo chanzo chake ni nani hasa kati ya Zitto na Kafulila aliyepeleka hoja bungeni ya kujengwa kwa daraja katika Mto Malagarasi.
Zitto anaandika kuahidi kuleta Hansards za Bunge za kuanzia mwaka 2006 hadi 2010 zinazonyesha michango yake bungeni kuhusu ujenzi huo.
Anaendelea kuandika: “Kafulila unajua kuwa hujafanya lolote kuhusu daraja. Unajua hivyo. Onyesha Hansard ya wewe kutetea daraja, ukionyesha najitoa kugombea ubunge, mimi nitakuonyesha Hansards, daraja tumeweka jiwe la msingi hujahudhuria hata bajeti moja ungeteteaje? Huoni aibu mdogo wangu?”
Akijibu mashumbulizi ya Zitto, Kafulila anaandika: “Nilimsikia JK (Jakaya Kikwete) anakusifu kama umemtuma vile.”
Naye Zitto anajibu: “Nimeweka facts (ukweli) ninazoweza kuzitetea popote, David (Kafulila) hajui daraja limekujaje maana hahusiki, hakuwa mbunge. David tumezindua daraja hata bajeti ya kwanza ya Bunge la kwanza bado. Ulitetea lini? Umekuta tumeshamaliza mpango wa daraja. Umedikira tu.”
Kufulila naye anaandika kujibu: “Zitto acha uzinduzi. Maswali yangu ya kwanza bungeni ni daraja. Kwenye mchakato majimboni nilizungumza daraja nikawahakikishia. Tatizo bro (kaka) unaugua wivu.”
Kafulila pia alimlalamikia Zitto kuwa anapenda sifa na kuhoji ni kwanini amekuwa akidanganya watu kuwa hoja ya kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 za Escrow alimpa yeye.
Zitto naye anajibu: “Mimi siwezi kukutukana maana wewe ni mdogo wangu. Wewe niite majina hayo maana mkubwa jalala, lakini ukweli unaujua. Huhusiki na daraja, huhusiki na barabara, kama unahusika mbona umeshindwa barabara ya Uvinza Darajani? Taja barabara moja ambayo wewe David ndani ya Mkoa wa Kigoma umeijengea hoja mpaka ikajengwa. Hakuna hata moja. Acha siasa za ujanja ujanja.”
Kufika hapo, Kafulila anaandika akimtaka Zitto waweke mafanikio ya jimbo katika mtandao huo ili walinganishe.
Kutokana na hilo, Zitto anaandika hivi kujibu: “Kwahiyo David uliuliza maswali bungeni ukapata daraja? Ama kweli. Tufanye ni sawa, umeweka rekodi ya dunia. Miezi mitatu daraja, miaka mitano umeshindwa kujenga lami km 56 tu. Rekodi ya jimboni kwangu ni pamoja na wewe David, wewe ni rekodi yangu mimi, hapo ulipo ni rekodi yangu mimi utake usitake.”
Kafulila naye anaandika kujibu akishangaa: “Unadanganya watu wewe ndiyo ulisababisha wabunge wa NCCR –Mageuzi wakati senti moja hukuchangia? Mnasema Nguruka Hospitali hakuna vitanda na godoro wakati nimeshamaliza?”
Zitto anamjibu Kafulila kwa kuandika: “David mimi siwezi kuja hapa kusema nimekuchangia nini. Mimi sikulelewa hivyo. Wewe binafsi unajua nimekuchangia nini, nafsi yako inajua. David miaka mitano barabara ya km 56 hatua za awali, miezi mitatu daraja na barabara ya Kidahwe Uvinza. Wewe kweli shujaa kaka.
“Nimefanya makubwa moja ni daraja, barabara za Kigoma na wewe mwenyewe ni mafanikio ya jimbo, ni utoto maana wewe mwenyewe ni mafanikio yangu, kufanya vizuri ni fahari yangu maana nimekutengeneza. David umedanganywa, hakuna aliyesema vitanda vya hospitali umelishwa kasa, sisi tuliongelea mambo makubwa. Sina siasa za kijingajinga.”
Baada ya ujumbe huo, Kafulila alimweleza Zitto kuwa wanafanya siasa za matusi kama hawakuwa na malezi, na kwamba inawezekana hafanyi mwenyewe bali anawatuma vijana wake.
Hoja hiyo ilijibiwa na Zitto ambaye alisema hafanyi siasa za matusi kwani si kawaida yake na wala hakuwahi kumfundisha Kafulila siasa hizo kwani anajenga hoja mfano kwa Ngaruka kuwa kijiji.
Zitto anaandika kuwa hawezi kumtuma mtu na kuhoji kama aliwahi kumtuma Kafulila alipokuwa kijana wake.
Kutokana na hilo, Kafulila alimtaka Zitto kufanya siasa za akili na kupunguza chuki za hovyo kwani ni mwanasiasa mkomavu.
Hapo, Zitto anaandika: “Wewe David umechagua kuwa manamba, endelea na umanamba wako, sisi tumeamua kujivua umanamba tuache na chama chetu cha mawese, baada ya Oktoba tutajua. Pia kuna maisha baada ya uchaguzi.”
Kafulila anamjibu Zitto kwa kuandika kuwa itajulikana kwani hana shaka na ushindi, atawashinda CCM na washenga wake.
Zitto naye anaandika akieleza kuwa hana chuki na Kafulila kwa sababu kamtengeza mwenyewe, kumkuza na kumwozesha.
“Acha inferiority complex, unasumbuliwa sana na ukubwa, siwezi kukuchukia mimi kamwe, mtoto akijinyea kiganjani hukati kiganja. Mungu ndiye anajua atashinda nani, ninachojua hakuna wakala wa manamba atashinda Mkoa wa Kigoma. Hakuna hata mmoja,” anaandika Zitto.
Kwa mwendelezo huo huo wa kushambuliana, Kafulila naye anajibu mapigo kwa kuandika: “Mimi nawaambia nilishinda 2010 kwa nguvu yangu na itakuwa hivyo 2015, una chuki mbaya, tena ya kutoa roho mtu.
“Kijana unapokuwa na chuki za kichawi ni mbaya sana maisha haya, nina uwezo wa kusimama mwenyewe.”
Zitto anaandika kujibu: “Ulishinda 2010 kwa nguvu yako, wewe ni supastaa na utashinda tena, kwa nguvu yako zimebaki siku 29 tusiandike mate na wino upo, unajisema mwenyewe.”
Hapo Kafulila anaandika kujibu: “Unapasuka kwa hasira tu, lakini nakuhakikishia sina shaka na ushindi, Nguruka ni chuo cha siasa, hawapangwi na wala hawajawahi kupangwa.”
Zitto naye anajibu: “Kigoma Mjini mimi sitambi kushinda, mimi ni mwanadamu tu kiumbe dhaifu, mola ndiye anajua ninashinda au la. Siwezi kujipa u-Mungu kama wewe, Mungu akipenda nitashinda, asipopenda nitafanya mengine.”
Hapo Kafulila anaandika maneno makali zaidi: “Unafiki mtupu, unasema asiyekufuata ACT hawi Mbunge Kigoma kama Mungu.”
Jitihada za kumpata Zitto kuzungumzia hali hiyo ya kuchafuka kwa uhusiano wake na Kafulila hazikuweza kufanikiwa hadi tunakwenda mitambani.
Tumerudia habari hii kuichapa tena kutokana na makosa ya kiufindi yaliyotokea katika toleo la jana la gazeti hili. Tunawaomba radhi wasomaji wetu wote kwa usumbufu uliojitokeza. Mhariri