Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM
KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, anasakwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kutoa lugha za uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli kwenye mkutano wa kampeni mjini Kahama.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Naibu Katibu Mkuu Bara wa ACT-Wazalendo, Msafiri Mtemelwa, ilieleza kuwa juzi Polisi wilayani Kahama wakiwa na magari saba kati yao manne ni ya Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakiwa na mabomu ya machozi walivamia mkutano wa kampeni Kata ya Isagehe, wakati Zitto akihutubia jukwaani.
Alisema baada ya kushuka jukwaani Zitto alipeana mikono na wananchi na baadaye alipotea katika eneo hilo.
“Jana (juzi) polisi waliingia mkutanoni na kuanza kumtafuta kiongozi wa chama (Zitto), lakini hawakuweza kumpata na kumkamata dereva wa gari alilokuwa anatumia Patrick Muhidin pamoja na katibu wa jimbo la Kahama Vincent Ikerenge.
“Wote walipelekwa kituo cha Polisi Kahama na kuandikishwa maelezo. Gari hiyo Land Cruiser V8 imeshikiliwa na polisi mpaka sasa.
“…hata hivyo tunawajulisha wanachama na Watanzania wote kuwa Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe, hajakamatwa na yupo salama,” alisema Mtemelwa.
Alisema ilipofika saa mbili usiku wa juzi polisi walivamia makao makuu ya kampeni ya chama hicho na kufanya upekuzi mkubwa wakimtafuta Kiongozi wa Chama hicho bila mafanikio.
“Baadaye waliweka mazuio ya njia zote za kutoka Kahama wakiamini kuwa Kiongozi wa Chama (Zitto) atakuwa anapanga kutoroka na kutoka nje ya Kahama.
“Tunapenda kuwajulisha yupo salama na yupo Kahama anasimamia ushindi wa kura. Amewaeleza viongozi wa chama kuwa polisi wataweza kumkamata iwapo yeye atataka kukamatwa na sio kwa kuvamiwa bali kwa kuitwa rasmi polisi na kuelezwa makosa aliyoyafanya.
“Chama kimefuatilia kujua ni kwanini polisi wanamtafuta. Tumejulishwa na polisi kwamba ana mashtaka ya kutoa lugha ya uchochezi katika hotuba zake za kampeni katika Kata ya Isagehe Kahama Mjini. Polisi wanasema kiongozi wa chama amemchonganisha Rais na wananchi,” alisema.