Bethsheba Wambura, Dar es Salaam
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amehojiwa na Jeshi la Polisi leo Jumatano Oktoba 31, akidaiwa kutoa matamshi ya uchochezi juu ya mauaji ya Polisi na raia yaliripotiwa wilayani Uvinza mkoani Kigoma.
Katika mkuta
no wake na waandishi wa habari aliouitisha mwishoni mwa wiki iliyopita Jumapili Oktoba 28 mwaka huu Zitto alisema katika kijiji cha Mpeta wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma yalitokea mauaji y askari wa Jeshi la Polisi ambapo Mkuu wa Kituo cha Polisi Nguruka aliuwawa na baadae yakazuka mapigano kati ya askari na wananchi na wananchi wa kabila la Wanyatunzu zaidi ya 100 waliuwawa.
Akithibitisha kushikiliwa kiongozi wao Katibu wa Itikadi, Mawasiliano ya Umma na Uenezi wa chama hicho, Ado Shaibu amesema leo walikwenda askari polisi nyumbani kwa Zitto maeneo ya Masaki na kumwambia anahitajika katika kituo cha polisi Oysterbay kwa mahojiano alikohojiwa kwa saa Nne kabla ya kuhamishiwa katika kituo cha Kati.
Shaibu amesema Kabwe alihojiwa kuhusu hali ya usalama nchini kiujumla na zaidi matamshi yake yaliyolitaka jeshi la polisi nchini kutoa idadi sahihi ya wananchi waliokufa kule Mpeta huku akimtaka IGP Simon Sirro kutembelea eneo yalipotokea mauaji hayo.
“Sisi kama ACT bado tunashikilia msimamo wetu na hatukubaliani na taarifa zilizotolewa na Jeshi la Polisi kuwa watu waliokufa si zaidi ya wawili,” amesema Shaibu.
Aidha mapema leo hii Kamanda wa Polisi Kinondoni kamanda Jumanne Muliro alithibitisha jeshi hilo kumshikilia Zitto kwa mahojiano maalumu hasa wakitaka awapatie taarifa alizonazo juu ya kilichotokea Mpeta.