SIKU Chache baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba kudai Umoja wa Katiba ya Wanchi (Ukawa), umeteua mgombea kutoka CCM, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ameibuka na kutoa madai yanayoshabihiana na hayo.
Akizungumza na kituo cha televisheni cha Azam, Profesa Lipumba alipoulizwa endapo kujiuzulu kwake ni njama za kuihujumu Ukawa alisema. “Ukweli wa hili tumejiparaganisha wenyewe, sasa katika nafasi ya mgombea urais, tuna mgombea wa CCM ambaye anagombea CCM na ukawa kuna mgombea urais anayegombea kutoka CCM.
“Kuna wana CCM wawili wanaogombea urais, wakati sisi tulikuwa na viongozi kama mimi mwenyewe, Dk Slaa (Wilbrod Slaa, Katibu Mkuu wa Chadema) aliyetaka kugombea kupitia Ukawa, badala yake tumeweka mtu wa CCM ambaya amegombea urais kwa tiketi ya Ukawa,” alisema.
Wakati mjadala wa Profesa Lipumba kujiuzulu na kutoa sababu hizo licha ya kuwa alishiriki hatua zote za kumpokea waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ukiendelea, Zitto naye ameibuka na kusema kuwa chama chake kilikataa kuingia katika upepo wa Ukawa.
Wakati Zitto akiyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara mjini Iringa, mara kadhaa amekuwa akilalamika kupitia vyombo vya habari na mitandao kwamba, alitaka kujiunga na umoja huo lakini amekataliwa.
Zitto anayedaiwa kumtumia Profesa Lipumba amuingize kwenye umoja huo, alisema baadhi ya vyama vilipokea barua yake ya kutaka kujiunga na Ukawa, lakini Chadema walikataa hata kuipokea.
Akizungumza mkoani Iringa, Zitto alisema. “ndiyo maana sisi tumekataa kuingia kwenye upepo (Ukawa), Watanzania tunahitaji refa, CCM itaanguka, lakini ikianguka itaparanganyika, CCM ikiparanganyika watawala wapya wataifisadi hii nchi, lazima kuwe na chama cha kuwasimamia wananchi wanyonge.
Miaka minane iliyopita tumekuwa tukipambana na ufisadi wa CCM, tunasema viongozi wetu wa kisiasa, wanasema Lowassa ni fisadi, leo wanasema ufisadi ni mfumo si mtu, ufisafdi ni mfumo na watu wanaouendesha.
Kwetu sisi ACT Wazalendo, vyama vikubwa ambavyo vimeteuwa wagombea ni wale wale, chama kimoja ndo kimeasisi ufisad kwenye nchi, ndiyo kinaongoza ufisadi kwenye nchi, chama kingine kinaongozwa na fisadi mkuu,” alisema.
Tangu Profesa Lipumba kujiuzulu na kutoweka nchini, kumekuwa na maelezo mengi ikiwa ni pamoja na usahihi wa madai yake ili hali yeye ni mmoja ya watu waliojitokeza hadharani na kumkaribisha Lowassa Ukawa.