28.7 C
Dar es Salaam
Friday, May 24, 2024

Contact us: [email protected]

Marando: Nitatangaza matokeo kabla ya NEC

marandoNA MWANDISHI WETU

MWANASHERIA wa Chadema, Mabere Marando, ameahidi kutangaza matokeo ya uchaguzi kila kituo kitakapomaliza upigaji wa kura kabla ya kutangazwa na Tume ya Uchaguzi (NEC).

Marando alitoa kauli hiyo alipotakiwa na Lowassa kulitolea ufafanuzi wa kisheria zoezi la kukusanya shahada za kura za polisi na wanajeshi, linalodaiwa kufanywa na viongozi wao.

Alisema njama zote zinazotumiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM)  za kutaka kuhujumu  matokeo, zikiwamo za kukusanya shahada za polisi na wanajeshi wameshazigundua na wamejipanga kuzikabili.

“Njama zote walizonazo kutaka kujaribu kuhujumu kura za Lowassa, wabunge na madiwani pamoja na za kuhujumu kura za Zanzibar tutazidhibiti, nawaambia mawakala baada ya kupiga kura tu msisubiri saa 12, nitumieni  saa saba mchana nitatangaza matokeo, mheshimiwa usiwe na wasiwasi, endelea na kazi yako,” alisema Marando.

Alisema  ofisi ya sheria ya chama hicho imejipanga kulinda kura za wagombea wote na hakuna atakayeibiwa mwaka huu.

 

WAFUASI WAHAMIA BIAFRA

Uongozi wa Chadema jana ulilazimika  kutumia viwanja viwili tofauti ili kuweza kutii kiu ya wafuasi na wapenzi wa vyama vinavyounda Ukawa kumpokea Lowassa.

Hali hiyo ilitokea baada ya eneo lililoandaliwa awali la  makao makuu ya chama yaliyopo Mtaa wa Ufipa, Kinondoni kushindwa kukidhi  idadi ya umati mkubwa wa wananchi waliojitokeza.

Mamia ya watu hao walianza kufika katika ofisi za Chadema saa nne asubuhi kwa ajili ya kumpokea na kumsikiliza Lowassa ambaye awali ilitangazwa kuwa angewahutubia wanachama katika eneo hilo.

Saa 9:45 alasiri, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salim Mwalimu, aliutangazia umati uliojazana katika ofisi hizo kwamba watulie kwa kuwa Lowassa amelazimika kupitia katika viwanja vya Biafra kuwashukuru wananchi kabla ya kufika katika eneo hilo maalumu aliloandaliwa.

“Jamani samahani ndugu wananchi naombeni kila mtu alipo atulie  kwakuwa watu waliopo hapa ni wengi na wanaotoka Posta ni mara tatu ya mliopo hapa, kwakuwa eneo letu ni dogo, tumeomba Mheshimiwa Lowassa  na baadhi ya viongozi waende moja kwa moja katika viwanja vya Biafra kwa ajili ya kuwahutubia wananchi waliotoka naye kuchukua fomu kwa sababu wote wakija hapa eneo hili haliwezi kutosha,” alisema Mwalimu.

Alisema baada ya Lowassa kumaliza kuhutubia katika viwanja vya Biafra ratiba iliyopangwa katika ofisi za makao makuu itaendelea kama zilivyopangwa.

AHUTUBIA BIAFRA

Hata hivyo baada ya kuhutubia wananchi katika viwanja vya Biafra, Mwalimu alitumia mbinu nyingine ya kuwatawanya wafuasi hao kwamba wasimsindikize tena Lowassa kwakuwa alikuwa anakwenda katika Ofisi za television ya Azam kufanya mahojiano akiwa na lengo la kupunguza msongamano ambao ungeendelea eneo la makao makuu ya Chadema.

 

 MGOMBEA MWENZA

Akihutubia wananchi nje ya ofisi za Chadema, mgombea mwenza wa Lowassa, Juma Duni Haji,  alisema hawaendi Ikulu kutafuta utajiri wala kufanya falsafa ya udini, bali wamepAnga kuwakomboa Watanzania ambao kwa sasa wanaonekana kuwa na njaa.

“Sijaona njaa ya kikristo wala ya Kiislamu,  kuna njaa ya mwanadamu na haki za binadamu, wanashindwa kutafuta hoja wanatumia za udini.

“Hatuendi Ikulu kujenga makanisa wala misikiti, tunaenda kuondoa umasikini,  hakuna asiyependa shibe, amani itaendelea kuwepo na kama mtashiba, watoto watakwenda shule, wakinamama wataachwa kudhalilishwa,  hayo ndiyo maisha tunayoyataka, kwa mara ya kwanza tumepanda gari moja, nimemwambia Lowassa umma una matumaini na wewe.

“JK alituambia anakuja na ari mpya na kasi mpya, kumbe amekuja na njaa mpya na rushwa mpya, sisi hatuendi Ikulu kutafuta utajiri,” alisema Duni.

 

MBOWE AUGUA GHAFLA

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, jana alizidiwa ghafla  wakati msafara ulipofika eneo la Kinondoni  Makaburini ambapo alilazimika kukatisha msafara na kuelekea Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni ili kupatiwa matibabu ya awali.

Akiwa ndani ya gari lake, Mbowe alionekana akikaa chini na badaye mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu alimvua  kofia aliyokuwa amevaa  huku dereva akifunga madirisha ya gari hilo na sehemu  ya wazi kwa juu ambayo alikuwa akiitumia kiongozi huyo kwa kuwapungia mikono wananchi akiwa katika msafara.

Msafara ulipofika eneo la Kinondoni Manyanya gari la Mbowe lililazimika kukatisha safari hiyo na kuelekea TMJ.

Baadaye kiongozi mmoja wa Chadema ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa sababu si msemaji, alisema Mbowe alipatiwa matibabu na kuruhusiwa kwenda nyumbani kwa ajili ya kupumzika.

“Ameshatolewa hospitali tayari yupo nyumbani, najua ni presha ndiyo ilikuwa imemsumbua, suala la kujua kama ni ya kupanda ama kushuka ni la madaktari,” alisema kiongozi huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles