29.9 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Zitto akemea siasa za chuki

Waandishi Wetu – dar es salaam

KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema wanasiasa wanaofanya kampeni za chuki miongoni mwa wanachama ndani ya chama chake, hasa zinazonuia kuwagawa kwa misingi ya dini, upande wa muungano, jinsia na kabila hawastahili kuvumiliwa kwa sasa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Halmashauri Kuu ya chama hicho Dar es Salaam jana, Zitto alisema kipindi hiki ambacho chama hicho kinaingia katika uchaguzi wa ndani na kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, wanasiasa wa aina hiyo hawatakiwi kuvumiliwa.

“Usalama wa chama lazima uzingatiwe, mgombea yeyote atakayefanya kampeni zinazojenga chuki miongoni mwa wanachama, zinazokigawa chama kwa maeneo, dini, upande wa muungano, jinsia, kabila hafai kuwa kiongozi wa chama chetu.

“Kama kuna mgombea ambaye anafanya haya niliyoyataja dhamira yake imsute, huwezi kufanya kampeni kwa kuwagawa wanachama halafu utegemee kuongoza chama kwa kuwaunganisha wanachama. Ukifanya kampeni kwa ubaguzi, utaongoza kwa kubagua,” alisema Zitto.

Alisema wakati huu mbapo chama hicho kinajiandaa kufanya uchaguzi wa ndani wa viongozi wa kitaifa, wanahitaji watu wanaojenga umoja zaidi miongoni mwa wanachama kwa manufaa ya chama hicho na manufaa ya taifa, hivyo wanahitaji kuongozwa na kaulimbiu ya ‘tuchague mmoja tubaki wamoja’.

Kuhusu Uchaguzi Mkuu, Zitto alisema chama chake kinahitaji kuendelea na kampeni ya tume huru ya uchaguzi ambayo ni lazima kwa sasa.

Alisema walipokutana mara ya mwisho walikuwa wanajiandaa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa na wote ni mashuhuda wa namna mchakato wa uchaguzi ule ulivyoporwa na wananchi kupokwa haki yao ya kuchagua viongozi wao.

Zitto alitoa ushauri kwa Halmashauri Kuu ya chama iazimie kuwataka wanachama kote nchini kuongeza juhudi katika kampeni ya kudai tume huru ya uchaguzi kwa kuwa bila hiyo, itakuwa ni vigumu kuhami demokrasia na kwamba viongozi wataendelea kutumia kila jukwaa litakalokuwapo kupigania uchaguzi wa huru, haki na unaoaminika.

Alisema ni vyema pia viongozi wa mikoa watumie majukwaa huko mikoani na majimboni na kuendeleza kampeni hiyo ya kudai tume huru ya uchaguzi.

Kuhusu katiba ya chama chao, aliwasihi wajumbe wawe makini kuhakikisha inazingatia kujenga taswira ya chama kinachozingatia uwiano wa kijinsia na uongozi wenye sura ya kitaifa.

Alisema katika mazingira ya sasa ya siasa ya dunia huwezi kumweka pembeni mwanamke, hivyo ni muhimu katiba yao kuweka mazingatio ya uwiano wa kijinsia katika uongozi wa ngazi zote za chama.

Zitto alisema mkutano huo pia utafanya uteuzi wa wagombea wa nafasi za juu za uongozi wa chama, hivyo wabunge wanatakiwa kuongozwa na misingi ya haki na demokrasia, suala ambalo ni muhimu ndani ya chama hicho, katika kutekeleza utamaduni wa kushindana kwa misingi ya kidemokrasia.

Makamu Mwenyekiti ACT Wazalendo, Shabani Mambo alisema chama hicho kinajali na kuamini misingi ya demokrasia na kina wajibu kutoa nafasi kwa wanachama wengine wanaotaka kugombea nafasi yoyote ndani ya chama hicho.

Imeandikwa na GODFREY SHAURI, BATROMAYO JAMES (DSJ) NA ANDREW MSECHU

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles