30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa: Tumechukua tahadhari ya corona

Amina Omari -Mkinga

SERIKALI imesema itahakikisha inaweka tahadhari zote za kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa corona katika maeneo ya mipakani, ikiwamo kuweka mashine za kubaini wagonjwa na  kuwapima wageni wote wanaotoka nje ya nchi.

Hayo yalisemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana, wakati akikagua kituo cha forodha cha Horohoro, Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga.

Alisema tayari zaidi ya nchi 50 duniani zimeshaathiriwa na ugonjwa huo, hivyo Serikali ina jukumu la kuhakikisha tahadhari inachukuliwa ili kujilinda.

Aliwataka watumishi wa mpaka wa Horohoro kuhakikisha wanawapima wageni wote wanaopita na kuwachukulia hatua za haraka watakaobainika wameathirika.

Majaliwa aliwataka pia Watanzania kuwa walinzi wa mipaka ili kuwadhibiti wahamiaji haramu wanaoingia katika njia zisiso rasmi.

“Nawaomba ndugu zangu wananchi wa Mkinga hakikisheni mnawabaini wahamiaji haramu wote pamoja na watu wanaohusika na kuwapitisha ili kuwadhibiti mapema.

“Bado tuna wahamiaji haramu wanaoingia kinyume cha taratibu, wiki iliyopita wamekamatwa 41 Dodoma wakitokea Horohoro. Watanzania wasiingie kwenye biashara ya kuwasafirisha wahamiaji hao,” alisema Majaliwa.

Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Yona Maki alisema kutokana na oparesheni mbalimbali, wameweza kudhibiti wahamiaji haramu jamii ya Wasomali na Waethiopia wanaoingia 131 hadi 103.

Alisema kuna wahamiaji walowezi 12,000 ambao bado wanasubiri utaratibu maalumu wa kutambuliwa.

Alimwomba Waziri Mkuu kuwasaidia uhakika wa mipaka hususani katika eneo la bahari kwa kuwekewa maboya.

“Mipango yetu ni kupanda miti katika eneo la mpaka la nchi kavu na kule kwenye bahari tuwekewe maboya ili kuweza kuulinda mpaka wetu,” alisema Maki.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amekasirishwa na vitendo vya baadhi ya majengo ya forodha ambayo hayana viwango, huku akitoa wiki moja kwa msimamizi wa jengo la Horohoro kuwasilisha taarifa za kina kuhusu jengo hilo.

“Nakutaka Meneja Estate pamoja na Mkandarasi wa jengo ifikapo tarehe 11 Mwezi huu muwepo Dodoma na taarifa kamili kuhusu jengo hili,” alisema Majaliwa.

Naye Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema  tayari wamefunga mashine katika kituo hicho ili kubaini wagonjwa wa corona.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles