26.7 C
Dar es Salaam
Saturday, February 24, 2024

Contact us: [email protected]

ZITTO AIRARUA SERIKALI SAKATA LA BOMBARDIER

Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM

MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), ameonya na kusema kuwa suala la ndege ya Tanzania aina ya Bombardier kuzuiwa nchini Canada lisifanywe ni suala la ushabiki kama ushabiki wa mpira.

Amesema suala hilo ni la nchi na mjadala wake ni lazima uwe na hadhi hiyo na kueleza kuwa kitendo cha Kaimu Msemaji wa Serikali, Zamaradi Kawawa, kulaumu wanasiasa kwa jambo la kisheria kama hili ni utoto.

Zitto aliyasema hayo kupitia taarifa yake aliyoitoa jana ambapo alisema kuwa historia inaonesha hakuna mwanasiasa hasa wa upinzani anayeweza kushirikiana na kampuni za kigeni kuhujumu nchi.

“Falsafa ya chama ninachokiongoza, ACT Wazalendo, ni ‘Taifa Kwanza, Leo na Kesho’. Mimi binafsi filosofia yangu ni rahisi sana ‘My Country First, Right or Wrong’ (Nchi Yangu Kwanza, Kwa Usahihi au Kwa Makosa). Maneno yanayosambazwa kuwa nimeshiriki kuwezesha ndege ya Bombardier iliyonunuliwa na Serikali kwa niaba ya ATCL kukamatwa huko Canada ni takataka tu zinazosambazwa na wapika propaganda. Ni upuuzi!

“Serikali lazima ifahamu kuwa ni lazima ihojiwe, na iwe tayari kutoa majibu. Sisi kama vyama vilivyo nje ya Serikali ni wajibu wetu kuhoji jambo lolote. Pia ni haki yetu kupata Taarifa zozote kutoka mahala popote zitakazosaidia kuisimamia Serikali.

“Wajibu wa Serikali ni kujibu hoja zinazoibuliwa nasi, majibu ya Msemaji wa Serikali yanataka kuligeuza suala hili kuwa la kisiasa na watu wameangukia kwenye ushabiki huo,” alisema Zitto.

Kutokana na hali hiyo Zitto alisema kuwa ni vema Watanzania kutokubali kuingia kwenye ushabiki kwani suala hilo ni la kisheria na la nchi ambapo wananchi wote wana masilahi ya kuona inakwenda mbele.

“Nchi yetu kudaiwa si dhambi. Hata mataifa makubwa duniani yanadaiwa. Watu binafsi tunadaiwa sembuse Serikali? Mimi binafsi ninadaiwa madeni ya uchaguzi mpaka sasa na wengine wamenipeleka mahakamani. Si dhambi kudaiwa.

“Muhimu ni (1) Je deni limetokana na nini? Ni maamuzi mabovu ya kisiasa? (2) Unalipa deni hilo au kuweka mikakati ya kulipa?

“Serikali yetu inafahamu kuwa nchi yetu ina madeni mengi, na miongoni mwa madeni hayo yapo ambayo yameshaamuliwa na Mahakama. Kinachopaswa ni kuwa na maarifa ya kupita ili kuzuia Mali zetu nje ya nchi kuzuiwa kama ilivyo kwa ndege hii,” alisema.

Alisema Serikali ni vema iwe wazi kuhusu suala hiloi la ndege. “Je ile ya Boeing (Terrible Teen) ipo salama? Madeni mengine yenye amri ya mahakama ni yepi? Kwanini Serikali inasubiri kuhojiwa ndipo itoe taarifa?,” alihoji.

Alisema Tanzania ni mali ya Watanzania wote na hakuna mwenye hati miliki ya ukweli. “Hakuna mwenye hatimiliki ya ukweli. Ukweli pia haupendi kupindwapindwa.

“Serikali itoke kueleza nini kimetokea mpaka ndege kuzuiwa, iachane na tabia ya ovyo ya kutafuta mchawi ‘kwamba eti wanasiasa ndio wamesababisha’. Kutafuta mchawi ni kutowajibika kwa maamuzi ya Serikali yenyewe,” alisema.

Sakata la kuzuiwa kwa ndege ya Bombardier limeibua mjadala mkali baada ya kuibuliwa na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu mwishino na mwa wiki na kujibiwa na Serikali kupitia Kaimu Msemaji, Zamaradi Kawawa ambapo alishutumu suala hilo linahujumiwa na wanasiasa wasiokuwa wazalendo.

Mwisho

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles