28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, February 22, 2024

Contact us: [email protected]

KIONGOZI MBIO ZA MWENGE AWAKOROMEA DC, DED

Na BENJAMIN MASESE

-MWANZA

KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Amour Hamad Amour, jana aligeuka  ‘mbogo’  na kutoa lawama kwa viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, kumpeleka katika mradi wa maji ambao haujakamilika.

Alisema mradi huo hauna ubora, ufanisi  na haujawashirikisha walengwa.

Kitendo hicho kilimfanya kiongozi huyo wa mwenge kuwahoji viongozi wa jiji hilo akiwamo Mkurugenzi wake, Kiomoni Kibamba, Mhandisi wa Maji, Zubeda Saidi, Mkandarasi wa Mradi, Richard Kerenge, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mary Tesha na Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula ambao kila mmoja  alitoa maelezo ambayo hata hivyo hayakumridhisha Amour.

Wakati viongozi hao wakitoa maelezo kwa kiongozi huyo wa Mwenge, wananchi walipaza sauti zao wakidai mradi huo ni feki na kumtaka asiuzindue kutokana na maji kutowafikia wakazi wengi wa vijiji vya Fumagila na Bukaga.

Hali hiyo ilimfanya Amour  ambaye alikuwa anaelekezwa na DC Tesha  sehemu iliyoandaliwa kwa ajili ya uzinduzi ambapo alisita na kuanza kukagua maeneo yote ya tanki pamoja na mashine ya kusukuma maji kwenda Fumagila.

Hata hivyo kiongozi huyo wa mwenge  alishtushwa na maji hayo ambayo yalionekana kuwa machafu hivyo aliagiza kufanyike mpango wa kuyatibu yanapofika katika matanki husika.

Hata hivyo kelele za wananchi kumtaka kiongozi huyo asizindue mradi huo zilimfanya kutoa nafasi kwa baadhi ya wananchi  ili asikie kero yao.

Baadhi ya wananchi walieleza kuwa hawajawahi kupata maji katika maeneo yao huku wenzako wakiitikia kwa shangwe.

Maelezo ya wananchi hao yaliwafanya viongozi wa jiji kuinamisha vichwa chini huku wakimwomba Amour kutembelea vituo vya maji Fumagila ambapo kiongozi huyo alisema hawezi kwenda huko wakati wananchi wamesema ukweli mbele yao.

Kutokana na hali hiyo, Amour alisema amekitishwa na maelezo ya mradi huo ambao unapingwa wazi wazi na wananchi hivyo haukuwa shirikishi, hivyo atauzindua baada ya siku 10.

“Sheria zimekengeuka katika mradi, hata  mwanasheria wa jiji amekiri, hivyo  naomba sheria zifuatwe na jumuiya iundwe ya wananchi  ya kusimamia mradi huu, tatu nataka mapungufu yote ya mabomba kupasuka na mengine yashughulikiwe na mradi ukamilike, ikifika Septemba Mosi nipate taarifa kwamba maji yanapatikana muda wote,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles