26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Zitto ahoji ziliko Sh tril. 2.1 nyingine

Na FREDY AZZAH -DODOMA

MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), amesema Sh trilioni 2.1 zilizooneshwa katika taarifa ya fedha iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango hazionekani.

Zitto ameibua suala hilo ikiwa sakata la Sh trilioni 1.5 aliloliibua kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Aprili 15, mwaka huu likiwa bado linashughulikiwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na CAG mwenyewe.

Akichangia mapendekezo ya mpango wa taifa wa maendeleo kwa mwaka 2019/2020, Zitto alisema kuna tatizo la uhasibu.

“Tuna tatizo la ‘accounting’ (uhasibu), nitaliandika vizuri kwenye mchango wa maandishi, ukitazama taarifa ya Serikali ya sasa hivi tunarudi kwenye lile tatizo la Sh trilioni 1.5. Ukitazama kwenye ripoti ambayo Serikali imeitoa fedha hizo kwenda kwenye mafungo kuna tofauti ya Sh trilioni 2.1.

“Na mbaya zaidi, mwenyekiti ukitazama taarifa ya mwaka 2017, hotuba ya waziri ya mwaka 2017 kama ingekuwa imezingatiwa na hazina, tatizo tunalozungumza sasa ambalo PAC wanalifanyia kazi la Sh trilioni 1.5 lisingekuwepo.

“Kwa sababu waliripoti vile walivyokusanya na vile walivyotoa, mkatazame ukurasa wa 11 na 12, CAG baadaye akaja kuonyesha kwamba kilichoripotiwa kuna hiyo tofauti ya Sh trilioni 1.5. Sasa hivi 2018 tatizo limejirudia.

“Mimi sitaki kusema kuna wizi, najua Dk. Mpango siyo mwizi na sisi watu wa Kigoma hatuna historia ya wizi, lakini kuna tatizo kubwa la ‘accounting’,” alisema Zitto.

Baada ya muda wake wa kuchangia kwisha, Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema Dk. Mpango anatakiwa kutoa taarifa ya Sh trilioni 1.5 mara mbili.

Aprili 15, mwaka huu, Zitto alisema CAG ameonesha kuwa kati ya bajeti ya Sh trilioni 29.5 zilizoidhinishwa na Bunge, Serikali iliweza kukusanya Sh trilioni 25.3 tu kutoka vyanzo vyote vya kodi, vyanzo visivyo vya kodi, mikopo ya ndani na nje na misaada ya wahisani na washirika wa maendeleo.

Pia alisema Serikali ilishindwa kukusanya Sh trilioni 4.2, sawa na asilimia 15 ya bajeti yote ya mwaka 2016/17.

“Katika fedha zote zilizokusanywa Sh trilioni 25.3, ni Sh trilioni 23.8 tu ndizo zilitolewa kwa ajili ya mishahara ya watumishi, matumizi mengine, matumizi ya maendeleo na kulipa madeni yatokanayo na amana za Serikali na riba.

“Lakini Sh trilioni 1.5 hazijulikani zimekwenda wapi na hizo ni asilimia sita ya fedha zote zilizokusanywa mwaka huo na ripoti hiyo inaonyesha pia kwamba Serikali ilitumia Sh bilioni 219 kulipa madeni ya nyuma.

“Matumizi hayo hayakuwa sehemu ya bajeti iliyoletwa na Serikali na kuidhinishwa na Bunge. Hivyo madeni hayo ni hewa na ulipwaji wake ni matumizi nje ya bajeti iliyopitishwa na Bunge,” alisema Zitto.

Aprili 20, mwaka huu, Serikali ilijibu tuhuma hizo ikisema Sh bilioni 697.9 zilitumika kulipa hati fungani, Sh bilioni 689.3 mapato tarajiwa na Sh bilioni 203.9 ni mapato yaliyokusanywa kwa niaba ya Zanzibar.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, akisoma kauli ya Serikali bungeni, alisema taarifa ya CAG inaonesha mapato yote ya Serikali ya mwaka 2016/17 yalikuwa Sh trilioni 25.3, fedha zilizojumuisha mapato ya kodi, yasiyo ya kodi, mikopo ya ndani na nje, misaada na mikopo yenye masharti nafuu.

“Kuanzia mwaka 2016/2017, TRA ilianza rasmi kuyatambua mapato kwa mfumo wa ‘accrual’, hivyo kati ya mapato haya ya shilingi trilioni 25.3, yalikuwepo pia mapato tarajiwa kama mapato ya kodi ya shilingi bilioni 687.3 pamoja na mapato ya kodi yaliyokusanywa kwa niaba ya Serikali ya Zanzibar ya shilingi bilioni 203.92,” alisema Dk. Kijaji.

Alisema katika uandishi wa taarifa yake, CAG alitumia taarifa za hesabu na nyaraka mbalimbali ikiwa ni pamoja na taarifa za utekelezaji wa bajeti ambapo hadi Juni 2017, mapato yaliyokusanywa yalikuwa Sh trilioni 25.3 na matumizi Sh trilioni 23.79.

“Matumizi haya hayakujumuisha Sh bilioni 697.85 zilizotumika kulipa dhamana na hati fungani za Serikali zilizoiva, matumizi haya yalikuwa hayajafanyiwa uhamisho wakati ukaguzi unakamilika.

“Hivyo basi, baada ya kufanya uhamisho jumla ya matumizi yote kwa kutumia ridhaa za matumizi yalikuwa Sh trilioni 24.4,” alisema Dk. Kijaji.

Akifafanua zaidi taarifa yake, Dk. Kijaji alisema mwaka 2012/2013 hadi mwaka 2016/2017, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango ilikuwa kwenye kipindi cha mpito cha miaka mitano ya utekelezaji wa mpango mkakati wa kuandaa hesabu za Serikali kwa kutumia mfumo wa viwango vya kimataifa vya uhasibu katika sekta ya umma.

“Katika kipindi hicho, Serikali iliendelea kukusanya taarifa mbalimbali kwa kutumia mfumo huu ili kutuwezesha kutambua kikamilifu hesabu za mali, madeni na mapato yatokanayo na kodi.

“Matokeo ya utekelezaji wa mfumo huo umeiwezesha Serikali na taasisi zake kutoa taarifa za kina na zinazoonyesha uwazi na uwajibikaji wa taasisi husika, hususani katika usimamizi wa mali na madeni ya taasisi.

“Kutokana na mfumo huo, napenda kuliarifu Bunge lako kuwa hakuna fedha taslimu ya Sh trilioni 1.51 iliyopotea au kutumika kwenye matumizi ambayo hayakuidhinishwa na Bunge.

“Hivyo basi, madai ya baadhi ya watu wasiolitakia mema taifa letu na Serikali yetu, hayana msingi wowote wenye mantiki,” alisema Dk. Kijaji.

Licha ya maelezo hayo ya Serikali, suala hilo limeendelea kuibuka mara kwa mara hali iliyofanya PAC kumtaka CAG kufanya uchunguzi mwingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles