26.1 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

ZIARA YA MAGUFULI GUMZO

Na AGATHA CHARLES

RAIS Dk. John Magufuli, amefanya ziara ya kushtukiza kwa kuvuka na kivuko kutoka Magogoni kwenda Kigamboni, Dar es Salaam jana ambako alizungumza na wananchi.

Katika ziara hiyo, Rais Magufuli pia alitembelea Chuo cha Kumbukumbu ya Mwl. Nyerere pamoja na Daraja la Nyerere.

Picha zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilimwonesha Rais akiwa amejumuika na wananchi waliokuwa wakisubiria usafiri huo ndani ya jengo la abiria wanaosubiri kivuko kuja upande wa pili na kupanda nao kwenda upande huo wa Kigamboni.

Katika jengo hilo, Rais alikaa katikati ya kundi la vijana ambao nao walikuwa katika viti hivyo vya kawaida vinavyotumiwa kusubiria usafiri huo wa kivuko.

Akiwa ndani ya jengo hilo, Rais alionekana kusalimiana na abiria na picha nyingine alionekana ‘akigonga tano’ na mmoja wa abiria hao aliokuwa amejichanganya nao katika viti hivyo.

 

Katika ziara hiyo, Rais akiwa ameambatana na walinzi wake, alipanda kivuko cha MV Kigamboni huku akiacha gumzo kwa wananchi hao ambao aliambatana nao.

Akiwa ndani ya kivuko hicho, Rais aliwahoji wananchi hao kuwa walikuwa wakisemaje ambako sauti zilizikika zikimshangilia na mwingine kusema hana mpinzani.

Magufuli: Mlikuwa mnasemaje?

Jibu: Huna mpinzani baba, huna.

Magufuli: Hapana mimi nawapongeza ninyi.. haya jamani asanteni sana (huku akipunga mkono)

Jibu: Watanyooka tu (huku kukiwa na kelele).

Baada ya kivuko hicho kufika ng’ambo, Rais Magufuli alionekana bado akizungumza na mtu mmoja mmoja waliokuwa jirani naye huku akitaniana nao na kufurahia jambo hilo.

Katika utani huo huku akiwa amemshika mkono kijana mmoja, walitembea kutoka kwenye kivuko hicho, alimhoji kuwa ni mwenyeji wa wapi ambako alijibu ni wa Morogoro na Rais alitania kuwa mbona yeye ni mrefu huku akidai watu wa mji huo pamoja na wale wa Mbeya ni wafupi, jambo lililoibua kicheko kwao.

Kila alikopita, Magufuli alisalimia kwa kupunga mkono na kutumia neno ‘hamjambo’.

Akizungumza eneo hilo la ng’ambo ya jiji, Rais alisema Serikali yake iko pamoja nao wala haitawaacha na itaendana na Watanzania wote bila kubagua vyama, dini, makabila kwa kuwa yeye ni wa Watanzania wote.

Kutokana na kupata maswali mengi kutoka kwa wananchi wa eneo hilo ambayo yalihitaji kupatiwa majibu, Rais alisema yatashughulikiwa na viongozi wao ambao atawaelekeza.

“Yapo mengi mliyouliza hapa, inawezekana mengine nisipate majibu leo, lakini nitawaelekeza watu wangu, Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, wakurugenzi haya yote mliyoyauliza yaweze kufanyiwa kazi. Ninafahamu kuhusu suala la barabara, palikuwa na barabara kuu, za mkoa, za wilaya na za Manispaa. Suala la barabara ndiyo maana tumeamua kuunda agency nyingine ya barabara ambazo zitashughulikia za halmashauri na zile za mitaa,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alisema Serikali itahakikisha barabara nyingi na hasa kwenye miji ziwe zimetengenezwa kwa kiwango cha lami kupitia mfuko wa barabara ulioanzishwa.

Baadhi ya wananchi ambao walionekana kuzungumzia kitendo hicho cha Rais kuvuka na kivuko hicho huku akichanganyikana na wananchi wa kawaida walionesha kushangazwa na jambo hilo.

“Unajua pantoni hii ni shida,” alisema mmoja wao.

Mwingine aliyezungumza alisema Rais Magufuli ni wa ajabu na amejisikia vizuri kujumuika naye.

“Nimejisikia vizuri, ni Rais wa ajabu, habaki ofisini kusubiri ripoti, anakuja kwa wananchi wa hali ya chini, ni Rais anayetaka kujua shida ya Mtanzania wa chini na muda wote yuko bega kwa bega na watu wa chini,” alisema.

Katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, ilieleza kuwa Rais Magufuli alizungumza na wananchi na kwa kuhusu ubovu wa barabara alisema Serikali ilichukua hatua ya kukabiliana  na tatizo hilo kwa kuanzisha Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) ambayo itafanya kazi ya kutengeneza barabara kwa kiwango cha lami.

Kuhusu suala la kukatika kwa umeme, Rais alisema Serikali inatekeleza miradi mbalimbali itayoongeza kiwango cha umeme katika gridi ya taifa pamoja na kurekebisha miundombinu yake hivyo aliwaomba kuwa na subira wakati juhudi hizo zinaendelea.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Rais akiwa katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwl. Nyerere, alikutana na vijana wa CCM vyuo vikuu vya Mkoa wa Dar es Salaam waliopiga kambi katika chuo hicho, ambako aliwaeleza viongozi wa Sekretarieti ya CCM aliowakuta wakizungumza na vijana hao kuwa anazo taarifa za watu waliojimilikisha mali za chama na kuwa anasubiri wakati ukifika achukue hatua zinazostahili.

Pamoja na vijana hao kumhakikishia kumuunga mkono katika kuitumikia nchi, Rais Magufuli aliwataka kuwa nguzo imara ya mabadiliko ya kweli nchini ili juhudi zinazofanywa na Serikali yake katika kurekebisha mambo yaliyosababisha kukiuka misingi ya Waasisi wa Taifa zizae matunda.

Rais alisema baadhi ya juhudi hizo kuwa ni kukabiliana na rushwa inayodhoofisha uchumi na huduma za kijamii, kudhibiti mianya ya matumizi mabaya na upotevu wa fedha na mali za umma, kuondoa watumishi hewa na wenye vyeti vya kughushi, kuongeza bajeti ya maendeleo katika bajeti ya Serikali, kuongeza uzalishaji wa umeme, kujenga viwanda, kujenga reli, kununua ndege za Serikali, kuongeza ukusanyaji wa kodi na kuchukua hatua kali dhidi ya wahujumu uchumi.

“Nataka niwahakikishie vijana wote kuwa nawapenda sana, hata mimi nilikuwa Umoja wa Vijana, yote yaliyotokea kinyume na misingi ya chama hiki na misingi ya waasisi wetu wakiongozwa na Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere, nimeamua kuyanyoosha na yatanyooka na nyinyi simameni imara, kitumikieni chama na msitumikie watu au vikundi vya watu, mkifanya hivyo kila kitu kitakwenda vizuri kabisa,” alisema Rais Magufuli.

Taarifa hiyo ilisema Rais Magufuli aliwataka vijana hao kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa chama utakaofanyika baadaye mwaka huu.

Aliwataka kutokuwa na hofu ya rushwa kwa kuwa wote watakaojihusisha na vitendo hivyo hawatapitishwa kuwania nafasi za uongozi ndani ya chama.

Baada ya kutoka hapo Rais Magufuli alitembelea Daraja la Nyerere na kuzungumza na wananchi wa eneo hilo

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles