27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

ZAO LA MKONGE LAWEZA KUFUTA UMASIKINI

Na AMINA OMARY


MKONGE unaozalishwa nchini Tanzania ni wa pili duniani kwa ubora kwenye  soko la dunia baada ya Brazil.

Zao hilo katika miaka ya 1970 hadi 80 lilikuwa likizalishwa kwa wingi na kuuzwa nchi za nje, hivyo lilikuwa ni moja ya zao ambalo lilikuwa linachangia pato la Taifa.

Kwani takwimu zilikuwa zinaonyesha zao hilo lilikuwa linachangia kiasi cha asilimia 65 ya pato la Taifa miaka hiyo lilitokana na uuzwaji wa malighafi ya zao hilo nje ya nchi.

Hali hiyo ilisababisha Mkoa wa Tanga kuwa maarufu kutokana na kuzalisha kwa wingi zao hilo pamoja na kuwepo kwa fursa za ajira kwa wananchi wake.

Mashamba makubwa ya zao hilo yalikuwepo kwa wingi  mkoani humo, huku mashamba machache yakiwa katika mikoa jirani ya Morogoro, Arusha na Kilimanjaro.

Hivyo kuwepo kwa zao hilo kulikuwa ni fursa nzuri ya kiuchumi kwa mkoa huo pamoja na Taifa kwa ujumla kutokana na umuhimu wake katika kuongeza kipato.

Zao hilo lilikuwa  linatumika kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo magunia, vikapu,viti pamoja na uzalishaji wa kamba pamoja na singa kwa ajili ya kuuzwa nje ya nchi.

Hata hivyo, waswahili wanasema ivumayo haidumu msemo huo ndio ulioikuta sekta ya mkonge kwani uzalishaji wake ulianza kuyumba na kushuka hadi kumkatisha tamaa mkulima.

Kwa mtazamo wangu ni kwamba kwa sasa zao hilo limeanza kurudi katika thamani yake kwenye soko la dunia, hivyo ni wajibu wa Serikali kuhakikisha inaweka mipango madhubuti ya kuhakikisha zao hilo linarudi kwenye chati.

Ikumbukwe kuwa mkonge ni zao ambalo linastahamili ukame na haliwezi kuathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi, lakini zaidi mkulima akiwa na uhakika wa soko lake kutokana zao hilo kuwa na matumizi makubwa mtambuka. Katika soko la dunia ni fursa kwa Serikali pamoja na bodi kuja na mikakati ambayo itasaidia kuongeza uzalishaji wenye tija.

Kwani licha ya zao hilo kuwa na eneo lenye ukubwa wa Hekta 150,000 nchi nzima, lakini eneo linalotumika kwa uzalishaji ni hekta 37,000 pekee.

Kwa mtazamo wangu kunahitajika uwekezaji mkubwa kwenye mashamba katika kuinua na kuimarisha uzalishaji wa kilimo hicho pamoja na kuwashawishi wakulima wadogo kuona umuhimu wa kulima zao hilo kwa wingi na hata kujiunga vikundi.

Kutokana na maendeleo ya kiteknolojia inayokua kwa kasi mazao ya zao hilo kuanzia majani hadi shina lake, hivyo kama kutafanyika uwekezaji mzuri zao hilo linaweza kuja kuwa mkombozi mkubwa wa uchumi.

Kutokana na kukua kwa teknolojia duniani, katani wani inaweza kutumika katika kuzalisha bidhaa za ujenzi, nishati ya umeme, bidhaa zitokanazo na urembo wa nyumba pamoja na vifaa vya magari.

Kutokana  na nchi yetu kutekeleza sera ya viwanda, zao la mkonge ni fursa pekee ambayo  ndio itakayoweza kuleta mapinduzi ya haraka ya ujenzi wa viwanda hadi katika maeneo ya vijijini.

Kwani kila penye shamba la mkonge ni wajibu kuwepo na mashine ya korona kwa ajili ya kuzalisha malighafi ya kamba au singa zitokanazo na zao hilo.

Naamini kama wananchi wataweza kuhamasishwa kulima kwa wingi zao hilo wataweza kuepukana na tatizo la ukosefu wa ajira, kwani wataweza kujiajiri wenyewe kupitia kilimo na viwanda.

Ni vema sasa uhamasishaji wa kilimo cha mkonge uende sambamba na matumizi ya bidhaa zitokanazo na zao hilo ndani na nje ya nchi ili kuongeza soko la bidhaa hizo kwa kiasi kikubwa.

Kutokana na kampeni ya upigaji vita wa mifuko pamoja na vifaa vinavyoharibu mazingira, tuwekee mkazo matumizi ya bidhaa zitokanazo na mkonge hususani vikapu kwani ni rafiki wa mazingira.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles