Pyinmana, Myamar
Idadi ya waandamanaji wanaounga mkono demokrasia waliouwawa tangu yaliypofanyika mapinduzi ya kijeshi nchini Myanmar,imefikia zaidi ya watu 500.
Hiyo ni kwa mujibu wa shirika la kufuatilia hali ya nchi hiyo ambalo limetoa ripoti hiyo leo jumanne. Shirika hilo la harakati za kuwasaidia wafungwa wa kisiasa AAPP limesema jumla ya waliouwawa ni watu 510.
Idadi hiyo imetajwa baada ya watu wengine 14 kuuwawa mikononi mwa vikosi vya usalama siku ya jumatatu.
Hali inayozidi kuwa mbaya nchini Myanmar imeishtuwa jumuiya ya kimataifa na hasa vifo vya watu 110 vilivyoripotiwa siku ya jumamosi ambapo Umoja wa Ulaya uliita siku hiyo kuwa siku ya ugaidi.
Moja ya makundi makubwa yaliyoko nyuma ya maandamano nchini humo,jana lilitowa mwito wa kuyataka makundi yote ya kikabila ya Myanmar yenye silaha kuwaunga mkono waandamanaji,wito ambao pia leo umeungwa mkono na makundi matatu.