Na Derick Milton, Busega
Serikali imetangaza rasmi bei ya zao la Pamba katika msimu mpya wa ununuzi wa zao hilo msimu wa 2020/21, ambapo kilo moja itanunuliwa kwa Sh 1,050 kwa pamba daraja la kwanza, huku daraja la pili bei yake ikiwa Sh 525.
Bei hiyo mpya imetangazwa leo ikiwa ni ongezekezo la Sh 240 ya bei iliyotangazwa mwaka Jana msimu wa 2019/20 ambapo ilikuwa Sh 810 kwa kilo moja sawa na asilimia 30 ya ongezeko la bei hiyo iliyotangazwa leo.
Akitangaza bei hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwera kwenye hafla ya uzinduzi wa msimu wa ununuzi wa zao hilo iliyofanyika katika kijiji cha Mkula, amesema kuwa licha ya bei kupanda bado tija imekuwa ndogo kwenye zao hilo.
Mwera amesema kuwa katika msimu wa mwaka huu, uzalishaji wa pamba umeongezeka kutoka tani 122,650 msimu wa mwaka 2019/20 na kufikia tani 393,000 msimu wa 2020/21 ongezekezo la asilimia 68 ya uzalishaji, ambapo mkoa wa Simiyu umezalisha tani 141,095.
“Niagize halmashauri pamoja na bodi ya pamba, kuhakikisha elimu zaidi inawafikia wakulima kufuata kanuni bora za kilimo, lakini pia kuimarishwa shughuli za ugani kwa maafisa ugani kwa kuwapatia vitendea kazi ikiwemo usafiri ili waweze kuwafikia wakulima wengi zaidi na kuwapa elimu,” amesema Mwera.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ameitaka bodi ya pamba kushirikiana Mahakama, katika kuanzisha Mahakama inayotembea kuweza kuwachukulia hatua kali wale wote ambao watabainika kuchezea mizani ya kupitia kwa lengo la kuwaibia wakulima.
Awali akizungumza kwenye hafla hiyo Mkurugenzi wa Bodi ya pamba Marko Mtunga amesema kuwa licha ya serikali kutoa Elimu kwa wakulima kufuata kanuni bora za kilimo, bado eneo la kupanda kwa mstari limekuwa changamoto kubwa kwa wakulima.
“Tija inapotea Sana kwenye eneo hili la kupanda kwa mstari, ingawa baadhi wanafuata kanuni hii lakini wengi bado hawafuati kanuni hii na kisababisha tija kuendelea kuwa kidogo, kuna mkulima anaweza kulima shamba la hekari 10 lakini mavuno yake ni shamba la hekari tatu kwa sababu hajafuata kanuni,” amesema Mtunga.
Aidha Mkurugenzi huyo amewataka wadau wa zao hilo kuhasisha wakulima kujiunga na Amcos kwani changamoto nyingi ambazo zinalikabili zao hilo utatuzi wake upo chini ya Amcos ikiwa wakulima wengi watajiunga.
Joshua Emmanuel mmoja wa wakulima ameishukuru bei kuongezeka huku akieleza kuwa bado ongezekezo hilo halijaleta matumaini kwa wakulima walio wengi kutokana na kutumia gharama kubwa katika uzalishaji.
Naye Katibu wa Chama cha wanunuzi wa pamba nchini, Boaz Ogolla amesema kuwa wanunuzi wako tayari kununua pamba yote ambayo wamezalisha wakulima kwani uwezo upo na uhitaji ni mkubwa kwenye viwanda vyao.
Hata hivyo licha ya serikali kutangaza bei, lakini haikutangaza mfumo upi wa ulipaji wakulima utatumika kama utakuwa wa benki, simu au pesa taslimu kama ambavyo ilitangazwa uko nyuma kuwa mfumo utakaotumika msimu huu ni Benki na simu.