Lulu Ringo, Dar es Salaam
Baada ya kusambaa kwa tetesi kuwa baadhi ya wachezaji wa Klabu ya Yanga kutakiwa na baadhi ya vilabu hapa nchini, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera amefunguka na kusema kama kuna mchezaji anayetaka kujiunga na klabu hizo ruksa kuondoka.
Akizungumza na Mtanzania Digital leo Ijumaa Machi 29, Zahera amewataja wachezaji hao kuwa ni Kelvin Yondani, Papy Tshishimbi, Ibrahim Ajibu na Feisal Salum (Fei Toto).
Amesema kama wachezaji hao wako tayari kuondoka waondoke kwani hakuna mchezaji ambaye akikosekana katika kikosi cha Yanga basi timu itashindwa kufanya vizuri.
“Nataka kuwakumbusha kwamba zipo mechi nyingi tumecheza bila Yondani na tukashinda, nyingine bila Feisal na tulishinda na kuna nyingine tulicheza bila wao wote na bado tulipata ushindi.
“Yanga ya leo hakuna mchezaji hata mmoja ambaye timu yetu inaweza kulia au kukosa usingizi kwa sababu hachezi au ameondoka kama kuna mchezaji yeyote anataka kuondoka anaweza kuondoka, hakuna mchezaji anaweza kuniogopesha kwa kuwa timu fulani inamtaka,” amesema Zahera.
Aidha, kocha huyo amesisitiza Yanga ina wachezaji wazuri lakini ana mikakati ya kusajili wachezaji wazuri na wakubwa hivyo msimu ujao anaamini Yanga itakuwa timu ya kuogopeka.
“Nimewaambia viongozi wa Yanga kama maneno ninayosikia kuwa mchezaji fulani anatakiwa na timu fulani ni yakweli wasitetemeke, tena wawape na ruhusa ya kuondoka kwa kuwa usajili wa msimu ujao si wa kitoto.
“Mimi napenda kumaliza usajili wa wachezaji wote baada ya Mei 15 na kutokana na usajili nitakaoufanya mtajionea wenyewe msimu ukianza baada ya miezi miwili mtaamini maneno yangu,” amesema Zahera.