*Kuala Lumpur, NS Matrix FC za Ligi Kuu zamuwinda
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
BEKI wa kati wa timu ya soka ya Yanga, Kelvin Yondani, huenda akatimka ndani ya klabu hiyo baada ya mkataba wake kumalizika, ikiwa dili lake la kwenda kucheza soka la kulipwa nchini Malaysia litakamilika.
Inadaiwa kuwa Yondani ambaye ni mmoja kati ya wachezaji wakongwe waliopo ndani ya kikosi cha Yanga, anahitajika katika klabu mbili kubwa zinazoshiriki Ligi Kuu ya Malaysia ya Kuala Lumpur inayoongoza katika msimamo wa ligi na NS Matrix inayoshika nafasi ya pili.
Chanzo cha habari ambazo zimelifikia MTANZANIA jana, kimeeleza kuwa mipango ya kumfuatilia mlinzi huyo ilianzia wakiwa visiwani Pemba, wakati Yanga ikiwa imejichimbia kambini kwa maandalizi ya mchezo wa awali wa hatua ya 16 bora dhidi ya timu ya Waarabu wa Misri, Al Ahly.
Chanzo hicho kimeeleza kuwa dili la kuuzwa kwa Yondani nchini Malaysia linasukwa na Mtanzania mmoja jina lake halikuwekwa wazi, ambaye anadaiwa kufanya mazungumzo na beki huyo ili kukamilisha suala hilo.
“Kuna mazungumzo ya chini kwa chini yanaendelea kati ya watu hao wawili ili kufanikisha dili hilo ambapo kama mambo yataenda sawa mchezaji huyo atapata fursa ya kucheza soka la kulipwa nje ya Bara la Afrika,” alisema.
Ikiwa dili hilo litafanikiwa, mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara watalazimika kutafuta mrithi wa Yondani au kuanza kumchezesha beki Pato Ngonyani, ambaye mara nyingi amekuwa akicheza kama mbadala wake anapokosekana ndani ya kikosi.
Timu ya Kuala Lumpur inayomuhitaji beki huyo ilianzishwa mwaka 1974 na sasa inaongoza katika msimamo wa ligi ya Malaysia, ikiwa imefikisha pointi 17 baada ya kucheza michezo saba na kushinda mara tano kupata sare mbili.
Kwa upande wa timu kongwe ya NS Matrix iliyoanzishwa mwaka 1923 katika mji wa Seremban, inashika nafasi ya pili kutokana na pointi 15 walizovuna kwa kucheza mechi saba, kushinda mara nne na kutoka sare mara tatu.
Kama Yondani atafanikiwa kuondoka Yanga baada ya mkataba wake kumalizika, klabu hiyo yenye maskani yake Mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam itakuwa imepata hasara kwa kukosa fedha za mauzo ya nyota huyo.
Suala la Yondani litakuwa halitofautiani na la winga, Mrisho Ngassa, kwani baada ya kumalizika ligi msimu uliopita mshambuliaji huyo pia aliondoka ndani ya kikosi kama mchezaji huru baada ya kumalizika kwa mkataba wake na kujiunga na klabu ya Free State Star ya Afrika Kusini.