Na KULWA Mzee – DAR ES SALAAM
UPANDE wa Jamhuri katika kesi inayomkabili mfanyabiashara Yericko Nyerere, unatarajia kuita mashahidi sita na kutoa vielelezo vitatu wakati wa usikilizaji wa shauri hilo.
Yeriko anakabiliwa na kesi ya kuchapisha maneno yenye nia ya uchochezi kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook iliyoko katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Hayo yalibainishwa jana na Wakili wa Serikali, Clara Charwe, wakati akimsomea Yericko maelezo ya awali mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, Respicius Mwijage.
Katika maelezo hayo, Yericko alikubali maelezo yake binafsi ambayo ni jina lake, yeye ni mfanyabiashara na kwamba alishtakiwa.
Yericko anadaiwa kuwa Mei 28, 2017 kwa nia ya kuwachochea Watanzania, alichapisha maneno kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook yasemayo:
“Maazimio ya Baraza Kuu yalikuwa (1) Katiba Mpya (2) Tume Huru (3) Bunge (4) Haki ya Kikatiba ya kuishi (Ben Saanane) (5) Haki ya Kikatiba ya kukutana na kuzungumza (Mikutano ya Hadhara ya Kisiasa) Hayo ndio yatahubiriwa katika Operesheni Ukuta.
“Baraza Kuu limeridhia kwa kauli moja kwamba vita rasmi ya kulikomboa taifa imezinduliwa na kama wewe Mtanzania unaogopa kulitetea taifa hili, ni bora ukakaa kando, nenda huko CCM ambako michemsho na supu vipo kwa wingi… kufa kwetu ni ukombozi wa Tanzania…
“Yaani sasa tunarejesha siasa za jino kwa jino, uso kwa uso, mguu kwa mguu, weka mguu niweke ugoko… Ni mwisho kuishi kinyonge, ni mwisho kulalamika, ni mwisho watu wetu kutekwa au kuuawa, ni mwisho watu wetu kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara… Tunasema sasa ni single touch double manifestational.” Mwisho wa kunukuu.
Shauri hilo limepangwa kuanza kusikilizwa kwa mashahidi wa upande wa Jamhuri, Desemba 13, mwaka huu. Mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.