30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MELI YA MATIBABU: WAGONJWA WATOLEWA HOSPITALINI

NASUBIRI HUDUMA: Mmoja wa wagonjwa akiwa amekaa chini kwenye foleni ya kuandikisha jina kwa ajili ya kupata huduma ya matibabu ya bure katika Meli ya Ark of Peace kutoka nchini Bandarini Dar es Salaam jana. Picha na Loveness Bernard

PATRICIA KIMELEMETA-DAR ES SALAAM

BAADHI ya ndugu na jamaa wamewatoa wagonjwa wao katika hospitali mbalimbali nchini na kuwapeleka kwenye kambi ya matibabu inayotolewa na madaktari kutoka China kwenye meli iliyotia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam (TPA).

Meli hiyo iliyowasili Novemba 20 mwaka huu ina madaktari bingwa 381,vifaa na dawa za kutosha kwa ajili ya kutoa bure huduma kwa wakazi wa Dar es Salaam.

 Wakizungumza na MTANZANIA jijini Dar es Salaam jana, ndugu wa wagonjwa ambao wametolewa hospitali kwenda pale kupata matibabu walisema wanaamini madaktari hao wanaweza kuwatibu kuliko tofauti na huko walipo.

“Nimemtoa mgonjwa wangu hospitali, anasumbuliwa na saratani, tunaamini madaktari wa China wanaweza kumtibu na akapona kuliko kupigwa mionzi,” alisema Amina Juma mkazi wa Kimara.

Hata hivyo hadi MTANZANIA linatoka eneo la Polisi Central ndugu huyo wa mgonjwa alikuwa hajapata namba, hali ambayo alieleza kuwa inaweza kusababisha wakashindwa kupata matibabu huku kiiomba Serikali kuwasaidia ili wapate huduma hiyo.

Mkazi mwingine wa Mbagala, Omary Khamis alisema mzazi wake anasumbuliwa na maradhi ya kuvimba tumbo na alikuwa amelazwa hospitali (hakuitaja) lakini waliposikia ujio wa madaktari hao walilazimika kumwondoa ili waweze kupata namba.

Hata hivyo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Grace Maghembe alipiga marufuku watu wanaowatoa wagonjwa hospitali na kuwapeleka kwenye kambi hiyo ili waweze kupatiwa matibabu.

Alisema, mgonjwa ambaye tayari alishaanza huduma za matibabu kwenye hospitali mbalimbali nchini, anapaswa kuendelea kutibiwa kwenye hospitali hiyo mpaka atakapomaliza matibabu yake.

“Ni marufuku kwa ndugu na jamaa kutoa wagonjwa hospitali na kuwaleta hapa kwa sababu wanaweza kuchanganyia dawa ambazo baadaye zinaweza kuwaletea madhara, hivyo tukigundua kama kuna mgonjwa ametolewa hospitali, tutamwondoa”alisema Dk Maghembe.

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda alisema hadi juzi jioni, zaidi ya wagonjwa 561 wamepatiwa huduma za matibabu kwenye meli hiyo.

Alisema wagonjwa ambao wataonekana kuwa na hali mbaya watalazimika kupelekwa China bure kwa ajili ya kupatiwa huduma za matibabu.

Makonda alisema ofisi yake itasimamia utaratibu wote wa upatikanaji wa hati za kusafiria (passport)  ili kuhakikisha wagonjwa hao wanapata fursa ya matibabu nchini humo.

Alisema meli hiyo ina zaidi ya vitanda 300, hivyo basi wagonjwa waliopangiwa kulazwa watapatiwa huduma hiyo pamoja na malazi bure ikiwemo chakula, vinywaji na mavazi.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles