Damian Masyenene, Mwanza
MABINGWA wa Kihistori Tanzania Bara, Yanga SC imewasili salama jijini Mwanza kwa ajili ya mchezo wao wa kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Alliance FC ya Mwanza utakaopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini hapa.
Yanga ambayo imewasili asubuhi Saa 1:30 kwa ndege ya Air Tanzania na kulakiwa na mashabiki wao kisha kuelekea Hoteli ya JB Belmont kwa mapumziko, wataivaa Alliance ambayo ilikuwa nchini Rwanda kwa kambi ya siku tano.
Hata hivyo Nahodha wa Wana Jangwani hao, Ibrahim Ajibu hajaongozana na wenzake kwenye safari hiyo (Ameachwa Dar), ambapo Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amebainisha sababu zilizofanya asijumuishwe kwenye mchezo huo.
Mkongomani huyo ameeleza kwamba Ajibu ameachwa Dar es Salaam kwasababu hajawa na utimamu wa mwili kutokana na kuanza mazoezi Jumanne baada ya kusumbuliwa na majeruhi ya nyama za paja hivyo hajafanya mazoezi ya kutosha na kuivaa kucheza mchezo huo.
Zahera amesema kwamba mchezo huo wa robo fainali ni muhimu kwao ili kujihakikishia nafasi ya kufuzu nusu fainali na kwenda fainali hatimaye kukata tiketi ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa barani Afrika mwakani.
Timu hizo zimekwishakutana mara mbili msimu huu kwenye Ligi Kuu, Yanga akishinda zote kwa jumla ya mabao 4-0, ambapo mchezo wa kwanza walishinda 3-0 (Uwanja wa Taifa) na 1-0 (CCM Kirumba).
Katika michuano ya FA, tayari timu za KMC na Lipuli FC zimekwishafuzu hatua ya nusu fainali baada ya kuahinda mechi zao za robo fainali hapo Jana, KMC wakiichapa African Lyon 2-0 na Lipuli wakiikung’uta Singida United 2-0.