24.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga yateka usajili

IMG_5436[1]NA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM

TIMU ya Yanga imeendelea kuteka soko la usajili nchini, baada ya jana mchana kuwanasa wachezaji wawili kwa mpigo, beki wa kushoto Mwinyi Haji Mngwali na kipa wa Kagera Sugar, Benedicto Tinocco.

Usajili wa wachezaji hao unaifanya timu hiyo kufikisha idadi ya wachezaji watatu iliyowasajili mpaka sasa baada ya Jumapili iliyopita kumsainisha winga Deus Kaseke aliyetoka Mbeya City.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro, alilithibitishia MTANZANIA jana kuwa wameingia mkataba wa miaka miwili na nyota hao ikiwa ni sehemu ya kuendelea kuimarisha kikosi chao.

“Ni kweli leo (jana) tumeingia mkataba na nyota hao, hiyo ni sehemu ya sisi kuimarisha kikosi chetu, kama unavyojua mwakani tunashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema.

Muro aliendelea kueleza kuwa bado wanaendelea na mazungumzo na winga Haroun Chanongo na kudai kuwa muda wowote kuanzia leo wanaweza kutangaza usajili wake.

Mngwali ni mmoja ya wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ walioshiriki michuano ya Kombe la Cosafa, alicheza mechi ya mwisho dhidi ya Lesotho iliyoisha kwa Stars kufungwa bao 1-0.

Beki huyo wa zamani wa KMKM ya Zanzibar, anaungana na wachezaji wa Yanga mkongwe, Oscar Joshua na kinda Edward Charles kuwania namba kwenye beki ya kushoto.

Tinocco aliyetokea kwenye programu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ya Stars Maboresho, yeye atakuwa na mtihani mkali kuwania namba langoni mbele ya wakongwe, Ally Mustapha ‘Barthez’ na Deogratius Munishi ‘Dida’.

Yanga imepania kufanya usajili wa nguvu ili kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa mwakani, hadi sasa ina wachezaji saba wa kimataifa ambao itawafanyia majaribio kuanzia wiki ijayo akiwemo mshambuliaji wa FC Platinum, Donald Ngoma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles