25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

YANGA YASHUSHWA SHIRIKISHO

WAANDISHI WETU-NDOLA NA BULAWAYO

TIMU ya Yanga imeangukia hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kuondolewa katika mchuano ya  Ligi ya Mabingwa Afrika, kwa kuchapwa mabao 2-1 na Zesco United,  katika mchezo wa marudiano uliochezwa jana Uwanja wa Levy Mwanawasa mjini Ndola,  Zambia.

Yanga imetupwa nje ya kinyang’anyiro hicho kwa kulazwa jumla ya mabao 3-2 na Zesco,  baada ya sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza uliochezwa Septemba 15, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hata hivyo, Wanajangwani hao wamepata nafasi ya kushiriki hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kulingana na kanuni za Shirikisho la Soka Afrika(Caf), ambalo linazipa ofa hiyo timu zilizofika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwa mara ya mwisho, Yanga ilitinga hatua ya makundi Kombe la Shirikisho mwaka juzi ilipokuwa inanolewa na kocha, George Lwandamina, ambaye jana aliiongoza Zesco kutinga hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa .

Katika mchezo wa jana, Yanga ilimaza mchezo ikiwa pungufu,  baada ya beki wake Mghana, Lamine Moro kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 90. Moro alipewa adhabu hiyo baada ya awali kulimwa kadi ya njano kutokana na mchezo usio wa kiungwana.

Yanga ilitinga hatua hiyo, baada ya kuitoa mashindanoni timu ya Township Rollers  ya Botswana kwa ushindi wa jumla ya mabao 2-1, ikianza kulazimishwa sare ya bao 1-1, Uwanja wa Taifa kabla ya kushinda bao 1-0 jijini Gaborone.

Wawakilishi wengine wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho, timu ya Azam FC jana ilifungashiwa virago baada ya kuchapwa bao 1-0 na Triangle United ya Zimbabwe ugenini mjini Bulawayo. Azam imeaga mashindano hayo kwa kufungwa jumla ya mabao 2-0, ikianza kuchapwa bao 1-0 nyumbani Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Mchezo huo ulianza kwa kasi huku wenyeji Zesco wakionekana kupania kutingisha nyavu za Yanga mapema.

Jesse Were aliindikia Zesco bao la kuongoza kwa kichwa dakika ya 24, akiunganisha krosi safi ya Simon Swilimba.

Bao hilo lilifanya Zesco kujiamini zaidi na kuendelea kumimina mashambulizi makali kwenye lango la Yanga, lakini uimara wa safu ya ulinzi iliyokuwa chini ya Kelvini Yondani,  ilikuwa kikwazo kwa Zesco.

Sadney Khoetage alizima tambo za mashabiki wa Zesco,  baada ya kuisawazishia Yanga dakika ya 30,  akimalizia pasi ya Patrick Sibomana.

Beki wa Yanga, Lamine Moro alilimwa kadi ya njano dakika ya 39 baada ya kumchezea rafu Were.

Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilikamilika kwa timu hizo kwenda mapumziko zikiwa zimefungana bao 1-1.

Kipindi cha pili, Zesco iliongeza kasi ya mshambulizi ikilenga kusaka mabao zaidi.

Wakati huu Yanga ilionekana kucheza mchezo wa kujilinda zaidi, hatua iliyotoa fursa kwa wapinzani wao kutawala.

Washambuliaji wa Yanga, Sadney na Sibomana walionekana kukosa  mbinu za kuwashinda mabeki wa Zesco.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alifanya mabadiliko alimtoa Sadney na  kumwingiza Juma Balinya dakika ya 70.

Kiungo wa Yanga, Abdulazizi Makame alifuta ndoto za mashabiki wa timu hiyo kutinga hatua ya makundi  baada ya kujifunga akiwa kwenye harakati za kuokoa hivyo kuipa Zesco bao la pili dakika ya 79 wakati akiwa katika harakati za kuokoa mpira wa krosi.

Bao hilo liliishtua Yanga na kuanza kupeleka mashambulizi ikitumia mipira mirefu ambayo hata  hivyo iliokolewa na mabeki wa Zesco.

Zahera alifanya mabadiliko mengine dakika ya 85, alimtoa Ally Ally na na kumwingiza Maybin Kalengo kabla ya kumtoa Sibomana na kumwingiza Mrisho Ngasa.

Moro alijikuta akishindwa kuhimili presha ya mchezo na kucheza rafu iliyomgharimu,  baada ya kulimwa kadi nyekundi dakika ya 90.

Dakika 90 zilikamilika kwa Yanga kulala kwa mabao 2-1.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles