24.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

YANGA YASHINDWA KULIPA KISASI

Zainab Iddy-Dar Es Salaam

TIMU ya Yanga na Azam, zimeshindwa kutambiana baada ya jana kutoka suluhu, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Timu hizo zilipokutana katika mchezo wa mzunguko wa kwanza kwenye uwanja huo, Azam ilitakata kwa bao 1-0 dhidi ya Yanga.

Sare hiyo imeifanya Yanga kubaki nafasi ya tatu, ikiwa na pointi 56, baada ya kucheza mechi 30, sawa na Azam iliyopo nafasi ya pili, ikiwa na pointi 58, huku Simba ikikamata uongozi wa ligi ikiwa na pointi 75.

Mchezo huo uliochezewa na mwamuzi Elly Sasii, ulianza taratibu lakini kadri muda ulivyokwenda kasi iliongezeka.

Dakika ya tisa, Azam ilikosa bao baada ya Idd Kipangwile akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga  kupiga shuti lililotoka nje, baada ya pasi ya Mudathir Yahya.

Dakika  ya 12, Kipangwele alipoteza nafasi nyingine ya kufunga baada ya mkwaju wake kutoka nje ya lango la Yanga.

Dakika ya 14, Patrick Sibomana alipokea krosi ya David Molinga, lakini kiki yake ilipanguliwa na kipa Benedick Haule wa Azam.

Dakika ya 15, Haule alifanya kazi nzuri, baada ya kupangua mpira wa kichwa uliopigwa na Ditram Nchimbi na kuzaa kona ambayo haikuwa na faida kwa Yanga.

Dakika ya 24 Metacha alifanya kazi nzuri, baada ya kupangua mashuti ya Mudathir Yahya na  Idd Seleman ndani ya sekunde chache.

Dakika ya 32, mkwaju wa Feisal Salum ulipanguliwa na Haule,

Dakika ya 33, Azam ifanya shambukizi la nguvu langoni mwa Yanga lakini kiki ya kiungo Never Tigere ilitoka nje.

Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika kwa Yanga na Azam kwenda mapumziko zikiwa nguvu sawa.

Yanga iliingia uwanjani kipindi cha pili ikiwa na nguvu zaidi, hasa baada ya kocha wa timu hiyo Luc Eymael kumtoka Sibomana na kumwingiza Benard Morrison.

Dakika  ya 47,  Seleman aliutumbukiza mpira wavuni lakini mwamuzi wa pembeni, Sudi Lila alinyoosha kibendera chake kuashiriki mfungaji alikuwa ameotea.

Dakika ya 48, mkwaju wa Morrison ulipanguliwa na Haule na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Dakika ya 51, Nchimbi angeweza kuifungia Yanga bao la kuongoza kama angekuwa makini kutumia vizuri krosi ya Morrison na badala yake kupiga mpira nje.

Dakika ya 69, mkwaju wa Yikpe Gislain  aliyepokea pasi ya Morrison ulitoka nje kidogo ya lango la Azam.

Pamoja na kila upande kujaribu kuutikisa wavu wa mpinzani wake, dakika 90 za kipute hicho zilikamilika kwa timu hizo kugawana pointi moja moja baada ya kutoka suluhu.

Kikosi cha Yanga:

Metacha Mnata, Deus Kaseke, Jafar Mohammed, Kelvin Yondan, Said Makapu, Feisal Salum Abdallah, Balama Mapinduzi/ Mrisho Ngassa (dk 64), Haruna Niyonzima, Ditram Nchimbi/ Abadullaziz Makame (dk 84), Patrick Sibomana/Bernard Morrison (dk 46)na David Molinga/ Ykpe (dk 64).

Kikosi cha Azam:

 Benedict Haule, Nico Wadada, Salmin Hozza, Abdallah Kheri, Oscar Masai, Mudathir Yahya, Idd Kipagwile/ Bruce Kangwa, Braison Rafael/ Khalefine Hamdoum (Dk 85), Richard Djodi, Niver Teger/ Shaaban Iddy (Dk 59) na Idd Seleman/ Abdallah Masoud (Dk 85).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles