22.5 C
Dar es Salaam
Friday, June 21, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga yasaka ushindi Shinyanga

yangaNA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

TIMU ya soka ya Yanga leo inakabiliwa na kibarua kigumu ugenini itakaposhuka dimbani kuvaana na Stand United katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Matokeo ya ushindi ni muhimu kwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu, ambao wamebakiza mechi nne lakini wanahitaji kushinda mbili kati ya hizo ili kutangazwa mabingwa.

Kwa sasa Yanga ndio vinara wanaoongoza katika msimamo wa ligi kwa kufikisha pointi 65 kutokana na mechi 26 walizocheza, wakifuatiwa na Azam FC waliojikusanyia pointi 59 ikiwa ni tofauti ya pointi moja dhidi ya Simba waliopo nafasi ya tatu kwa pointi 58 walizonazo.

Ikiwa Yanga watafanikiwa kuondoka na ushindi ugenini dhidi ya Stand wanaoshika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi wakiwa wamefikisha pointi 34, watakuwa wamejirahisishia kazi kwenye mbio za ubingwa msimu huu kwani watakuwa wamewaacha kwa mbali wapinzani wao Azam na Simba.

Wanajangwani hao wataingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 2-1 iliyopata dhidi ya Toto Africans Jumamosi iliyopita katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Akizungumza na MTANZANIA jana Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu ya Yanga, Jerry Muro, alisema licha ya kufurahia matokeo ya suluhu kwa Simba na Azam, wamepania kuhakikisha timu yao inaondoka na ushindi leo ili wazidi kukaribia kutetea ubingwa wanaoshikilia huku wakiwa hawajamaliza mechi zao.

“Matokeo ya sare juzi kwa wapinzani wetu Simba na Azam yalituongezea changamoto ya kuhakikisha tunapambana zaidi ili tupate ushindi dhidi ya Stand na Ndanda FC utakaochezwa Mei 16, mwaka huu,” alisema Muro.

Alisema baada ya mchezo wa leo wataanza maandalizi ya mchezo wa kimataifa wa hatua ya 16 bora wa Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya timu ya Sagrada Esperanca ya Angola utakaochezwa Mei 6, mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

“Michezo yote iliyobaki Ligi Kuu itakuwa ni sehemu ya maandalizi yetu kimataifa kwani tunaamini itasaidia kutujenga na kutuongezea ari ya kupambana ili kubaki na ushindi nyumbani,” alisema.

Muro alisema lengo la Yanga ni kuhakikisha timu hiyo inanyakua mataji matatu msimu huu ambayo ni ubingwa wa ligi, Kombe la FA na Kombe la Shirikisho Afrika.

Wakati huo huo, Bodi ya Ligi Kuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imepangua ratiba na kurudisha nyuma kwa siku moja mchezo kati ya Yanga na Ndanda ambao sasa utachezwa Mei 14 badala ya Mei 15, mwaka huu ili kutoa nafasi kwa Wanajangwani hao kujiandaa na safari ya kwenda nchini Angola kwenye mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho.

Pia kamati hiyo imesogeza mbele kwa siku moja mchezo wa Ligi Kuu kati ya Simba na Mwadui FC, ambapo sasa utachezwa Mei 8 badala ya Mei 7, mwaka huu kutokana na Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kutumika siku hiyo kwa mchezo wa awali wa Kombe la Shirikisho kati ya Yanga na Sagrada Esperanca ya Angola.

Mchezo mwingine uliosogezwa mbele ni ule utakaozikutanisha timu za Kagera Sugar na Azam FC ambao sasa utachezwa Mei 8, badala ya Mei 7, mwaka huu kutokana na Uwanja wa Kambarage, Shinyanga kutumika siku hiyo kwa mchezo kati ya Stand dhidi ya Coastal Union.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles