24.7 C
Dar es Salaam
Saturday, April 13, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga yampa kibarua kizito Pluijm

pg32 febr 10*Bunduki 21 zatumwa kufanya kazi Mauritius

ADAM MKWEPU NA THERESIA GASPER, DAR ES SALAAM

UONGOZI wa Klabu ya soka ya Yanga umempa majukumu mazito kocha wa timu hiyo, Hans van Pluijm, kuhakikisha anaifikisha timu  katika hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika.

Pluijm kabla ya kupewa jukumu hilo, kikosi chake kilikuwa kikisuasua kupata matokeo mazuri katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Hali hiyo ilipelekea baadhi ya mashabiki wa timu hiyo kutoa maoni tofauti juu ya mfumo wa 4-2-3 anaotumia kocha huyo, wakidai kuwa ndio chanzo cha timu hiyo kufanya vibaya baada ya mzunguko wa kwanza kumalizika.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Pluijm alisema timu hiyo inaweza kufikia malengo endapo wachezaji watakuwa kwenye kiwango  na ubora wa kuridhisha wa kupata ushindi.

“Siwajui vizuri wapinzani wangu, lakini si kitu muhimu, ninachotakiwa kufanya ni kuhakikisha wachezaji wanakuwa katika kiwango bora kitakachoniwezesha kupata ushindi.

“Najua watu wengi wanazungumzia mfumo wangu, kwa kuwa hawajui mfumo si unaocheza soka, bali ari ya wachezaji ndiyo inaweza kutufanya tupate matokeo mazuri, hivyo najiandaa kwenda kuchezesha mfumo huo ambao utawapa nafasi wachezaji ya kushambulia zaidi na kukaba,” alisema Pluijm.

Akizungumzia uimara wa kikosi chake, alisema kwamba baada ya mazoezi ya siku kadhaa,  ameweza kurekebisha makosa yaliyokuwa yakijitokeza kwenye baadhi ya michezo, hasa katika mzunguko wa pili.

“Tunasafiri kesho (leo) ili kupata siku mbili za mazoezi tukiwa ugenini na tupate kuzoea hali ya hewa ya ugenini,” alisema Pluijm.

Pluijm aliwataja baadhi ya wachezaji watakaosafiri kwenye kikosi hicho ni pamoja na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, licha ya mchezaji huyo kutokuwa na asilimia 100 ya kucheza kutokana na majeraha aliyokuwa nayo.

“Nasikitika tunaweza kumkosa Thaban Kamusoko, kutokana na jeraha la mfupa wa mguu alilopata kwenye mchezo wa juzi dhidi ya JKT Ruvu, lakini tutasafiri na Cannavaro, licha ya kutokuwa fiti kutokana na hali yake,” alisema Pluijm.

Ofisa Habari wa klabu hiyo, Jerry Murro, alisema kikosi hicho kimejiandaa kupata  matokeo mazuri katika mchezo huo wa awali dhidi ya timu ya Cercle De Joachim, unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi hii katika Mji wa Curepipe, nchini  Mauritius.

“Kikosi kinatarajia kuondoka kesho (leo) alfajiri, msafara ambao  utajumuisha wachezaji 21 pamoja na benchi la ufundi lenye watu saba, huku kiongozi wa msafara akiwa Ayoub Nyenzi, kutoka Shirikisho la Soka nchini (TFF), ambapo mechi hiyo itachezwa saa tisa na nusu alasiri kwa saa za Mauritius,” alisema.

Alisema waamuzi katika mchezo watakuwa ni Hubert Marie, Bruno, Randriannarivelo Ravonira, Augustin Gabriel Herinirina na  Anndofetrra Avombitana Rakotojiaona, wote kutoka nchini Madascar, huku kamisaa wa mchezo huo atakuwa  Feizal Ismael Sidat kutoka nchini Msumbiji.

“Kikosi chetu kimejiandaa vizuri kuhakikisha wachezaji wote wapo fiti kukabiliana na timu hiyo, ili kutimiza lengo letu la kuifikisha timu katika hatua ya makundi,” alisema.

Alisema wachezaji ambao wataukosa mchezo huo ni Geofrey Mwashiuya, golikipa namba tatu Tinoko ambao wanafuatilia hati za usafiri, pamoja na Matheo Simon, ambaye hayupo fiti kimchezo.

Jerry aliongeza kuwa mchezo wa marudiano unatarajiwa kufanyika baada ya wiki mbili katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Aidha, kiungo wa timu hiyo, Haruna Niyonzima, alisema kuwa baada ya kucheza michezo ya Ligi Kuu na kocha wao kujitahidi kurekebisha eneo lililokuwa na matatizo, wana matumaini ya kufanya vizuri kwenye mchezo  huo.

“Tuna uhakika wa kupata ushindi, licha ya mchezo kuonekana kuwa mgumu kulingana na mazingira, hivyo hatutaweza kudharau wapinzani wetu,” alisema Niyonzima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles