Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
BODI ya wadhamini wa klabu ya Yanga imeweka hadharani mkataba wa miaka 10 wa kigogo anayetaka kuikodisha klabu hiyo, ikiwa imepita miezi miwili tangu kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa dharura wa wanachama Agosti 6, mwaka huu.
Bodi hiyo chini ya Mjumbe Francis Kifukwe, imetengua kitendawili hicho cha muda mrefu baada ya wanachana kuridhia kwa kauli moja kumkodisha kigogo huyo aliyetaka kuchukua asilimia 75 ya mapato, huku 25 ikibaki kwa wanachama.
Baadhi ya vipengele vya mkataba wa kukodishwa timu hiyo kwa miaka 10 vinaonyesha kuwa kuanzia sasa klabu itajulikana kwa jina la Yanga Yetu Limited kutoka Yanga Africans Sports Club.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Baraza la Wadhamini la Yanga, ilieleza kuwa mkataba huo ulifanyika kwa kuzingatia haki miliki kutolewa kwa mkodishwaji ambapo jina lake na nembo zitatumika kibiashara na kuendesha shughuli za timu ya soka, bila kuingiliwa kwa muda wa miaka 10 kuanzia Septemba mosi, mwaka huu.
Kipengele kingine cha mkataba huo kinaeleza kuwa kigogo huyo atailipia Yanga deni la Sh bilioni 11,676, inayodaiwa kama mmiliki na mkopeshaji mmoja.
Pia atailipa klabu hiyo kiasi cha Sh milioni 100 kwa mwaka, ambapo klabu itapata fursa ya kuwekeza kiwango kisichopungua asilimia 90 ili kuimarisha mtandao wa matawi yake.
Kwa upande wa uwanja, mkataba unaonyesha kuwa kigogo huyo atailipa klabu katika mwaka wa fedha wowote ule, kukiwa kuna faida ya fedha taslimu ya asilimia 25 itakayotumika kujenga uwanja wake wa soka, ikiwamo majukumu ya kifedha kujumuishwa ada za usajili zinatakiwa kuanzia tarehe ya ufanisi na majukumu mengine.