27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

YANGA YAJIKAMULIA KAGERA SUGAR

  • Yaitungua mabao 3-0, Kamusoko aanza kazi

Na THERESIA GASPER – DAR ES SALAAM


YANGA imejifuta machozi ya kuchapwa mabao 2-1 na Township Rollers ya nchini Botswana katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya jana kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar, mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mabao ya Yanga yote yalipatikana kipindi cha pili yakifungwa na Ibrahim Ajib kwa mkwaju wa penalti dakika ya 53, Emmanuel Martin dakika ya 77 na lile la kujifunga la beki wa Kagera Sugar, Juma Shemvuni, dakika ya 88.

Kwa matokeo hayo, Yanga imefikisha pointi 43 na kurejea katika nafasi ya pili ikiishusha Azam yenye pointi 41 kwenye nafasi ya tatu, huku Simba ikiendelea kukalia kiti cha uongozi na pointi zake 46.

Mchezo huo ulianza taratibu lakini kadiri muda ulivyozidi kwenda kasi iliongezeka.

 

Dakika ya sita, Pius Buswita, alipokea pande safi la Ajib, lakini mkwaju wake dhaifu ulitoka nje la lango la Kagera Sugar.

Dakika ya 13, kipa wa Kagera Sugar, Ramadhan Chalamanda, alipangua kiki ya Buswita.

Dakika ya 18, mwamuzi Shomary Lawi wa Kigoma, alimlima kadi ya njano, Japhary Salum wa Kagera Sugar kutokana na kumfanyia madhambi Kelvin Yondani.

Dakika ya 19, Mwaita Gereza wa Kagera Sugar, alionyeshwa kadi ya njano baada ya kumchezea rafu, Emmanuel Martin.

Dakika ya 20, mkwaju wa mpira wa adhabu wa Ajib ulipaa juu ya lango la Yanga.

Yanga iliendelea kufanya mashambulizi na dakika ya 28, kipa Chalamanda alipangua kiki ya Ajib.

Dakika ya 33, kocha wa Yanga, George Lwandamina, alifanya mabadiliko alimtoa Pato Ngonyani na kumwingiza Maka Edward.

Chalamanda aliendelea kuizuia Yanga isiguse wavu wa Kagera dakika ya 34 baada ya kupangua kiki ya Obrey Chirwa.

Dakika ya 35, Kagera ilijibu kwa kufanya shambulizi, lakini kiki dhaifu ya  Japhet Makarai, iliishia mikononi mwa kipa wa Yanga, Rostand.

Dakika ya 44, Yanga ilifanya shambulizi la nguvu ambapo mkwaju mkali wa Martin ulipanguliwa na Chalamanda na kuwa kona kabla ya kuuwahi mpira na kuudaka.

Dakika ya 45 za kipindi cha kwanza zilikamilika kwa timu hizo kwenda mapumziko zikiwa suluhu.

Kipindi cha pili kila upande uliongeza kasi ya mashambulizi, dakika ya 49, mpira wa kichwa wa Atupele Green ulitoka nje kidogo ya lango la Yanga.

Dakika ya 49, Kagera Sugar ilipata pigo baada ya beki wa timu hiyo, Mohamed Fakhi, kuunawa mpira akiwa ndani ya eneo la hatari na mwamuzi kuamuru ipigwe penalti.

Penalti hiyo ilipigwa dakika ya 53 na Ajib ambaye aliiandikia Yanga bao la kuongoza.

Kuona hivyo, kocha wa Kagera Sugar, Mecky Mexime, aliamua kufanya mabadiliko alimtoa Adeyun Ahmed na kumwingiza Godfrey Taita.

Dakika ya 68, mkwaju dhaifu wa Ally Mashaka, ulitua mikononi mwa kipa wa Yanga, Rostand.

Dakika ya 70, mkwaju mkali wa Chirwa ulitoka nje kidogo ya lango la Kagera Sugar.

Dakika ya 71, kiungo Thaban Kamusoko, ambaye jana alicheza mechi ya kwanza tangu kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu baada ya kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na majeraha alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Yusuph Mhilu, wakati huo huo Kagera Sugar ilifanya mabadiliko alitoka Atupele Green na kuingia Omary Daga.

Mabadiliko hayo yalionekana kuiongezea Yanga nguvu kwa kiasi kikubwa, kwani dakika ya 77, Martin aliifungia bao la pili baada ya kuunganisha krosi makini ya Chirwa.

Bao hilo liliilazimisha Kagera Sugar kufanya mabadiliko mengine dakika ya 80, alitoka Japhet Makarai na kuingia Peter Mwalyanzi.

Hata hivyo, Yanga ndiyo iliyofaidika na mabadiliko hayo kwa kufanikiwa kuandika bao la tatu dakika ya 88 baada ya beki wa Kagera Sugar, Juma Shemvuni, kujifunga akiwa katika harakati za kuokoa mpira wa krosi iliyopigwa na Mhilu.

Dakika ya 89, Yanga ilifanya mabadiliko alitoka Martin na kuingia Juma Mahadhi, huku beki Haji Mwinyi akionyeshwa kadi ya njano dakika ya 90 akidaiwa kuchelewesha mpira kwa makusudi.

Dakika 90 za pambano hilo zilimalizika kwa Yanga kutoka kifua mbele kwa  ushindi wa mabao 3-0.

Kikosi Yanga: Youthe Rostan, Hassani Kessy, Mwinyi Haji, Said Juma, Kelvin Yondani, Pato Ngonyani, Emmanuel  Martin, Thaban Kamusoko, Pius Buswita, Obrey Chirwa na Ibrahim Ajib.

Kikosi Kagera Sugar: Ramadhan Chalamanda, Mwaita Gereza, Adeyun Salehe, Juma Shemvumi, Mohamed Fakhi, George Kavila, Japhet Makarai, Ally Nassoro, Atupele Green, Ally Mashaka na Japhary Salum.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles