33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MWANAFUNZI ‘ALIYETEKWA’ ASAFIRISHWA USIKU KWENDA DAR

Na FRANCIS GODWIN -IRINGA


JESHI la Polisi Mkoa wa Iringa,  limemsafirisha usiku mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Abdul Nondo (24), aliyedai kutekwa na watu wasiojulikana hadi Makao Makuu ya  jeshi hilo kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa mahojiano zaidi.

Kamanda wa Polisi  Mkoa wa Iringa, Juma Bwire, alimweleza mwandishi wa  habari hizi  jana  kuwa  mwanafunzi  huyo amesafirishwa usiku na jana asubuhi alikuwa tayari ofisi ya DCI  kwa  mahojiano  juu ya madai yake ya  kutekwa.

“Baada ya polisi ngazi ya mkoa  kumaliza kazi yetu ya kumhoji na kwa  kuwa alisema alitekwa Dar es Salaam   tulilazimika kumsafirisha  hadi  Dar es Salaam  kwa ajili ya kuhojiwa na  DCI  pamoja na kuonyesha  eneo ambalo   walimteka.”

Kamanda Bwire alisema kwa sasa  wanamwomba  mtu aliyejitambulisha  kwenye mitandao kwa jina la Jonathan  Kwepe, ili kulisaidia Jeshi la Polisi kujua  ukweli zaidi wa tukio hilo  kwa  kuwa inaonyesha alisafiri  naye na  walikaa siti  moja.

Pamoja na kumwomba Kwepe  kujitokeza pia alitoa rai kwa wananchi  wengine wenye taarifa zaidi za Nondo, kujitokeza ili kusaidia kupata ukweli wa  jambo hilo.

Nondo ambaye ni Mwenyekiti wa  Mtandao wa wanafunzi Tanzania (TSNP), alidai  kutekwa na  watu  wasiojulikana kabla ya Machi 7, mwaka  huu na taarifa  zake zilianza kusambaa katika mitandao ya  kijamii kabla ya  jioni  kuripotiwa  kupatikana  akiwa  hajitambui  na  kwenda  kituo cha polisi Mafinga Wilaya ya Mufindi  mkoani  Iringa kuripoti kutekwa kwake.

Hata  hivyo, taarifa ya Jeshi la Polisi  Mkoa wa Iringa iliyotolewa Machi 8 saa 4.45 na Kamanda wa Polisi Mkoa, ilidai  kuwa  Nondo  alipatikana Machi 7, mwaka huu saa 1 asubuhi baada ya kufika Kituo kidogo cha polisi Mafinga   Wilaya ya Mufindi na kueleza kuwa alitekwa na watu wasiojulikana.

Tayari Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limefungua jalada la uchunguzi ili  kubaini  ukweli  kama  alikuwa ametekwa na  kama kweli wahusika  watasakwa na kama  si kweli sheria  itachukuwa mkondo  wake dhidi ya Nondo.

Taarifa za kutekwa kwa Nondo ziliwalazimu wanafunzi wenzake kuripoti  Kituo Kikuu  cha Polisi jijini  Dar es  Salaam  na  kupewa  RB namba; UD/RB/1438/2018.

Kwa mujibu wa wanafunzi wenzake kabla ya Nondo kudaiwa kutekwa aliandika ujumbe mfupi kupitia simu yake ya kiganjani uliosomeka  ‘Iam at High Risk’ akiwa na maana yuko hatarini  na baada ya hapo hakupatikana tena hadi alipoonekana Mafinga.

Mwandishi wa habari  hizi jana alifika  katika  Hospitali ya Wilaya ya  Mafinga kutaka kujua kama Nondo alipatiwa matibabu ambapo Mganga  Mkuu wa Hospitali  hiyo, Dk. Innocent Mhagama, alisema jina la mwanafunzi huyo halimo kwenye kumbukumbu ya wagonjwa  waliofika hospitalini hapo.

MTANZANIA Jumamosi jana liliwasiliana na DCI, Robert Boaz, kwa njia ya simu ili kufahamu kama amempokea Nondo ambapo aliomba atafutwe kwa njia ya ujumbe mfupi kwani muda huo saa 11 jioni alikuwa kwenye kikao.

Alipotumiwa ujumbe mfupi, DCI Boaz hakujibu, gazeti hili linaendelea kufuatilia tukio hili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles