Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
BAADA ya kutolewa mapema katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, uongozi wa Klabu ya Yanga umewataka mashabiki wake wasiwe wanyonge kwani kikosi kizuri wanacho na wana uhakika wakufanya vizuri Ligi Kuu Tanzania Bara wakianzia mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba.
Yanga ambayo imeondolewa na River United ya Nigeria kutokana na kupoteza mechi zote za nyumbani na ugenini, inatarajia kukutana na Simba Jumamosi hii Septemba 25, 2021 katika mchezo wa Ngao ya Jamii ikiwa ni ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu 2021/2022 kwenye Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya mchezo wa jana waliofungwa 1-0 na Rivers United nchini Nigeria, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Haji Mfikilwa amesema timu imecheza vizuri tofauti na ilivyokuwa nyummbani na wachezaji walipambana.Â
Amesema wanachoangalia kwa sasa ni majukumu yaliyopo mbele na wanaridhika kuwa wana kikosi kizuri kinachohitajikia ni muunganiko wa timu.
“Tunajua mashabiki wameumia, hata sisi tumeumia lakini wakati mwingine ni lazima upate machungu ili uweze kwenda mbele zaidi, uwape wachezaji muda na mwalimu.
“Kwa sasa tunaendelea na maandalizi ya mechi yetu ya ngao ya jamii, ni mchezo mkubwa kwetu, tutaendeleza pale tulipoishia. Tumepata hasara ya kuondolewa michuano ya Kimaifa lakini faida tumepata ni michezo iliyotupa mazoezi.
“Sisi kama uongozi tunaridhika tuna kikosi kizuri na tunaondoka kifua mbele kwa sababu tumepambana, wachezaji wamejitoa. Tunajiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii, ni mchezo mkubwa kwetu,” amesema Mfikilwa.
Kwa upande wake Ofisa Habari wa timu hiyo, Hassan Bunguli amesema wapinzani wao walikuwa na mbinu ya kuwatoa mchezo kutokana na baadhi ya wachezaji kutajwa kuwa na Covid-19.
“Mechi iliyopo mbele yetu ni dhidi ya watani ya Ngao ya Jamii, tunakwenda kupambana, mashabiki wetu wasiwe wanyonge kabisa, kikosi tunacho kizuri,” amesema Bumbuli.